Friday, December 25, 2015

Mambo 6 pasua kichwa siku 50 za Magufuli leo

Rais Dk. John Magufuli, leo anatimiza siku 50 tangu akabidhiwe nafasi hiyo, tayari akipongezwa kwa kufanya makubwa yanayowazidi baadhi ya watangulizi wake ndani ya muda mfupi aliyokaa madarakani.

Miongoni mwa mafanikio yanayompa sifa Rais Dk. Magufuli, ni kuweka rekodi kubwa ya kukusanya ndani ya muda mfupi, inayokadiriwa kufika Sh.trilioni 1.3 ndani ya mwezi mmoja, kudhibiti wizi wa fedha za serikali na kubana bajeti.

Kiongozi huyo aliyekabidhiwa nafasi hiyo Novemba 5, mwaka huu, licha ya kioo bora cha mafanikio aliyoyaonyesha, pia anakabiliwa na changamoto ya kutekeleza ahadi kuu sita alizozitoa wakati wa kampeni, ambazo ni zifuatazo:

Ujenzi wa Mahakama ya Mafisadi
Ni ahadi aliyokuwa akiitoa kwamba angeitekeleza mara moja, pindi angechaguliwa kushika madaraka aliyo nayo sasa.

Katika moja ya mikutano yake, Rais Dk. Magufuli, katika mikutano yake ya kampeni, alikuwa kila mara alikuwa akirudia matashi: “Nitasimamia uundwaji Mahakama ya Kushughulikia Mafisadi na ‘Majizi’ wa nchi ili wafungwe.”


Hata hivyo, ahadi hiyo haijatekelezwa na bado hakuna tetesi zinazohusiana na uundwaji wa chombo hicho cha kisheria, katika kipindi hiki ambacho tayari ameshaunda Baraza la Mawaziri, ambalo halijakamiika.

Huku wananchi wakisubiri kwa hamu utekelezaji wa ahadi hiyo kwa matarajio ya kuondokana rasmi kero hiyo kubwa kwao, Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano, chombo chenye mamlaka ya kuidhinisha uundwaji huo, limeshakutana mara moja.

Tanzania katika historia ya hivi karibuni imeshakumbwa na kashfa kadhaa, ikiwa ni pamoja na inayohusu rushwa ya ununuzi wa rada ya kijeshi, iliyoinunua kutoka Uingereza kwa bei kubwa ya Sh. bilioni 70,
Nyingine ni inayohusu kampuni ya uzalishaji umeme ya Richmond na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, iliyowang’oa madarakani baadhi ya vigogo wa serikali, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema kujiuzulu.

Katiba Mpya
Ni ahadi iliyoshindikana kwa mtangulizi wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye alianzisha mchakakato huo katika kipindi chake cha uongozi.

Pamoja na kuanza katika muda uliopangwa na kuongezwa siku 90 za majadiliano na hatimaye kutoa rasimu ya mwisho ya katiba ili ipelekwe kwa wananchi kupigiwa kura, azma hiyo haikufikiwa.

Bunge lilimaliza muda huo, likiwa mikono mitupu na tayari lilishatumia Sh. bilioni 40, pasipo kupatikana muafaka.

Rais Kikwete alilazimika kuongeza siku nyingine 60, lakini kutoka na mwingiliano na ratiba ya Bunge la Bajeti, liliahirishwa na haikutolewa tarehe maalumu ya kuanza tena kwa mchakato huo.

Hivyo, hili linamfanya Rais Dk. Magufuli awe na mtihani mkubwa katika kukamilisha mchakato huo, katika mazingira anayohitaji ushirikiano wa karibuni kutoka kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe mna Mwanasheria Mkuu wa Seriklali George Masaju.

Mgogoro wa Kisiasa Zanzibar
Ni mojawapo ya maeneo ambayo Rais Dk. Magufuli anawajibika moja kwa moja, kuhakikisha uanfikia katika hatua ya ufumbuzi kwa ustawi wa kisiasa na kijamii wa Zanzibar na Tanzania Bara, pia uchumi wake.

Sakata hilo ambalo inakabiliwa na jicho la wafadhili wa kimataifa, limesababishia Tanzania kukwamishwa kupatikana msaada kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani, kiasi cha Dola za Marekani milioni 472 (Sh. bilioni 999.4).

Fedha hizo ni msaada wa awamu ya pili iiyoidhinishwa hivi karibuni,kwa sharti la kupatikana ufumbuzi wa haraka wa mgogoro huo, ambao chanzo chake ni matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Ni hatua inayotokana na tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, baada ya siku ya tatu, yaani Oktoba 28, alipofuta matokeo ya uchaguzi huo kwa nafasi ya Rais na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Ni jambo lililozua malumbano mengi ya kisiasa na kisheria kuhusu hatua hiyo na hadi sasa kuna vikao kadhaa vya kuidaka suluhu vimeshafanyika, baina ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF), visiwani humo.

Makosa ya Mtandao
Ni mojawapo ya maeneo ya changamoto kwa Rais Dk. Magufuli, baada ya serikali ya Marekani kuiwekea vikwazo Tanzania, ikihitaji maelezo ya kina kuhusu watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni, wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Sheria hiyo iliyoanza kutumika Septemba Mosi mwaka huu na tayari imeshawatia matatani wa kadhaa, wakiwamo wafanyakazi na viongozi 38 wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Pia tuhuma hizo zinawahusu baadhi ya watu walioweka taarifa batili kwenye mtandao, ikiwamo taarifa zinazodaiwa kuwa potofu, zinazomhusu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange.

Ujenzi wa Viwanda na Hospitali
Dk. Magufuli alikuwa akiahidi katika kampeni zake kuwa atajenga viwanda katika kila mkoa, kulingana na mahitaji ya sehemu husika, ili kulifanya taifa lijitegemee na wakati huo huo, kuongeza fursa za ajira, jambo ambalo hajalitolea kauli tangu aingie madarakani.

Ahadi nyingine ni kuhusu ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata, hospitali kwa wilaya zote na Hospitali ya Rufaa kwa kila mkoa. Hadi sasa mchakato wa kukamlisha ahadi hizo imebaki kuwa kimya.

Changamoto ya amani na utulivu
Matukio ya ukosefu wa utulivu amani, kama vile vurugu kutawala kwenye matukio ya uchaguzi katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi, ni changamoto ya utawala mpya wa Rais Dk. Magufuli.

Mojawapo ni tukio la Desemba 20, mjini Tanga katika uchaguzi wa Meya na naibu wake, zilitawaliwa na vurugu, hali kama hiyo nayo ilitiokea siku ya Desemba 10, mwaka huu katika kikao kama hicho, katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Kote Polisi walilazimika kuingilia kati.

Ufanisi wa serikali yake
Rais Dk. Magufuli mara baada ya kuapishwa Novemba 5, siku hiyo hiyo alimteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju, amsaidie majukumu ya msingi yaliyimkabili ndani ya muida mfupi.

Siku moja baadaye, Novemba 6, alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha na Ofisini ya Hazina, kubaini uhalisia wa utendaji wa watumishi serikalini.

Ilipofika Novemba 19, alimteua Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu, ambaye wamekuwa wakiendesha kampeni nzito katika safu ya timu moja.

Desemba 3, mwaka huu, Rais alifanya kikao na jumuiya ya wafanyabiashara akiwaagiza wote wanaotuhumiwa kutoa mizigo yao bandarini bila ya kulipiwa kodi, walipe madeni yao ndani ya siku saba, kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Rais Dk. Magufuli, kwa akishirikiana na Waziri Mkuu Majaliwa, walisaidia kukamatwa kwa makontena tisa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) eneo la Mbezi, Tangibovu yakiwa yametoroshwa bila kulipiwa ushuru wa Sh. milioni 58.

Kubana matumizi
Siku ya Novemba 7, Rais Magufuli alifanya kikao na watumishi wa serikali, wakiwamo makatibu wakuu wa wizara na naibu wao, pia watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali za umma, kujadili hoja ya namna ya kufanya kazi kwa ufanisi katika serikali yake.

Dk. Magufuli aliwatangazia watumishi hao kufutwa safari za nje za watumishi mpaka pale atakapotoa tena tamko au kwa ridhaa yake.

Alichukua uamuzi wa kufuta safari hizo baada ya kubaini kuwapo kwa matumizi makubwa ya fedha kwa watumishi wa serikali, walioko katika taasisi, wizara na idara za serikali ambao walikuwa wakijipangia safari bila ya utaratibu maalum.

Pia, Rais Magufuli Novemba 23, alitangaza kufuta Sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara, ukiotakiwa kufanyika Desemba 9 na akaagiza itumike kusafisha mazingira, tukio lililofanyika kwa mafanikio makubwa.

Inaelezwa kuwa, uamuzi huo iliokoa kiasi cha Sh. bilioni nne ambazo zingetumika kwa sherehe hizo na zikahamishiwa katika mradi wa ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaam, kipande cha Morocco - Mwenge.

Pia katika hatua hiyo hiyo ya kubana matumizi, Rais Dk. Magufuli amefuta matumizi holela ya fedha za umma katika ununuzi wa kadi za sikukuu na samani za ofisi kutoka nje ya nchi.

Katika tukuio lingine lililovutia umma ni la Novemba 20, mwaka huu Rais Dk. Magufuli aliagiza fedha zaidi ya milioni Sh. 225 zilizokuwa zitumike katika sherehe za kufungua bunge mjini Dodomam, zielekezwe katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kufanya maboresho ya huduma.

Siku tano baadaye, Novemba 25, mwaka huu, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitangaza kufutwa kwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani nchini, akaelekeza bajeti ya sherehe hizo zitumike kununua dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs).

Maamuzi magumu
Novemba 9, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako alikuta hali mbaya ya huduma, huku baadhi ya mashine muhimu za vipimo ikiwamo CT Scan havifanyi kazi kwa miezi kadhaa.

Ni tukio liliooendana na kufutwa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali hiyo na kuuondolewa kwa Kaimu Mkurugenzi wake, Dk.Hussein Kidanto, aliyejeshwa katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jisnia,Wazee na Watoto.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli aliagiza mashine za vipimo za MRI na CT-Scan zitengenezwe mara moja kwa kutolewa kiasi cha Sh. bilioni 3 kugharimia matengenezo hayo, huku akiamuru mgonjwa aliyetelekezwa kwa miezi zaidi ya miwili, atibiwe mara moja.

Baadaye, Novemba 27, mwaka huu, alihamia katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kumsimisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade.

Ilikuwa ni baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini upotevu wa makontena 349, yaliyotolewa bandarini bila ya kulipiwa ushuru na kuisababishia serikali kukosa mapato yake ya Sh. bilioni 80.

Desemba 7, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe, kisha akaivuja Bodi yake Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), iliyokuwa chini ya Profesa Joseph Msambichaka.

Hali kadhalika, Desemba 16, mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, akitoa sababu ya kutoridhishwa na utendaji wa taasisi yake, katika kasi kukabiliana na rushwa nchini.

Ni hatua iliyoendana na kufutwa kazi kwa watumishi wanne wa Takukuru, aliosema walikaidi agizo la kutoruhusiwa kwenda nje ya nchi, pasipo kibali cha mamlaka inayowasimamia.

Juzi, Rais aliendeleza pamnga lake hilo, kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito, akitaka apishe uchunguzi wam, kuhusu tuhuma za kukiuka taratibu za manunuzi ya umma, katika mchakato wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.

AHADI ALIZOZITEKELEZA
Rais Magufuli wakati akifanya kampeni za urais alitoa ahadi mbalimbali kwa wananchi kuwa angezitekeleza mara tu atakapoingia madarakani.

Mojawapo ya ahadi ambayo ameshaitekeleza tangu aingine madarakani ni utoaji wa elimu bure kuangia elimu ya msingi hadi sekondari kuanzia mwaka 2016/17 hatua ambayo imeshaanza kutekelezwa na baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya.

Ahadi nyingine ni kuwaajibisha watendaji wazembe serikalini kwa kuwafukuza kazi bila ya kuwaamisha vituo vyao vya kazi kama ilivyozoeleka kwa watangulizi wake walivyokuwa wanafanya.

Kutekeleza hilo, Rais Magufuli ameshamsimamisha kazi Dk. Edward Hoseah wa Takukuru, Kamishna wa TRA, Rashed Bade, Mkurugenzi wa TPA, Awadhi Massawe na Mkurugenzi wa Rahco, Mhandisi Benhadard Tito.

Kadhalika, Rais Magufuli ameshaanza kutekeleza ahadi ya kuongeza makusanyo ya mapato kutoka bilioni 800 hadi kufikia trilioni moja, kwani kwa muda wa siku 30 aliweza kukusanya mapato yanayokadiriwa kufikia Sh. trilioni 1.3.

Kimataifa
Tangu aingie madarakani, Rais Dk. Magufuli amekuwa gumzo katika nchi mbalimbali duniani, ikiwamo Afrika, Ulaya na Marekani.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sunday Independent la Afrika Kusini, ilibeba tahariri ya kimataifa yenye kichwa cha manenio yanayomsifia Dk. Magufuli ” Afrika ifuate mfano wa Tanzania.”

Sehemu ya tahariri hiyo ilikuwa na maelezo: “Afrika inahitaji Rais kama Dk. Magufuli, ambaye ameonyesha kwa dhati, nidhamu katika matumizi ya serikali.”

Pia, nchi za Ghana na China nazo zimejitokeza kusifu uchapakazi wa Rais Magufuli.

Nchini Kenya, wananchi wake nao wamekuwa wakitaka serikali yao iwe na mfumo kuwajibika kwa mfano wa utendaji wa Rais Dk. Magufuli, huku katika katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Uganda, mgombea mmoja alijinadi kwa kudai auchaguliwe, ili achape kazi kwa mfano wa Rais Dk. Magufuli.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: