TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Kwa
mujibu wa Sheria ya Sikukuu za Kitaifa
(The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa
mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe
za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi. Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga
tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku
hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini,
sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi
kwa vitendo.
Aidha, kwa
kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo
yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya
sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na
kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda
vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.
Ieleweke
kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya
uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi
zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
23
Novemba, 2015
3 comments:
Safi sana mh. Sisi watanzania ni wavivu sana sasa ni kuchapA kazi. Ahsante sana. Tufanye usafi
Safi sana ...na naomba afute mbio za mwenge pia...hazina maana wala faida yyote zaidi ya ulaji wa pesa za serikali tu
Mchakamchaka chinja
Post a Comment