Advertisements

Monday, November 30, 2015

RAIS MAGUFULI: BILIONI 4 ZA SHEREHE ZA UHURU ZITUMIKE KUPANUA BARABARA YA MWENGE-MOROCO YENYE UREFU WA KILOMITA 4.3

Sehemu ambako utaanzia upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami kufuatia agizo la Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli la kutumia fedha shilingi bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharamia Shamrashamra za siku ya Uhuru Desemba 9, 2015 kutumika kufanya upanuzi wa barabara hiyo. PICHA NA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharamia shamra shamra za siku ya Uhuru ambazo zingefanyika tarehe 09 Desemba 2015, kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.

Tayari fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni nne zimepelekwa kwa wakala wa barabara hapa nchini TANROADS kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, linalopaswa kuanza mara moja.

Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi PATRICK MFUGALE Ikulu Jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli ametaka ujenzi wa barabara hiyo uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika  barabara hiyo
Kujengwa kwa njia hizo kutaifanya barabara ya Morroco hadi Mwenge kuwa na njia tano.

Wakati huo huo, Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba Ikulu Jijini Dar es salaam.

Katika Mazungumzo hayo Prof. Lipumba amempongeza Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kwa kutoa hotuba nzuri ya uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyokonga nyoyo za Watanzania.

Kwa Upande wake Rais Magufuli amempongeza Prof. Lipumba kwa msimamo wake thabiti wa kupinga ufisadi na amemtakia heri katika shughuli zake.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es Salaam.
30 Novemba,2015

3 comments:

Unknown said...

Nampongeza Raisi Magufuli kwa kasi nzuri ya utendaji. Naona mambo yanaanza kunyooka.

Tahadhari:
Katika taaluma za mitandao ya barabara za usafirishaji mijini kuna kitu kinaitwa "THE BRAESS PARADOX". Hiki kitu kinamaanisha kuwa kuongeza au kupanua barabara tu mijini sio lazima kuwa kutapunguza msongamano. Inategemea ni barabara ipi unayoipanua. Saa nyingine unaweza kujenga barabara mpya au kupanua iliopo na msongamano ukazidi kuongezeka badala ya kupungua.

Natumaini Mhandisi Mfugale na timu yake ya TANROADS wamefanya TRANSPORTATION NETWORK ANALYSIS nzuri na kujiridhisha kuwa upanuzi wa barabara hii ni muafaka kitaaluma.

Pongezi kubwa kwao.

RAI: Katika kasi yako mheshimiwa Raisi usiwasahau watu wa mikoani nao.

Anonymous said...

Mheshimiwa Rais Dr. PJM asante kwa uono huo wa haraka na nina Imani tutaweza kuendelea kupunguza maeneo kadhaa yanayoathiri sana shughuli za utendaji na kweli makusanyo ya fedha yakienda sawa na ukajumuisha hata wahisani tunauwezo kabisa wa kujenga barabara ya da Chalinze kuwa na njia nane(8) tutakidhi mahitaji ya mwendo wa haraka. Lingine pamoja na majukumu uliyo nayo, hebu tupia jicho kwenye magari ya polisi yaliyoagizwa mengi sana na awamu ya pili haijawasili ili kuelekeza fedha hizo katika njia nyingineyo kama kuwaomba wauzaji hao kutuletea Ambulance, helkopta au gari za zimamoto.. Asante

Mwanamakole said...

ASANTE BABA KWA MATUMIZI MAZURI YA FEDHA ZA WATANZANIA. MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU MBARIKI RAIS WETU MAGUFULI, MPE MAISHA MAREFU. AMINA