Friday, December 25, 2015

Mchezo wa Upatu chanzo cha polisi kuuana Mwanza

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Justus Kamugisha

Mauaji ya kinyama yaliyofanywa na askari polisi H852 PC Masunga Elisha, kwa kumuua mwenzake H5950 PC Petro Matiko (29), wote wa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mwanza juzi, yamedaiwa yalitokana na mchezo wa kupeana fedha maarufu kama ‘upatu’ kati ya wawili hao.

Habari za kiuchunguzi zilizofanywa na Nipashe baada ya kuzungumza na baadhi ya watu wa karibu wa marehemu hao, zilidai askari hao walikuwa wakifanya mchezo wa kupeana sehemu ya mishahara yao mwisho wa mwezi kwa lengo la kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Ilielezwa kuwa wakati mishahara ya watumishi wa serikali wakiwamo polisi kulipwa wiki hii, PC Matiko ilikuwa zamu yake kupewa ‘upatu’ huo toka kwa mwenzake PC Masunga ambaye siku ya tukio alikuwa zamu ya ulinzi katik Benki ya Posta iliyopo barabara ya Kenyatta jijini hapa.

Siri hiyo ilivuja baada ya baadhi ya marafiki wa marehemu hao, kudai siku ya tukio marehemu Matiko alikwenda katika benki hiyo kuchukua fedha zake katika akaunti yake, lakini kutokana na tatizo la kimuamala, alishindwa.

“Kutokana na kutofanikiwa huku akifahamu anamdai PC Masunga aliyekuwapo lindoni katika benki hiyo, alimfuata na kumtaka ampe ‘chake’ kwa kuwa mwezi huu ilikuwa zamu kuchukua,” alisema mmoja wa marafiki wa PC Matiko.

Alidai kuwa wawili hao ambao hawana muda mrefu kuajiriwa Jeshi la Polisi, kauli ya PC Matiko ilimkwaza PC Masunga na hivyo akaamua `akakoki’ silaha yake na kumlenga mdai wake katika bega la kushoto.

Maamuzi hayo ya hasira yaliyofanywa na Masunga, yaligeuka na kuamua kuhitimisha uhai wake kwa kujilenga kidevuni na kujilipua kwa risasi iliyochomoza kichwani.

Hata hivyo, ilielezwa PC Matiko ambaye alifariki dunia akiwa akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando alimtaka PC Masunga amlipe upatu huo ili akanunue mahitaji ya sikukuu ya Krismasi.

“Masunga aliamini akimlipa Matiko fedha zile, hatabakiwa na chochote, hivyo yeye na familia yake ya mke na mtoto mmoja wa miaka miwili, watashindwa kujihudumia kipindi hiki cha sikukuu,” alidai.

Askari hao ambao wote walikuwa wakiishi nyumba za uraiani jijini hapa, ilielezwa Masunga alikuwa akiishi Magomeni Kirumba na Matiko Mabatini jijini hapa.

Matiko aliyeuawa akiwa amevaa nguo za kiraia, aliagwa jana katika viwanja vya polisi jijini hapa na mwili wake kusafirishwa kupelekwa kijijini kwao, Nyamitembe Wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Mwili wa marehemu Masunga ambaye haikuwezekana kuagwa jana, unatarajiwa kusafirishwa hadi nyumbani kwao Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kwa maziko.

Mauaji hayo ya kinyama yalifanyika juzi saa 8:30 mchana, baada ya PC Masunga akiwa na mwenzake lindoni, H4291 PC Lemigius Alofoustin, kumfyatulia risasi PC Matiko.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Justus Kamugisha, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo huku akisema uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea kufanyika.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, jana aliongoza baadhi ya wananchi wa jijini Mwanza katika shughuli za kuuaga mwili wa PC Matiko iliyofanyika kwenye viwanja vya Polisi Nyamagana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: