Friday, October 23, 2015

Rekodi mpya mikoa saba Uchaguzi Mkuu

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Kwa miaka 20, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikipeta kwenye mikoa saba, lakini kukua kwa upinzani katika kipindi hicho au chama hicho tawala kuendelea kutamba itakuwa ni rekodi mpya.

Mikoa hiyo haijawahi kuwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani tangu siasa za vyama vingi zirejeshwe nchini mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo huo kufanyika mwaka 1995.

Mikoa hiyo, Morogoro, Dodoma, Mtwara, Pwani, Ruvuma, Tabora na Tanga haijawahi kuwapa wapinzani ubunge na hivyo kuendelea na hali hiyo kutaweka rekodi na wapinzani wakishinda itakuwa rekodi pia.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa upinzani uliongezeka nguvu mwaka huu, umefanya ushindani kuwa mkubwa na kuweka uwezekano wa chama chochote kilichosimamisha wagombea kuweza kushinda.

“Mwaka huu tumeshuhudia upinzani mkali Dodoma na hii hatukuiona miaka ya nyuma,” alisema mkazi wa Dodoma, Yahya Hussein aliyehojiwa na Mwananchi kuhusu hali inavyoendelea.

“Watu wanahitaji mabadiliko na katika mazungumzo ya watu wengi unasikia wanasema mwaka huu wanataka upinzani uchukue jimbo hasa hili la Dodoma mjini.”

Dodoma

CCM imemsimamia Anthony Mavunde, mtoto wa kada maarufu wa chama hicho na meya wa zamani wa Dodoma, Peter Mavunde, kugombea ubunge wa Dodoma Mjini.

Mavunde anachuana vikali na mgombea wa Chadema, Benson Kigaila, ambaye uchunguzi unaonyesha amejijenga kwenye maeneo ya mjini.

Nguvu ya Kigaila pia inatokana na uamuzi wa vyama vinne vya Chadema, NLD, NCCR Mageuzi na CUF kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja chini ya ushirikiano unaoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Dodoma, ambayo imeandikisha wapigakura 1,071,383, ina majimbo 10 ya Dodoma Mjini, Bahi, Chilonwa, Mtera, Kongwa, Mpwapwa, Kibakwe, Chemba, Kondoa Mjini na Kondoa Vijijini, lakini Dodoma Mjini ndilo linaloonekana kuwa hatarini.

“Kwa mara ya kwanza tutashuhudia wapinzani wakichukua jimbo katika mkoa wa Dodoma kutokana na wananchi kutaka mabadiliko,” alisema mkazi mwingine wa Dodoma, Elias Eliabu.

Lakini, Asnath Mushi alisema kuwa hakuna mtu anayeweza kuutabiri uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa mpaka sasa hakuna anayeweza kujihakikishia ushindi kwa asilimia mia.

Morogoro

Mkoa wa Morogoro ambao una majimbo 11 na wapigakura milioni 1.3 umekodolewa macho na vyama vyote.

Upinzani ulianza kujikita kwenye baadhi ya majimbo hayo tangu mwaka 2005 na 2010 baada ya wagombea wa Chadema na CUF kuanza kujitokeza kuwania ubunge.

Kwa mara ya kwanza, Chadema imesimamisha wagombea kwenye majimbo yote, likiwamo la Mikumi ambalo ushindani ni mkubwa.

Msanii maarufu wa rap, Joseph Haule, maarufu kama Profesa Jay, amesimamishwa na Chadema kuwania ubunge Mikumi na amevuta watu wengi kwenye mikutano yake, akipambana vikali na mgombea wa CCM, Jonas Nkya.

ACT Wazalendo imemsimamisha Onesmo Mwakyombo, ambaye anafuata kwa ushindani.

Mkazi wa Morogoro, Amandusi Kaisi alisema: “Lile jimbo kwa muono wangu anapewa nafasi mgombea wa Chadema. Amekuwa na wafuasi wengi, ila hiyo haiondoi ukweli kwamba katika uchaguzi chochote kinaweza kutokea.”

Hali si shwari pia Kilombero ambako mgombea wa CCM, Aboubakar Asenga anachuana vikali na Abdul Mteketa, ambaye alishinda ubunge mwaka 2010 kwa tiketi ya CCM, lakini sasa amehamia CUF.

Kilombero ni moja ya majimbo ambayo Ukawa hawakukubaliana na hivyo Chadema imemsimamisha Peter Lijualikali.

“Majimbo yote mawili ya Wilaya ya Kilombero yana upinzani mkali na kwa ninavyoona, moja lazima liende kwa wapinzani,” alisema mkazi wa Ifakara, Agnes Msambira.

Katika jimbo la Mlimba, mchuano upo kati ya waliokuwa wabunge wa viti maalumu mkoa wa Morogoro kwa vyama tofauti; Susan Kiwanga (Chadema) na Mchungaji Dk Getrude Rwakatare (CCM).

Ushindani pia uko katika jimbo la Morogoro Kusini linalowaniwa na wagombea na wanne, Mbena Prosper (CCM), Dk Hongo Hamimu (ACT-Wazalendo), Noge Mwegallawa TLP na Chanzi Suleiman Zuberi wa Chadema.

Mtwara

Mkoa wa Mtwara, wenye wapigakura 728,981, wakazi wanasema kilichofanya wapinzani wasichaguliwe ni ukosefu wa elimu ya uraia kwa wananchi, lakini mwaka huu hali inaweza kubadilika.

Mkazi wa Mtwara, Dadi Likinde alisema tangu mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa ahamie upinzani kumekuwa na mwamko mpya wa kisiasa unaotishia baadhi ya majimbo kuchukuliwa na upinzani.

“Tangu vurugu za gesi zitokee miaka mitatu iliyopita watu walianza kuichoka CCM. Lowassa naye ndio kabisa amebadili mwelekeo wa siasa hapa Mtwara,” alisema.

Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Mtwara, Ibrahim Mandoa alisema ana imani yapo majimbo yatakayochukuliwa na upinzani hasa baada ya vyama vinne kuunda Ukawa.

Tabora

Mkoa wa Tabora umefanikiwa kumtoa mbunge mmoja tu wa upinzani, Dk Jacob Msina aliyetwaa Jimbo la Urambo akimuangusha Samuel Sitta mwaka 1995.

Kuanzia mwaka 2000, Tabora ambayo imeandikisha wapigakura milioni 1.1, haijapata mbunge wa upinzani.

Lakini mwaka huu, CCM inaonekana kuwa na wakati mgumu katika majimbo ya Kaliua na Tabora Mjini. Wakati wa Kaliua wanadai kuchoshwa na mbunge wao, Profesa Juma Kapuya, ambaye pia amekuwa akieleza kwenye kampeni zake kuwa ushindi ni lazima.

Kada huyo wa CCM anapambana na Magdalena Sakaya wa CUF.

Upinzani katika jimbo hilo ni mkubwa kiasi cha wanawake kuzomeana mitaani.

Katibu wa CCM wa wilaya, Rehema Adam alikiri kuwapo kwa tabia hiyo na kuwataka wanaozomewa kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola.

Katika Jimbo la Tabora Mjini hali ni tete kutokana na CCM kushindwa kufanya kampeni za nguvu kama ilivyo kwa vyama vya CUF na ACT Wazalendo. Hali hiyo imesababishwa na makundi yaliyotokana na kuenguliwa kwa Aden Rage katika kura za maoni.

“Kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Tabora Mjini zilisimama kwa muda huku sababu za kusimama kwake zikiwa hazielezwi kwa wananchi,” mkazi wa Isevya, Juma Bakari alisema.

Kampeni za mgombea wa CUF, Peter Mkufya na mgombea wa ACT Wazalendo, Mohamed Mapalala zinaendelea vizuri. Mkufya alisema amezunguka na kuzungumza na watu mbalimbali katika kata zote na ana matumaini ya kushinda ubunge.

Tanga

Tanga imeibukia kuwa mkoa unaongaliwa kwa karibu na vyama vyote, hasa kutokana na idadi yake kubwa ya wapigakura. Ikiwa na wapigakura 1,009,755, Tanga inaangaliwa kama moja ya mikoa saba iliyoangaliwa kwa karibu na viongozi wa vyama vyote na hivyo inaweza kuvunja mwiko wa kutotoa wapinzani.

Wabunge wa upinzani waliowahi kupatikana katika mkoa huo ni wale wa viti maalumu ambao ni pamoja na Amina Mwindau, (2010-2015), Nuru Bafadhili (2005-2010) na Adelastela Mkilindi (2000-2005).

Mwaka huu, CCM imemsimamisha Omari Nundu kugombea Jimbo la Tanga, wakati CUF imemsimamisha Mussa Mbarouk chini ya Ukawa.

Katika Jimbo la Pangani mgombea wa CCM, Jumaa Awesso anapambana na Amina Mwindau wa CUF.

Upinzani huo unatokana na ukweli kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mwindau ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu kupitia CUF alitumia muda mwingi kujiimarisha kisiasa.

Katika jimbo la Korogwe Mjini, Mary Chatanda anaonekana kutofanya vyema kutokana na wapinzani wake kusema si mwenyeji.

Ruvuma

Hali mkoani Ruvuma pia ni tete kwa chama tawala, hasa katika Jimbo ya Tunduru Kaskazini linalowaniwa na Ramo Makani (CCM) na Dastan Kambili (CUF). Mgombea wa CUF ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda.

Mmoja wa viongozi wa CCM, Seleman Abdallah alisema bado hali si shwari katika jimbo hilo kwa upande wa CCM kwani Injinia Ramo ameshindwa kuvunja makundi yaliyoibuka bada ya uchaguzi wa ndani.

Mbali na Tunduru Kaskazini, jimbo jingine lenye upinzani mkali ni Songea Mjini linalowaniwa na Leonidas Gama (CCM) na Joseph Fuime (Chadema) bila kusahau Jimbo la Mbinga Mjini.

Pwani

Mkoani Pwani kuna majimbo tisa ya uchaguzi ambayo ni Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Chalinze, Bagamoyo, Kibiti, Rufiji, Mafia, Kisarawe na Mkuranga, kukiwa na wapigakura 697,533.

Baadhi ya wakazi wanasema majimbo wanayoona yanaweza kuchukuliwa na upinzani ni Bagamoyo, Mafia, Kibaha Vijijini na Kibaha Mjini. “Hata kama viongozi wetu wanasema tutashinda mchana kweupe, hali si shwari kabisa. Upinzani ni mkali mno, hasa baada ya wazee wenzetu wa siku nyingi kung’atuka CCM,” alisema Yusuf Mohamed.

Habari hii imeandikwa na Rachel Chibwete, Lilian Lucas, Haika Kimaro, Robert Kakwesi, Burhani Yakub, Joyce Joliga na Julieth Ngarabali.

No comments: