Advertisements

Sunday, November 29, 2015

‘Wananchi onesheni mali za maofisa wa TRA’

‘Wananchi onesheni mali za maofisa wa TRA’
WANANCHI wamehamasishwa kujitokeza kusaidia uongozi wa Rais John Magufuli, kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria, vinavyofanya uchunguzi kuhusu mali za maofisa na vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ushauri huo kwa wananchi umetolewa baada ya Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, kuagiza mali za maofisa waliosimamishwa kwa upotevu wa zaidi ya Sh bilioni 80 za kodi, baada ya kupotea kwa makontena 349 yaliyopaswa kutoa mapato hayo ya Serikali.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema hatua hiyo ni vema izingatie misingi ya haki na uwajibikaji kwa kushirikisha wananchi, kwa kuwa wanajua yanayoendelea kwa watendaji wa mamlaka hiyo.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu, kwani wanajua mbinu zote wanazotumia maofisa hao katika ukwepaji kodi, makontena yanavyotoroshwa na mali walizonazo.

Ally alisema wananchi wanajua majengo makubwa wanayomiliki watendaji hao, magari na mali zingine kwa kuwa baadhi yao ni vijana wadogo waliosomeshwa na Serikali kwa kutumia fedha za umma kwa lengo la kufanya kazi, lakini wamegeuka na kudhulumu watu.

Mhadhiri huyo alishauri uchunguzi unaofanyika uwe wa kina na mapana na washiriki wote, wakiwemo watumishi wa umma na wafanyabiashara, wachukuliwe hatua kwa kuwa huo ni mtandao unaohusisha watu wengi.

Alisifu hatua hiyo ya Serikali, akisema itaongeza nidhamu na heshima kwa Serikali na kuongeza kuwa watendaji hao wasipokuwa na maelezo ya kutosha ya mali walizonazo kwa kuzingatia mshahara wao na muda waliofanya kazi, ni sahihi mali zichukuliwe kwa kuzingatia sheria. Mbali na watumishi hao, Ally alishauri na wafanyabiashara watakaobainika kushirikiana na watumishi hao, wachukuliwe hatua pia kwa kuwa nao ni wahusika.

“Hawa wafanyabiashara wakubwa wametumika kuwarubuni watumishi wa umma, nao warejeshe kodi waliyokwepa na ikiwa watabainika kuwa na kosa la jinai, wafikishwe mahakamani na kushitakiwa ikibidi na mali zao zifilisiwe,” alisema.

Majina mengine Naye, Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alitaka maofisa hao wa TRA wachunguzwe kwa kina kwani watu kama hao mali zao nyingi wanaziandika kwa majina mengine ili wasijulikane.

Alisema hatua ya Serikali kuagiza mali za maofisa hao zichunguzwe kama zinaendana na kipato cha mtumishi wa umma ni nzuri, kwani mara nyingi watu walikuwa wakilalamika kuwepo kwa watumishi wanaojitajirisha kwa kukwepa kodi. Kwa mujibu wa Profesa Bana, wafanyakazi wa TRA wanalipwa vizuri zaidi katika sekta za umma kwa lengo la kuwatosheleza, ili wasishawishike kuingia katika ukwepaji kodi utaratibu ambao ni mzuri, lakini wameshindwa kutumia vema fursa hiyo ya kuthaminiwa na Serikali.

Alitaka taasisi za udhibiti wafanye kazi zao, badala ya kusubiri Rais au Waziri Mkuu kugundua masuala mazito kama hayo, huku akitaka wananchi kusaidia kubaini mali walizonazo na kuwachukulia hatua.

Akizungumzia wafanyabiashara wanaomiliki makontena yaliyokwepa kulipa kodi, Profesa Bana alisema haitoshi kuwataka kulipa kodi, bali ni lazima baada ya kulipa, waadhibiwe kwani wao ndiyo walioharibu mifumo ya ukusanyaji kodi ya Serikali. Profesa Bana alisema baadhi ya wafanyabiashara hao, wamekuwa wakiweka mitandao inayotengeneza mifumo ya kushawishi watendaji wa Serikali, ili wakwepe kulipa kodi.

Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu alisema hatua hiyo inaonesha kusonga mbele katika mapambano ya ufisadi, lakini inatakiwa kuwa endelevu na kuacha kuwa sehemu ya matukio.

Katibu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya, alisema anaunga mkono maofisa hao kuchunguzwa na kutaka kuwe na mtindo wa kuchunguza mali za watendaji wote wa sehemu nyeti serikalini.

Mgaya alisema ni vema kufahamu watendaji hao, wanapata wapi fedha za kujenga majengo ya fahari, wakati hawana mkopo ili kuleta usawa kwa kupata kitu alichofanyia kazi na si nje ya utaratibu.

Aliitaka Serikali kuendelea kuchunguza taasisi na sekta nyingine za umma, kwani bado zipo sehemu nyingine zenye matatizo kama hayo. Akizungumzia wenye makontena, Mgaya alisema ni vema Serikali ifanye hesabu upya za wafanyabiashara wote wanaokwepa kodi.

Alisema ni vema wafanyabiashara wote wanaoingiza vitu kutoka nje, wafanyiwe ukaguzi wa vitu walivyoingiza kwa miaka mitano iliyopita na kodi waliyolipa na kama wanadaiwa, walipe, lakini wakishindwa mali zao ziuzwe na kufilisiwa kisheria, kwani kodi hizo zitasaidia kutoa elimu bure na kufanya nchi kuendelea kiuchumi.

Habari Leo

No comments: