KAMISHNA wa Bajeti wa Wizara ya Fedha, John Cheyo, amesema fedha za msaada za Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) kutoka nchini Marekani zinatarajiwa kupatikana Juni, mwakani.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, alipozungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku moja baada ya baadhi ya magazeti, likiwemo gazeti hili, kuripoti kuhusu barua ya MCC ya Novemba 19, mwaka huu, iliyoandikwa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, ikionya kuwa mgogoro wa Zanzibar na sheria ya uhalifu wa mtandao vinaweza kuathiri vigezo vya kuiwezesha Tanzania kupata msaada wa zaidi ya Sh trilioni moja.
Alisema kikao cha Bodi ya MCC kitakachofanyika Desemba 17, mwaka huu kitakuwa na matokeo mazuri juu ya kupatikana kwa fedha hizo na kuwa kila kitu kinakwenda vizuri.
“Vigezo vilivyotajwa katika barua hiyo vinafanyiwa kazi na fedha hizo zinatarajiwa kupatikana ifikapo Juni, mwakani kwa ajili ya kutumika katika bajeti ya 2016/2017.
“Pamoja na hilo, Cheyo alipongeza mikakati ya Rais John Magufuli ya kubana matumizi, kwa kuwa itasaidia katika mpango wa taifa wa elimu kutolewa bure.
“Kitu anachofanya Rais ni kizuri katika kusaidia mkakati wa elimu kuwa bure utakaofanyika kuanzia mwakani, kwa kuwa hapakuwa na bajeti hiyo,” alisema Cheyo.
Alisema mwelekeo wa bajeti kuanzia Julai hadi Oktoba, mwaka huu ni mzuri kwa kuwa asilimia 97 imekamilika.
Alisema suala la kupiga marufuku matumizi mbalimbali yasiyo ya lazima ni jambo zuri litakalosaidia kupata huduma kwa gharama nafuu.
Alipotakiwa kutaja ni kiasi gani cha fedha kilichookolewa kutokana na mikakati ya kubana matumizi ya Magufuli, alisema jambo hilo linahitaji muda kutolea ufafanuzi na si la siku moja.
“Hata hivyo, kujua ni fedha kiasi gani alizofanikiwa kuziokoa si jambo la siku moja kwa kuwa unatakiwa kupitia kila wizara, hivyo inahitaji wiki moja kupata hesabu zote,” alisema Cheyo.
Katika hatua nyingine, alikanusha madai ya Serikali ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kukomba fedha Hazina.
Alisema jambo hilo halina uhalisia kwa kuwa hadi sasa Serikali imeweza kumudu majukumu yake bila kutetereka, ikiwamo kulipa mishahara ya wafanyakazi, gharama za uchaguzi na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
“Suala la Hazina kutokuwa na fedha si la kweli, kwa kuwa fedha zinaingia na kutoka kila siku na kama kweli amekomba tusingeweza kumudu gharama zote hizo. Hazina inazo fedha za kutosha na tunajivunia kufanya uchaguzi wa mwaka huu, kununua mashine za BVR kwa kutumia fedha za Watanzania bila kutegemea msaada wowote kutoka nje ya nchi na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka huu,” alisema Cheyo.
Alisema serikali imeendelea kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa bomba la gesi lililokamilika hivi karibuni, vinu vya kuchakata gesi na ujenzi wa barabara nchini.
Alisema mfumo wa serikali wa bajeti unaiwezesha serikali kupanga vipaumbele vya matumizi kulingana na bajeti ilivyopangwa, ambapo fedha zinazokusanywa kupitia mfuko mkuu wa serikali ndizo hutumika.
Cheyo alisema bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa kipindi cha mwaka 2015-2016 ni Sh trilioni 22.5 na bajeti hiyo inatengenezewa mpango wa makusanyo na matumizi kwa kulipia mishahara ya wafanyakazi na miradi mbalimbali iliyoidhinishwa.
Mtanzania
No comments:
Post a Comment