ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 27, 2015

UONGOZI WA JNIA: UKAGUZI MIZIGO YA POSTA SASA KUKAGULIWA MARA YA PILI KABLA YA KUPAKIZWA KWENYE NDEGE

  Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Bw.Injinia Thomas Haule, (katikati), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa uwanja huo leo Ijumaa Novemba 27, 2015. 
Utawala wa uwanja huo ulio chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, umejipanga upya katika kuimarisha ulinzi ambapo kuanzia sasa, vifurushi na mizigo yote kutoka posta itakaguliwa kwa mara ya pili kabla ya kupakiwa ndani ya ndege, ikiwa ni hatua ya kudhibiti vifurushi na mizigo haramu kupenya kwenye ndege. Kushoto ni Kaimu Meneja Usalama wa Uwanja huo, Bw.David Ngaragi, (kushoto) na Afisa Usalama Mwandamizi wa Uwanja huo, Dorice Uhagile. (Picha na K-Vis Media/Khalfan Said).
 Meneja wa Usalama wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Bw.David Ngaragi, akifafanua jambo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari
 Na K-Vis Media
UONGOZI wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaomilikiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, umetangaza leo Ijumaa Novemba 27, 2015 kuwa kuanzia sasa vifurushi na mizigo mingine yote ya Shirika la Posta Tanzania, itakaguliwa kwa mara ya pili kama mizigo mingine yoyote kabla ya kupakiwa ndani ya ndege.
Uamuzi huo umetangazwa na Mkurugenzi wa Uwanja huo, (JNIA), Injinia Thomas Haule, wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa VIP ulioko uwanjani hapo.Alisema, uamuzi huo ni baada ya Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege, TAA, kutoa maonyo kadhaa, kwa Shirika la Posta, kuimarisha ukaguzi wa vifurushi na mizigo itokayo Posta kwa vile imekuwa ikikamatwa na mizigo ambayo ni tofauti na iliyokusudiwa.
Alitaja mizigo hiyo kuwa ni pamoja nabangi, na kwamba, Uholanzi wamekuwa wakilalamika mara kadhaa kuwa wamekuwa wakikamata vifurushi vya Posta vikiwa na mizigo iliyoharamishwa.
"Sisi Kama Mamlaka, wajibu wetu mkubwa ni kuzuia kitu au vitu vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa abiria wawapo ndani ya ndege au ndege yenyewe haviingii ndani ya ndege." Alianza kwa kusema Injinia Haule na kuongeza kuwa, vitu vingine kama madawa ya kulevya, pembe za ndovu, na vingine vingi, , vinashughulikiwa na mamlaka nyingine ambazo zina maafisa wake hapa JNIA wakishirikiana na maafisa wetu.
Hata hivyo makosa yafanywayo na idara Fulani ya serikali yenye afisa wake hapa JNIA, ni wazi kwamba watakaonyooshewankidole ni TAA, alisema na kubainisha kuwa Mamlaka haitavumilia tena uzembe utakaofanywa na taasisi nyingine ya serikali katika kuhakikisha zinatekeleza wajibu wake ipasavyo.
 Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Injinia Thomas Haule, akizungumza kwenye mkutano huo
 Waandishiw a habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, JNIA, Injinia Thomas Haule

No comments: