ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 24, 2015

WANANCHI WA NGORONGORO WANAKABILIWA NA UHABA WA MAJI

Wananchi wa kijiji cha Naiyobi wilaya ya Ngorongoro wakichota maji ambayo hutumia na mifugo kijiji hicho kinakabiliwa na uhaba wa maji.

Na Ferdinand Shayo, Arusha.

Wananchi wa Kijiji cha Nayobi  kilichopo tarafa ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wamelalamikia kero ya uhaba wa maji inayowasababishia kukesha kwenye bomba la kijiji kwa takribani siku tatu wakisubiri maji jambo linalopelekea shughuli za kijamii na kiuchumi kusimama kwa muda mrefu na kinamama kutembea umbali mrefu wakitafuta huduma hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa kwa muda mrefu wamekua wakiteseka kupata huduma za maji huku kinamama wajawazito wakijifungulia bombani apo baada ya kukaa kwa muda wakitafuta maji huku wengine wakilazimika kukesha na watoto wadogo .

Wanakijiji Daniel Sereki  na  Rehema Laizer  na wamesema kuwa kwa sasa wanakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji pamoja na chakula na hata pale wanapopata chakula hukosa maji ya kupikia chakula hicho na kuziacha familia zao zikitaabika kwa njaa.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji Naiyobi  Meleji  Sikoni amesema kuwa kwa muda wa miaka 20 wamekua wakikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji hivyo ameiomba serikali na mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  iwasaidie kutatua tatizo hilo sugu linalowaathiri  wananchi wengi.

Mgombea Ubunge Jimbo la Ngorongoro Wiliam Olenasha  ameeeleza kisikitishwa na wananchi wanaoteseka kwa kero ya maji ambayo hushirikiana na mifugo katika matumizi yake hivyo ameaidi kutatua kero hiyo pindi atakapopata ridhaa ya kuongoza wilaya hiyo.

Wilaya ya Ngorongoro inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji pamoja na chakula hasa katika kipindi hiki cha kiangazi ,juhudi zinahitajika kwa upande wa serikali na Mamlaka ya Ngorongoro ili kuweza kuwanusuru wananchi na baa la njaa pamoja na uhaba wa maji.

No comments: