ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 3, 2015

Yericko Nyerere kizimbani kwa taarifa za kwenye facebook

MFANYABIASHARA Yericko Nyerere amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka matano ya kutoa taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Nyerere alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na mawakili wa Serikali, Simon Wankyo na Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Anashitakiwa chini ya Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandao Namba 14 ya 2015. Nyerere anadaiwa Oktoba 25, mwaka huu katika eneo lisilojulikana, alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook, akidai kuwa “Piga kura leo huku ukikumbuka kifo cha Mwangosi, Mateso ya Ulimboka na Kibanda, mateso ya vijana wetu wa JKT, ukikumbuka hayo fanya uamuzi sahihi bila ushabiki”.

Wanyo alidai kuwa Oktoba 24, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Nyerere alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuwa Taifa la Tanzania kuanzia leo halihitaji amani, linahitaji haki tu.

Inadaiwa, alichapisha taarifa za uongo kupitia mtandao huo kuwa, “siku ya leo mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa halihitaji amani, bali taifa hili linahitaji haki tu, amani ilishatoweka siku nyingi, kilichobaki ni uvumilivu tu…, njia sahihi ya kulitibu taifa hili ni kwa dola dhalimu kutenda haki hata kama itawauma”.

Inadaiwa Nyerere aliendelea kudai kuwa “Uchaguzi huu ni vita, anayedhani ni demokrasia apimwe akili…hii ni vita kati ya umma na dola, ni vita kati ya wema na ubaya, kati ya shibe na njaa, kati ya masikini na matajiri… umma umekosa amani na furaha, fursa pekee waliyoipata watanzania wanamjua rais wao wanayekwenda kumchagua kesho, jaribio lolote litakalofanywa na CCM na vibaraka wao la kukwamisha matakwa ya umma, litaondoa hata ule uvumilivu kidogo walionao watanzania na kisha vitazaliwa vichaa chongo ambavyo hata risasi na mabomu hayatakizima”.

Aidha, anadaiwa siku hiyo hiyo alichapisha taarifa nyingine ya upotoshaji kupitia mtandao ikisema “mipango ya hujuma ya JK toka Ngurdoto Arusha muda huu…Kikwete yupo Ngurdoto Arusha na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima pia wakuu wa vyombo vya dola na wanadhimu mbalimbali… wakuu wa mkoa wanaelezwa kuwa NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa kutumia mfumo wa kalamu za kichina… pia wanaamuliwa kuhakikisha wanahujumu kampeni za Ukawa kwa kutumia vyombo vya dola, wanaagizwa kuhakikisha kamatakamata ya vijana bodaboda wiki moja kabla ya uchaguzi na zaidi wanaagizwa wakawaagize maDC kote nchini kuhakikisha wanalinda maslahi ya CCM siku yaUchaguzi.

Katika mashitaka mengine, Nyerere anadaiwa Septemba 3, mwakahuu katika eneo lisilojulikana alichapisha taarifa za uongo kuhusu uwepo wa akaunti ya benki ya kughushi inayomilikiwa na mtanzania katika benki ya HSBC Tawi la North London, ikionesha CCM imemwekea Dk Wilbrod Slaa Euro milioni 1.5 kupitia kwa mchumba wake, Josephine Mshumbusi ikiwa ni rushwa ili kushinda uchaguzi mwaka huu.

Nyerere anadaiwa alichapisha na kusambaza taarifa hizo za uongo kupitia mtandao wa Facebook kwa lengo la kupotosha umma katika Uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Mshitakiwa alikana mashitaka na upande wa jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, pia hawana pingamizi la dhamana kwa mshitakiwa huyo.

Nyerere aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja, aliyesaini hati ya Sh milioni tano. Kesi itatajwa tena Desemba Mosi mwaka huu.

HABARI LEO

3 comments:

Anonymous said...

Am still struggling to understand what is wrong with Yericko posts. It real depends on your interpretation. There is more to this than what is said in the media.

Anonymous said...

Imefika wakati kwa Watanzania hasa vijana kuacha tabia ya kuamini bila mashaka habari wanazozisoma kwenye mitandao ya kijamii. Hii ni kutokana na ukweli usiopingika kwamba asilimia kubwa ya habari zinazochapishwa ktk mitandao kama facebook na Instagram imekuwa ikitoa habari za kupotosha, kuchafuana majina na za uchochezi.
Inasikitisha kuona kwamba kuna asilimia kubwa ya watu wanaoamini kwamba Serikali ya JK hasa JK mwenyewe hakuna walichofanya pamoja na kwamba kuna ushahidi ulio wa wazi wazi kuhusu mafanikio ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Waandishi wa habari hizi wamekuwa kwa makusudi kabisa wakitoa habari zinazolenga kuiondolea sifa serikali na taasisi zake na linalosikitisha ni kwamba idadi kubwa ya vijana hawana muda kutafuta ukweli wa kusoma au kupata taarifa sahihi kutoka maeneo husika. Linaloandikwa katika mitandao ya kijamii basi huliamini kwa asilimia 100 kuwa ni habari za kweli na kinachofuata ni kulisambaza kwa kazi ya upepo.

Ifike wakati vijana wetu wabadilike na waanze kusoma na kutafuta majarida yenye tafiti mbalimbali za kimaendelea badala ya kuendekeza mitandao ya kizushi na isiyojenga akili za vijana. Vijana wetu wasipobadilika na kuacha tabia za kukurupuka na kuamini kila jambo linalotundikwa kwenye mitandao ya kijamii itafika wakati tutakuwa na taifa la vijana ambao hawatumii akili zao. Ni muhimu vijana kuwa wadadisi na kutafakari na kuichambua kila habari unayopata. Uchambuzi wako utakufanya afanye maamuzi sahihi kuhusu ama kuiamini habari hiyo au kuipuuzia. Kutafuta ukweli ni jambo jema kumtuhumu mtu kwa habari za kushuku ni kuviza ubongo, ni makosa na kutotendea wengine haki.

Anonymous said...

Allegations zake zimewekwa wazi, labda ukitaka kujua kama habari alizokuwa anapost was based on facts,fatilia mwenendo wa kesi yake.