ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 19, 2015

Kasi ya Magufuli yabaini vyeti feki 219

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki (wa pili kushoto) akilakiwa na watendaji wa ofisi yake mara baada ya kuapishwa hivi karibuni Ikulu Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu ofisi hiyo, Tixon Nzunda. Picha na Maktaba

By Fidelis Butahe, Mwananchi

Dar es Salaam. Kasi ya mawaziri wa Rais John Magufuli kufanya ziara za kushtukiza na kutoa maagizo kwa watendaji, imeanza kufumua ‘uozo’ baada ya jana kubainika kuwa watumishi 219 kati ya 704 wa Serikali wameajiriwa kwa vyeti vya kughushi.

Sakata hilo liliibuka baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki kutembelea idara, vitengo vya ofisi ya rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kutokana na sakata hilo, Kairuki ameiagiza idara ya usimamizi wa rasilimali watu (Utumishi), kuwachukulia hatua watumishi hao waliotumia vyeti feki kupata ajira serikalini.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Rasilimali watu Utumishi, Leonard Mchau alisema Ofisi ya Rais, imehakiki watumishi 704, lakini 219 baada ya vyeti vyao kuhakikiwa na Baraza la Mitihani, NECTA, wamegundulika kuwa waliajiriwa kwa vyeti vya kughushi.

Mchau alisema baadhi ya watumishi waliobainika kujipatia ajira serikalini kwa vyeti vya kughushi wamekimbia vituo vyao vya kazi, kuwataka wananchi kuepuka mchezo huo wa kughushi vyeti.

“Ni kosa la jinai kughushi vyeti kwa lengo la kujipatia kazi. Endapo utagundulika utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.” alisema Mchau.

Alisema ofisi hiyo inaendelea na uhakiki wa vyeti kwa watumishi wote wa umma nchini na matarajio ni kuwahakiki watumishi wote.

Akizungumzia suala hilo, Kairuki alisema, “Watumishi wote waliobainika kupitia HCMIS (Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara) wachukuliwe hatua stahiki.”

Waziri huyo alimtaka Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimali watu Utumishi, Emmanuel Mlay kutafuta ufumbuzi wa kumaliza tatizo la watumishi wanaotumia vyeti vya kughushi.

“Wasilisheni vyeti vyao baraza la mitihani kwa ajili ya uhakiki na baada ya uhakiki muwachukulie hatua stahiki watumishi wanaoonekana kutumia vyeti visivyo halali kwao” alisema Kairuki.

Itakumbukwa, Februari 24 mwaka huu, NECTA ilitangaza kuanza kuwasaka waajiriwa wote wanaotumia vyeti bandia katika ajira zao.

NECTA ilisema kuwa nchi kwa sasa inakabiliwa na tatizo la kuzagaa kwa vyeti bandia, hivyo limewataka waajiri nchini kote kushirikiana na baraza hilo kupeleka vyeti vya waajiriwa kwa ajili ya kukaguliwa.

Mkuu wa Idara ya Utawala na Fedha NECTA Daniel Matie alisema ili kufanikisha kupungua kwa tatizo la vyeti bandia nchini waajiri wanayo nafasi kubwa ya kushirikiana na NECTA katika ukaguzi wa vyeti ili kuchukua hatua za haraka kwa wale watakaobainika wanafanya kazi kwa njia ya kughushi vyeti.

Mei 21 mwaka jana, suala la vyeti bandia kwa watumishi wa umma na hata miongoni mwa wabunge, liliingia bungeni na kuzua mjadala mkali.

Vyeti feki bungeni

Wakati wa Bunge la Kumi, suala hilo lilileta mjadala mzito aliyekuwa Mbunge wa Ole, Rajabu Mohamed Mbarouk (Cuf) alileta hoja ya kuitaka Serikali kueleza ni kwa nini NECTA inashindwa kudhibiti vyeti feki huku akisema kuna mchezo mchafu unaoathiri mfumo wa elimu nchini na uchumi wa Taifa.

Alisema kuzagaa kwa vyeti hivyo kunaifanya hadhi ya NECTA kushuka na kukosa imani hata katika jumuiya za kimataifa.

“Suala la vyeti feki ambalo Baraza la Mitihani la Taifa ndilo lenye dhamana na jukumu la kuhakikisha halitokei katika taifa limeonekana kama suala la kawaida,” alisema na kuongeza; “Vyeti feki ni vingi kiasi kwamba linasababisha kuajiriwa kwa watendaji ambao ni feki na mawaziri mizigo.”

Alisema kuzagaa kwa vyeti hivyo kunasababisha kupata makatibu wakuu na watendaji feki huku akisema katika Chuo cha Polisi cha Moshi walirejeshwa wadahiliwa 122 kwa sababu ya kukutwa na vyeti feki.

Akitoa ufafanuzi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati huo, Dk Shukuru Kawambwa alisema NECTA baada ya kugundua udanganyifu wa vyeti ilibadilisha namna ya kuchapa vyeti hivyo.

“Hivi sasa vyeti vinavyotolewa vina Serial number, jina la mhitimu katika cheti cha kuzaliwa na picha na kwamba siyo rahisi kughushi vyeti hivyo,” alisema.

Hata hivyo, Mbarouk alikataa ufafanuzi huo na kusema asilimia sita ya wanaoomba kazi nchini wana vyeti feki na kutaka kufahamu hatua zilizochukuliwa ikiwamo za kinidhamu katika kukabiliana na suala hilo.

No comments: