Azam FC
Simba SC
TIMU ya Azam FC imewatangazia hali ya hatari Simba katika mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara, itakayochezwa Desemba 12 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam imetamba kuinyuka Simba katika mchezo huo, ambapo hadi sasa vinara hao wa ligi kuu wamefikisha pointi 25, wapinzani wao hao wakishika nafasi ya nne wakiwa na pointi 21 katika mechi tisa walizocheza kila mmoja.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd, alisema maandalizi yao kwa mchezo huo yanaendelea vizuri kwani wengine wapo kwenye timu zao za taifa zinazoshiriki michuano ya Chalenji nchini Ethiopia.
Alisema wapinzani wao waingie uwanjani wakijua kuwa wanakutana na timu yenye uchu wa kutwaa ubingwa hivyo hawapo tayari kuwachekea na kuwapa pointi ambazo Azam inazihitaji.
“Tunaijua Simba ni timu ya aina gani, hivyo hatuidharau lakini pia nao waje wakijua wanaenda kukutana na kikosi kipi kwani uchu tulionao ni wa kutwaa ubingwa, hatupo tayari kuona tunapoteza mechi yoyote iliyopo mbele yetu,” alisema.
Akizungumzia usajili katika kikosi hicho kipindi hiki cha dirisha dogo litakalofungwa Desemba 15 mwaka huu, alisema watamsajili mchezaji yeyote na kwa gharama yoyote iwapo benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Stewart Hall likimhitaji.
Mtanzania
No comments:
Post a Comment