Saturday, December 26, 2015

HII NDIYO YANGA MANJI YAZIDI KUPAA, TAMBWE HAKAMATIKI, SIMBA YA AVEVA IKISHIKWA KIDEVU NA MWADUI


Mshambuliaji wa Yanga Amis Tambwe (katikati) akipongezwa na wachezaji wenzake Mwinyi Haji (nyuma) pamoja na Deus Kaseke
Hamisi Tambwe ameendeleza kasi yake ya ufungaji mara baada ya leo kutupia bao mbili nyavuni wakati Yanga ikichomoza na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Mbeya City kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa taifa.

Tambwe alianza kupasia nyavu kipindi cha kwanza akiutendea haki mpira uliopigwa na Simon Msuva ambaye alimzidi mbio beki wa kushoto wa Mbeya City Hassan Mwasapili kisha kuachia krosi ambayo ilimkuta Tambwe akapachika mpira wavuni.

Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Yanga wakiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City ambao muda mwingi wa kipindi cha kwanza walicheza kwa tahadhari kubwa huku kukiwepo na matukio kadhaa ya kuchelewesha muda.

Kipindi cha pili Tambwe akapachika bao lake la pili kwenye mchezo huo akiunganisha krosi kwa kichwa na mpira huo kumshinda mlinda mlango wa Mbeya City Juma Kaseja kisha kutinga wavuni.

Mbeya City walipata pigo kufuatia beki wao mpya waliyemsajili katika kipindi cha dirisha dogo kutoka Coastal Union Tumba Sued aliyeoneshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo Jeonesia Rukyaa baada ya kumfanyia madhambi striker wa Yanga Donald Ngoma.

Thaban Kamusoko alihitimisha sherehe kwa upande wa Yanga kwa kupiga kamba ya tatu na kuipa Yanga ushindi wa bao 3-0 ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Kipindi cha pili mchezo huo ulijawa na vurumai za hapa na pale kutokana na wachezaji wa timu zote kutunishiana misuli na kumpa kazi ya ziada mwamuzi kazi ya ziada kuumudu mchezo huo.

Magoli mawili yaliyofungwa na Tambwe le , yanamfanya aongoze orodha ya wafungaji bora kwa kufikisha magoli 10 akimpiku striker wa Stand United Elius Maguli mwenye bao tisa hadi sasa.

Ikumbukwe Tambwe alikuwa na magoli nane kabla ya mchezo wa leo ambapo kwenye mchezo uliopita alifunga magoli matatu (hat-triki) dhidi ya Stand United na kujivuta kutoka kwenye magoli matano hadi nane.
Michuano ya ligi kuu Tanzania bara iliendelea tena leo December 26, 2015 kwa michezo kadhaa kupigwa kwenye viwanja vya miji tofauti ya Tanzania bara na kushuhudia matokeo tofauti katika viwanja hivyo kwa baadhi ya timu kuibuka na pointi tatu huku zingine zikishindwa kabisa kutamba na baadhi ya mechi kumalizika kwa timu kugawana pointi.
Haya ni ni matokeo ya mechi zote ambazo zimepigwa leo siku ya Boxing Day.
Mwadui FC 1-1 Simba 
Ndanda FC 1 – 3 JKT Ruvu 
Coastal Union 1 – 3 Stand United 
Maji Maji FC 0 – 2 Prisons
Mtibwa Sugar 3-0 Mgambo JKT

SOURCE:SHAFFIHDAUDA

No comments: