Zanzibar. Wagombea wa urais wa Zanzibar wa vyama sita, wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN), Ban Ki Moon kumwomba asaidie kutatua mgogoro wa Zanzibar uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Vyama hivyo ni Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, Chaumma, Sau, DP na NRA ambavyo mbali na kumweleza Ban kwamba hawakuridhishwa na kufutwa kwa matokeo na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, pia wamemwomba aingilie kati mkwamo huo.
Katika barua hiyo, vyama hivyo vimesema vimevunjwa moyo na Jecha kufuta matokeo, wakati alitakiwa aendelee na kumtangaza mshindi ili kuepusha machafuko.
Mgombea wa NRA, Seif Ali Iddi alisema wameamua kuandika barua hiyo wakiamini kuwa UN inaweza kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Katibu mkuu wa Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir alisema wamepeleka barua UN kwa sababu hawana imani na Mwenyekiti wa ZEC na hawatambui uamuzi wake kwa kuwa hakukuwa na malalamiko.
Katibu Mkuu wa Chaumma, Ali Omar Juma: “Tunataka matokeo ya Zanzibar yatangazwe, pia tunataka mgogoro huu umalizwe na Jumuiya ya Mataifa iingilie kati na tunaomba kamati ya wataalamu kuchunguza na kupata ushahidi wa uchaguzi wa Zanzibar ulivyokwenda.”
Juma alithibitisha kumwandikia barua Ban iliyotiwa saini na wagombea hao sita wakitaka kuona mgogoro huo unatatuliwa kwa njia za kidiplomasia kwa kuwa wanaamini Serikali ya Tanzania haina nia ya kuutatua.
Vyama hivyo vimemweleza Ban kwamba, uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki na baadhi ya majimbo yalishatangazwa huku waangalizi wa ndani na wa kimataifa wakishuhudia lakini jambo la kusikitisha matokeo yasitishwa.
“Makamu mwenyekiti wakati anatangaza matokeo alisitishwa asiendelee huku tukasikia kupitia televisheni kwamba matokeo yamefutwa na Mwenyekiti Jecha. Sasa tunajiuliza, ni kwa nini yafutwe na mamlaka hayo ya kuyafuta kayatoa wapi?” alihoji Juma.
Barua hiyo iliyopokewa na ofisa wa UN, Alvaro Rodriguez ilisema jambo la kushangaza katika kufutwa kwa matokeo hayo ni kwamba hakuna malalamiko yaliowasilishwa na chama chochote cha siasa ambayo yangeweza kuonyesha kasoro za uchaguzi huo ilhali waangalizi wa ndani na nje wote waliona uchaguzi umekwenda kwa salama, amani na haki.
Wagombea hao walisema Umoja wa Mataifa ndiyo taasisi pekee inayoweza kutatua mgogoro huu na si Serikali ya Tanzania kwa madai kuwa tayari imeshavunja Katiba ya nchi kwa kushindwa kusimamia suala zima la hali iliyojitokeza Zanzibar. “...Inajua kwamba mwenyekiti hana mamlaka lakini kwa sababu ni mtu wao wanamwachia tu.”
Tangu kufutwa kwa matokeo Novemba 28 na Jecha, hali ya kisiasa Zanzibar bado haijatulia huku wananchi wakiwa na hofu ya kutokea kwa vurugu licha ya wanasiasa kuwatuliza wafuasi wao kila mara.
5 comments:
Asiejua maana basi wakati mwengine mwachie aishi na ujinga wake kwani wasiria, wairaki, waafganstani, walibya, wamisri wanapoendelea kuuana, na hata jirani zetu warwanda na waburundi na kenya walipouwana kwa mamilioni kwani UN haipo? Hata somali kusambaratika kwake UN iko wapi? Siku zote tunasema kule nyumbani kuna mijitu ya hovyo sana eti alafu huyo alieandika barua UN kujishtaki yeye mwenyewe anaitwa kiongozi? Nasema kujishtaki yeye mwenyewe kwa sababu nini maana ya wewe kuchaguliwa kuwa kiongozi kama si kutumia hekima yako ya uongozi kutatua matatizo? Kama barua ingeandikwa na wananchi sawa lakini eti viongozi? UN, hawana uwezo na mamlaka wa kuingilia mambo ya ndani ya nchi husika labda mpaka mkisha kuuwana, kwa hivyo la msingi ni kutumia busara na hekima zote kwa wadau wa ndani kutatua migogoro ndio njia sahii na pekee ya kuleta amani . Hiyo yakwenda UN ni upumbavu wa hali ya wakati nyinyi wenyewe hamjakaa chini kujaribu kulitatua tatizo linalo wakabili .UN inamambo mazito duniani hivi sasa mfano mamilioni ya wakimbizi barani ulaya kiasi kwamba wamehemewa hawajui wafanye nini, leo hii watu mna kijimgogoro ambao upo ndani ya uwezo wenu kabisa kuutatua mnawapelekea barua UN iwatatulie? Yawezekana kabisa mmeshikishwa kitu kidogo na CUF kuandika hiyo barua UN kwa hivyo ni masuala ya biashara ila mjenga na mvunja nchi ni mwananchi mwenyewe sio mgeni.
Hi jamani kwanini baadhi ya wasomi wa kitanzania tunaogopa debate?? Kwanini baadhi yetu tunapenda kulazimisha mawazo yetu kwa kutumia ubabe na lugha za matusi badala ya ku-reason?? Kwa mawazo yangu baadhi yetu ni wavivu wa kufanya utafiti na pengine kusoma vitabu ili kuongeza uwezo wa kufikiri. Mtoa maoni namba moja amewaita wenzake "mijitu ya hovyo sna" kwenye mstari wa nne. Hii inatokana na uwezo mdogo wa kushawishi kuwa yeye yupo sahihi na wale anaotofautiana nao wako wrong. Debate ni ushindani wa ku-reason na siyo umahiri wa kutoa lugha za matusi.
Huu ni ulimbukeni na kasumba mbaya ya kufiki kuwa ni wageni,mataifa ya kigeni ndio yanayoweza kutatua matatizo yetu ya ndani.
Matatizo ya uchaguzi hutokea kila mahali including USA. kumbuka case ya uchaguzi- George Bush Vs Al-Gore, Bush Vs Kerry.Ifike wakati tutumie uwezo wetu wa ndani kutatua matatizo yetu wenyewe.
Ni aibu kwa nchi hata baada ya miaka 54 ya uhuru bado tunahitaji wakoloni watuamulie matatizo zetu ya ndani,kwani nani hutatua matatizo yao?
Haya matatizo ni TZ tu uwezi kukuta USA wewe anoy 5:53pm unapoteza kinachotokea znz ni ukosefu wa demokrasia ya kweli maalim aliwawahi. hata bara EL angekuwa anaapishwa sasa lakini ndiyo hivyo tena.
Nani alikwambia kuwa matatizo ya uchaguzi ni Tanzania tu.Tofauti na mataifa mengine ambayo hupitia the same experience ni kuwa wanayamaliza mambo yao wenyewe kwakutumia taratibu waliojiwekea.Huwasikii wakienda kulialia IN what will UN do by the way?
Post a Comment