Advertisements

Saturday, November 28, 2015

Makontena 31 ya magogo yakamatwa bandarini Dar


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
By Julius Mathias, Mwananchi

Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii imekamata makontena 31 yaliyokuwa na magogo ya mninga katika Bandari ya Dar es Salaam yenye thamani ya zaidi ya Sh300 milioni ambayo yalikuwa yanasafirishwa kwenda China.

Usafirishaji wa magogo hayo ambayo taarifa za awali zinaeleza yametoka Zambia, ilipigwa marufuku na Serikali za nchi zote mbili, hivyo biashara yake kuwa haramu.

Akizungumza na waandishi wa habari ambao pia walijionea baadhi ya makontena hayo akiwa sambamba na Balozi Mdogo wa Zambia nchini, Elizabeth Phiri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Adelhelm Meru alisema wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia ofisi za Tunduma inaendelea kufuatilia nyaraka muhimu za kampuni zilizohusika.

“Usafirishaji wa magogo ulishazuiwa chini ya Sheria ya Misitu ya mwaka 1999 na yeyote anayepewa kibali cha biashara ni ile ya mbao na bidhaa nyingine za misitu ambazo zimechakatwa.

“Miti ya magogo haya inapatikana mikoa ya Mbeya na Ruvuma na baadhi ya maeneo nchini. Bado tunaendelea kujiridhisha kama hazikutoka huko,” alisema Dk Meru.

Akifafanua juu ya umuhimu wa rasilimali hizo za asili, alisema kutokana na unyeti wake Serikali iliamua kuilinda miti hiyo ili isipotee na hakuna kibali kinachotolewa kwa ajili ya uvunaji wake, hivyo washukiwa waliokuwa wanayasafirisha kwenda China watakuwa wamevunja sheria za nchi.

Pamoja na changamoto iliyopo, alisema ingawa biashara hiyo haramu inashamiri na kujitengenezea mtandao mkubwa, wizara kwa kushirikiana na TRA imejipanga kukabiliana nayo kwa nguvu zote.

“Miti hii inapatikana Tanzania na Zambia pekee. Kuna dalili ya kuwapo kwa mchezo mchafu,” alisema katibu mkuu huyo.

Licha ya hapa nchini, biashara ya usafirishaji wa magogo hayo imeharamishwa katika mataifa mengine.

Balozi Phiri alisema kuna haja ya kujiridhisha kwa nchi zote, ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya waliohusika.

“Nchi za (Umoja wa Maendeleo Kusini mwa Afrika) SADC zilisaini mkataba wa kuzuia biashara hii kutoka miongoni mwao. Zambia ni mwanachama hivyo kwa kilichotokea hata kama kampuni hizi zilikuwa na vibali vya biashara, bado hii waliyofanya ni haramu. Chochote kitachobainika kwenye nyaraka zao bado wana kesi ya kujibu mahakamani,” alisema.

Kwa kuwa watuhumiwa bado hawajafikishwa mahakamani mpaka sasa, Dk Meru alisema watatajwa baada ya taratibu za kuwachukuliwa hatua za kisheria kukamilika na kukabibidhiwa kwenye mamlaka husika.

No comments: