Friday, December 4, 2015

BALOZI SEIF AIFARIJI FAMILIA YA KOPLO YESAYA MWAKAMBI ALIYEFARIKI DUNIA KWA AJALI YA PIKIPIKI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seigf Ali Iddi akikabidhi Ubani na Kutoa Pole kwa Mke wa Koplo Yesaya Mwakambi, Bibi Wema Sanga ambaye Mumewe alipata ajali mwezi Mmoja uliopita akiwa kazini kuiongoza misafara ya Viongozi wa Kitaifa Ubungo Mjini Dar es salaam
Balozi Seif ni miongoni mwa Viongozi waliokuwa wakioongozwa na Askari huyo wa Jeshi la Polisi Marehemu Yesaya wakati wa safari zake awapo Mjini Dar es salaam.
Mke wa Marehemu Koplo Yesaya Bibi Wema Sanya wa kwanza kutoka kulia akiwa na Dada yake pamoja na watoto wake wawili wakati wakipewa mkono wa pole na Balozi Seif aliyefika kwenye Kata yao ya Goba Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam kuwafariji baada ya kufiwa na mpendwa wao.

Afisa wa Polisi S.P Zakaria Benard akitoa shukrani kwa niaba ya Jeshi la Polisi kwa uamuzi wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa kuifariji familia ya askari wa ngazi ya chini ya Jeshi la Polisi Nchini Marehemu Yesaya aliyefariki kwa ajali ya Piki piki akiwa kazini.
Kiongozi wa Familia ya Marehemu Koplo Yesaya Mwakambi Mchungaji Isaya Isaleka akitoa ushauri kwa Serikali Kuu kuisaidia Familia ya Marehemu Koplo Yesaya ambae ameacha familia ya Watoto wadogo.
 
Picha na – OMPR – ZNZ.


Jeshi la Polisi Nchini limeelezea faraja yake kutokana na mfumo wa Viongozi wa Kitaifa kuonyesha muelekeo wa kuwajali watumishi wao kutoka Taasisi tofauti za Umma na hata binafsi lakini zaidi wake watumishi wa ngazi ya chini.

Afisa wa Polisi S.P Zakaria Benard alitoa faraja hizo kwa niaba ya Jeshi la Polisi wakati akitoa shukrani za Jeshi hilo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika katika Kata ya Goba Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam kutoa mkono wa pole pamoja na kuifariji Familia ya Koplo Yesaya Mwakambi aliyefariki Dunia kwa ajali ya Piki pili Ubungo Jijini Dar es salaam.

Koplo Yesaya ni miongoni mwa Askari wa Usalama Bara barani wa Jeshi la Polisi Nchini wanaowajibika kuiongoza Misafara ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa akiwemo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata ajali akiwa kazini mwezi Mmoja na nusu uliopita .

S.P Zakaria Benard alisema kitendo cha Viongozi hao wa Kitaifa kuungana na Watumishi wao wa ngazi ya chini kimeonyesha upendo, huruma na moja ya njia itakayotowa mapenzi ya dhati kati ya pande hizo mbili kuendelea kushirikiana katika ujenzi wa Taifa.

Kamanda Zakaria alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa uamuzi wake wa kutenga muda kwa lengo la kuifariji Familia ya Koplo Yesaya.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanafamilia wa Koplo huyo Mchungaji Isaya Isaleka aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuisadia Familia ya Marehemu Koplo Yesaya Mwakambi ili iweze kuwa na nguvu za kukabiliana na maisha yao ya baadaye.

Mchungaji Isaleka alisema katika uhai wake tayari alikuwa aameshaanza kujenga hatma ya familia yake ya watoto wawili wadogo kwa kuwawekea vitega uchumi alivyovianzisha kwa nia ya kuwasaidia hapo baadaye lakini kukatika kwa uhai wa Kijana huyo pia umeenda sambamba na kusita kuendelea kwa vitega uchumi hivyo.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiifariji Familia hiyo inayoongozwa na Mke wa Marehemu Bibi Wema Sanga alisema familia ilikuwa ikimpenda sana Marehemu, lakini Mwenyezi Muungu alimpenda zaidi na ndio maana akaamua kumrejesha katika himaya yake ya milele.

Balozi Seif aliitaka familia ya marehemu Yesaya hasa Mkewe Mama wa watoto wawili Bibi Wema Sanga kwa kuwa na moyo wa subira katika kipindi hichi kifupi walichoondokewa na Mpendwa wao.

Othman Khamis Ame


Ofisi ya Makamu wa 9ili wa Rais wa Zanzibar







No comments: