ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 19, 2015

Ligi Kuu yazidi kukoleza utamu

 Yanga, Stand United Dar, 
Azam FC wako Songea, 
Simba kuumizana na Toto Mwanza.
Ikiwa bado wamenogewa na ushindi walioupata baada ya kuvuja jasho jingi wa bao 1-0 dhidi ya Africans Sports ya Tanga, Yanga wanashuka Uwanja wa Taifa kuikabili Stand United, huku Kocha Hans van der Pluijm akitarajia kumpa nafasi mshambuliaji wake mpya kutoka Niger, Issoufou Boubacar Garba.

Wakati Yanga ikikamuana na United, mahasimu wao, Simba wako Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kuumana na Toto Africans katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji huyo alifuzu vipimo wakati wa dirisha dogo la usajili lililofungwa Desemba 15 na alikuwapo kwenye mazoezi ya jana ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Boko Veterans.

Msemaji wa Yanga, Jerry Murro alisema jana kuwa mchezaji huyo amemalizana na uongozi, hivyo kucheza au kutocheza leo ni uamuzi wa kocha.

Kuja kwa mchezaji huyo kumeongeza ushindani wa namba, kwani tayari klabu hiyo ina washambuliaji wenye uwezo mkubwa kama Donald Ngoma, Amiss Tambwe, Malimi Busungu, Anthony Simon na Simon Msuva.

Kocha Pluijm alisema wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kubaki kileleni kwa kushinda mchezo wa leo.

“Tumetoka kwenye michezo migumu ya ugenini, tumetumia nguvu nyingi kupata pointi nne kati ya sita tulizotarajia awali. Mchezo wa leo lazima tushinde ili kujiweka pazuri,” alisema Pluijm.

“Nilichokiona katika mechi zetu mbili, kimenihakikishia kwamba msimu huu hakuna timu legelege, kwani hata mchezo mmoja tulioshinda ulikuwa mgumu kwetu,” alisema Pluijm.

Alikiri kuwapo na matatizo madogo kwenye mechi mbili zilizopita na kwamba tayari ameshafanya marekebisho kuelekea mchezo wa leo.

Kocha wa Stand United, Patrick Liewig alisema jana kuwa anatambua anakwenda kucheza na timu ngumu, lakini amejipanga kuhakikisha wanashinda ugenini.
“Yanga ni timu nzuri, nafahamu uwezo wao. Nimewaambia wachezaji wangu kuwa makini muda wote wa mchezo. Unapocheza na Yanga hutakiwa kufanya makosa,” alisema.

Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Simba watakuwa wakisaka ushindi wa kwanza baada ya ligi kuendelea tena kutokana na kusimama kwa muda kupisha mechi za kimataifa.

Katika mchezo uliotangulia, Wekundu hao wa Msimbazi walilazimishwa sare ya 2-2 na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa wiki iliyopita, hivyo leo watataka kujirekebisha kwa ushindi.

Wanakutana na Toto yenye tabasamu la ushindi mnono walioupata kwenye mechi yao dhidi ya Majimaji waliposhinda mabao 5-1 ugenini.

Kocha wa Toto, John Tegete alisema jana kikosi chake kimejipanga kushinda mchezo huo kama walivyofanya kwa Majimaji.

“Simba sasa ni timu ya kawaida, siyo ile nayoifahamu imekuwa timu ya kawaida ndiyo maana haijawahi kutwaa ubingwa kwa misimu mitatu sasa,” alisema Tegete.

Kocha wa Simba Dylan Kerr alisema anaamini mchezo utakuwa mgumu kwake kwa vile anafahamu jinsi timu ndogo zinavyozikamia kubwa.

“Toto ni timu nzuri, walishinda idadi kubwa ya mabao katika mechi iliyotangulia, wangependa kuendeleza ushindi. Sisi pia tumejipanga kushinda,” alisema.

Azam FC watakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea kusaka ushindi dhidi ya wenyeji Majimaji na wanaweza kurejea kwenye uongozi wa ligi kama watashinda na Yanga kupoteza.

Yanga inaongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 27, wakifuatiwa na Azam FC wenye pointi 26, Mtibwa katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 23 na Simba pointi 22.

Mechi zingine leo zitakuwa Kagera Sugar dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, huku Ndanda FC wakisafiri kwenda Mwadui kupambana na Mwadui na Prisons watakuwa nyumbani dhidi ya Mtibwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: