
Dar es Salaam. Serikali imeanza kuzichunguza benki ya Stanbic (T) na Kampuni ya Egma ya hapa nchini kutokana na kuhusika katika udanganyifu wa riba ya mkopo Dola za Kimarekani 600milioni (Sh1.3 trilioni) iliyopewa Tanzania na benki ya Standard ya Uingereza.
Benki ya Standard ina hisa katika benki ya South African Group ya Afrika Kusini ambayo ndiyo inaimiliki Stanbic tawi la Tanzania. Kampuni mama ya benki hizo zote ni Industrial and Commercial Bank of China (ICBC) ambayo imekiri kushindwa kuzuia ufisadi huo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kashfa hiyo mpya mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema Stanbic na Egma zilihusika na wizi wa Dola 6 milioni (Sh13 bilioni) na kwamba katika uchunguzi huo wanafuatilia zilikokwenda fedha hizo. Kiasi hicho ni asilimia moja ya mkopo na kiliongezwa kinyume cha taratibu za kibenki.
Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Kampuni nchini (Brela), Egma ambayo ni kifupi cha Enterprise Growth Market Advisors Ltd mwenyekiti wake ni aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wakurugenzi wake ni Gasper Njuu na Fratern Mboya.
“Sasa unafanyika uchunguzi wa kina hapa nchini kujua ilikuwaje asilimia moja ikaongezeka katika mkopo mbali na makubaliano ya awali. Tunataka kujua hiyo pesa iliyolipwa ilikwenda wapi? Kama zilitumika kumhonga mtu, je, ni nani? Watu wa Stanbic wana haki ya kutueleza,” alisema Balozi Sefue.
“Tunaishukuru Serikali ya Uingereza, pamoja na SFO, kwa kuonyesha njia katika kusaidia nchi maskini zinazodhulumiwa na wapokea rushwa na watoa rushwa. Maana zipo nchi nyingine tajiri ambazo wanapigia kelele rushwa kwa kuangalia upande wa mpokeaji tu, na kusahau makampuni makubwa kutoka kwao yanayopenda kuhonga watu wetu. Natoa wito kwa nchi nyingine tajiri kutoa ushirikiano kama huu wa Serikali ya Uingereza.
Nazishukuru taasisi zetu, Benki Kuu, na Takukuru, FIU na wengine kwa kutimiza wajibu wao na kutoa ushirikiano kwa SFO uliowezesha SFO kushinda kesi hii, na sisi kurejeshewa fedha ambazo zitatumika kutatua matatizo yetu ya maendeleo na kero za wananchi,” alifafanua Sefue.
Alisisitiza, “Baada ya ushindi huo uchunguzi unaendelea ndani ya nchi ili tujue hizo Dola 6 milioni zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu tujue ni nani. Katika hili tutaomba ushirikiano wa wenye kampuni hiyo ya Egma ambao kwa taarifa za vyombo vya habari vya Uingereza ni Bwana Harry Kitillya, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bwana Mboya ambaye ni marehemu na Bwana Gasper Njuu.”
Sefue alisema mwaka 2012-2013 Serikali ya Tanzania ilikopa Dola 600 milioni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa makubaliano ya kulipa deni hilo pamoja na riba ya asilimia 1.4, lakini katika mazingira ya ajabu riba iliongezwa na kuwa asilimia 2.4.
Balozi Sefue alisema masharti ya mkopo yaliitaka Serikali kulipa deni hilo katika kipindi cha miaka saba, hivyo mkopo huo unapaswa kumalizika mwaka 2019. Lakini mwaka 2013 iligundulika kuwa fedha taslimu Dola 6 milioni ziliingizwa katika akaunti ya Egma na ndipo walianza kulifanyia uchunguzi suala hilo.
Alisema Serikali haikuhitaji wakala wakati walipofanya maombi ya mkopo huo na kuwa haijulikani kampuni ya Egma iliingiaje katikati na kulipwa asilimia moja ya mkopo huo. Balozi alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba fedha hizo ziliwekwa katika akaunti na siku chache zikatolewa hivyo Serikali inachunguza kujua fedha hizo zilichukuliwa na nani, zilipelekwa wapi na kwa malengo yapi.
“Wakati Serikali inaomba mkopo katika benki ya Standard, si Serikali wala Standard Bank waliohitaji wakala. Sasa hatujui hawa Egma waliingiaje na kulipwa kiasi hicho cha pesa! Tunachojua ni kuwa malipo hayo hayakustahili,” alisisitiza Sefue.
Mazungumzo ya mkataba huo yalifanyika wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic alikuwa Bashir Awale na mkuu wa uwekezaji alikuwa Shose Sinare aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996. Wote wawili waliacha kazi.
Sakata hilo limeibuka wiki hii baada Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO) kutoa ushahidi wake katika Mahakama ya Southwark Crown ya jijini London, Uingereza namna ukiukwaji wa taratibu za kibenki ulivyosababisha Sh13 bilioni kuingizwa kifisadi katika kampuni ya Egma ikijifanya kuwa ni wakala.
Kwa mujibu wa kesi inayosikilizwa kwa mtindo wa makubaliano ya kumlipa fidia mlalamikaji (DPA) Standard Group ya Afrika Kusini inayomilikia benki ya Stanbic ya Tanzania pamoja na Standard Bank na kampuni mama ya Industrial and Commercial Bank of China (ICBC) zimekiri makosa.
Kufuatia hukumu ya kesi hiyo iliyotolewa juzi katika mahakama hiyo Standard Bank imetozwa jumla ya Dola 32.2 milioni (Sh69.2 bilioni) ambapo kati ya hizo Dola 16.8 milioni (Sh36.1 bilioni) ni faini inayolipwa kwa SFO, Dola 8.4 milioni (Sh18.0 bilioni) ni malipo ya fidia; na Tanzania italipwa Dola 7 milioni (15.0 bilioni).
Akizungumzia kurejeshwa kwa fedha hizo, Balozi Sefue alisema, “Serikali ya Tanzania italipwa Dola 7 milioni. Fedha hizo ni Dola 6 milioni ambazo tulitozwa isivyostahili na Dola 1 milioni ni riba ya fedha hizo. Fedha tunazorejeshewa zililipwa isivyostahili kwa kampuni ya Kitanzania iitwayo Egma. Kesi inayohusika ilifunguliwa na SFO dhidi ya Standard Bank.”
Mwananchi lilieleza jana kwa kina sakata hilo katika habari kuu iliyosema “Miss Tanzania atajwa ufisadi wa Sh1.3 trilioni.” Hata hivyo, Sinare na Awale hawajatajwa mahali popote kama walinufaika na mipango hiyo.
Utata
Hata hivyo, kumbukumbu zilizopo kwenye ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni zinaonyesha kuwa kampuni iliyopo sasa ni Egma Consult Ltd iliyosajiliwa Agosti 22, 2015, ikitofautiana umri wa miaka minne na siku mbili na Egma Ltd iliyohusika katika kashfa hiyo.
Taarifa hizo zinabainisha kuwa wakurugenzi walioisajili kampuni hiyo yenye makao makuu yake kwenye jengo la Alfa, ghorofa ya kwanza iliyopo kwenye kiwanja namba 25, Barabara ya Bagamoyo na kupatikana kwa sanduku la barua 79807 Dar es Salaam ni Harry Msamire Kitillya, Mtanzania na mchumi ambaye pia ni mkurugenzi wa ZAN Securities, kampuni ya ushauri wa masuala ya hisa.
Wengine ni Peter Atandi Nyabuti, Mkenya ambaye pia ni mkurugenzi wa Astra Insurance Brokers (T) Ltd akiwa pia ni mbobezi wa masuala ya bima, na Gasper Casmir Njuu, Mtanzania, mfanyakazi wa benki. Njuu amewahi kuhudumu kama mkurugenzi wa huduma za kibenki na benki ya Citibank nchini.
2 comments:
Hili swala ni nyeti lichunguzwe na wataalam, fbi, chain ni kubwa. Watakuwepo vigogo wengi. Viongozi siyo waaminifu. Tunataka viongozi wenye hofu ya mungu. Ndani yake. Awe na dini ya kiislam, kikristo, mpagani. Mungu ibariki Tanzania ili viongozi wetu wabadilike, isiwe laana hata kwa vizazi vijazo.
UCHUNGUZI? AU TUNAWEKA CHAIN UWE MRADI WA ULAJI KWA TAKUKURU,CID,OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI NA DPP.KWANZA NATANGULIZA KWA KUAPA KWAMBA VYOMBO HIVI VYA DOLA NILIVYOVITAJA KWA ASILIMIA KUBWA NI MAJANGA,NI JANGA LA TAIFA,VIMEHARIBIKA,VIMEHARIBIWA NA PESA.NAUNGA MKONO UFUMBUZI ULIOBUNIWA NA KUIBULIWA NA MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI.YAANI KUPELEKA MAPENDEKEZO MAKUBWA BUNGENI YA KUTUNGA SHERIA KALI YA WEZI WA MALI ZA UMMA,MAFISADI NA WATUMISHI WENGINEO WAKIWEMO WASTAAFU WAANDAMIZI.IUNDWE MAHAKAMA MAALUM YENYE SIFA ZA FAST TRACKING.HUKUMU NDANI YA MIEZI MITATU.TURUDI KWENYE SOMO.EGMA WAMEIBA,WAZI-WAZI DOLA MILLION 6,WAMEIBA.UNANGOJA NINI?HIZI NI PESA NYINGI MNO.ILI KUJINUSURU, WATAWASAMBAZIA NA WALIOTUMWA KUWACHUNGUZA,PANA NINI HAPO? HUU NI UHUJUMU UCHUMI MKUBWA MNO.SIJUI,NGOJA TUONE.
Post a Comment