Advertisements

Sunday, November 29, 2015

Papa Francis kumtangaza Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa mtakatifu.



NA MWANDISHI WETU
ZIARA ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis nchini Uganda imetajwa kuwa itafufua mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa mtakatifu.

Kwa mujibu wa mtandao wa ETN wa nchini Uganda, ziara hiyo ya kitume ya Papa Francis itamfikisha katika eneo la Namugongo ambalo mashahidi wa imani ya dini ya Kikristu walichomwa moto.

Ni katika eneo hilo la Namugongo ambako Hayati Nyerere alitangazwa kuwa Mwenyeheri huku mchakato wa kumtangaza mtakatifu ukiwa ulianza miaka tisa iliyopita.

Namugongo ndiko ambako pia waumini wa dini ya Kikristu wa Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani hufika kuhiji.

Taarifa ya ETN imeeleza kuwa ziara ya Papa Francis Namugongo itasaidia kufufua mchakato uliodumu kwa miaka tisa sasa wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa kuwa mtakatifu.

Tayari mjane wa Hayati Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere yuko nchini Uganda ambako amekwenda kujumuika na waumini wengine wa dini ya Kikristu kumpokea na kushiriki ibada itakayoongozwa na Papa Francis.

ETN imemkariri Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, akisema kuwa mchakato wa kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu umetokana na mchango wake wa kuhimiza heshima na usawa kwa binadamu ambao aliutoa wakati akiwa kiongozi.

Kwa mujibu wa ETN, Rais Museveni amesifu mchango wa Hayati Mwalimu Nyerere ambao haukuwa tu wa kuunganisha Watanzania bali alifanya kazi kwa kujali utu wa Waafrika.

“Hayati Julius Nyerere alikuwa mwanaharakati wa Afrika ambaye alimpenda Mungu na alijali utu, aliwaunganisha Watanzania wa dini zote na alisaidia ukombozi wa mataifa mengine ya Afrika kama vile Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika Kusini na Uganda,” alisema Museveni.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu hilo, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema mchakato wa kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu unaendelea vizuri.

Alisema suala la kuendesha mchakato huo ni jukumu la Tanzania na si Uganda hivyo jina la Hayati Mwalimu Nyerere linaweza kuibuka katika ziara ya Papa nchini Uganda kwa kutajwa tu, kwa sababu Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, amekuwa na mazingira ya karibu na familia ya Hayati Mwalimu Nyerere.

“Jukumu la kuendesha mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa kuwa Mtakatifu ni letu na linaendelea vizuri. Kuna mambo mengi ya kuchunguzwa mpaka mtu kutangazwa kuwa mtakatifu, inawezekana Papa akamzungumzia Mwalimu kwa sababu ya Rais Museveni mara kwa mara ameonyesha kuguswa na mwenendo wa mchakato huo,” alisema Askofu Kilaini.

Papa Francis aliwasili nchini Uganda jana jioni saa 4:50 na kulakiwa na Rais Museveni na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo.

Kwa mujibu wa ziara yake nchini humo iliyotolewa na Kanisa Katoliki la Uganda leo anatarajiwa kufanya ziara ya kitume katika miji ya Munyonyo, Nikiyanja, Nalukolongo, Namugongo, Kalolo na Rubaga na kesho atamaliza ziara yake nchini humo na kusafiri kwenda nchini Afrika ya Kati (CAR).

Taarifa kutoka nchini Uganda zinaeleza kuwa ulinzi umeimarishwa na Serikali imeandaa wahudumu wa afya 400 na magari 38 ya kubebea wagonjwa ambayo yamepelekwa maeneo yote ambayo Papa atayatembelea.

Papa Francis atakuwa Papa wa tatu kutembelea taifa hilo ambapo mwaka 1969, Papa Paul VI alitembelea nchi hiyo akifuatiwa na Papa Paul II mwaka 1993.

Kampeni za urais zasimama

Katika hatua nyingine wagombea urais wa vyama vyote wamelazimika kuahirisha mikutano yao ya kampeni kwa ajili ya kupisha ziara ya Papa Francis nchini humo.

Rais Museveni ambaye anawania urais kwa muhula mwingine, aliwaambia wafuasi wa chama chake kuwa atamuomba Papa asaidie kutangaza utalii wa taifa hilo.

Akemea ukabila na rushwa nchini Kenya

Awali kabla hajaondoka nchini Kenya, Papa Francis alihutubia maelfu ya vijana katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi ambapo aliwahimiza vijana wa taifa hilo wasijihusishe na ukabila.

Alisema vijana wanaweza kuchangia katika kukabiliana na changamoto za ukabila ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya mataifa ya Afrika.

Aliwashauri viongozi wa Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu na ajira kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuwazuia kujiingiza katika makundi yenye itikadi kali za kigaidi.

Kabla ya kuhutubia vijana katika Uwanja wa Kasarani, Papa Francis, alitembelea Mtaa wa Kangemi ambako wanaishi watu masikini na kukemea dhuluma ya huduma bora ambazo wanatakiwa wapatiwe masikini.

“Ninafahamu kuhusu tatizo kubwa linalosababishwa na wawekezaji wasio na sura ambao hujitwalia ardhi na hata kujaribu kunyakua viwanja vya kuchezea watoto wenu shuleni. Hili ndilo hufanyika tunaposahau kwamba Mungu aliwapa watu wote ardhi waitumie kwa maisha yao bila kutenga au kupendelea yeyote,” alisema Papa Francis.

Mtanzania

No comments: