MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad, amekiuka agizo la Rais Dk. John Magufuli, baada kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, CAG aliondoka nchini Jumamosi (Desemba 12, 2015) kwenda jijini Nairobi, Kenya na kurejea nchini Jumanne wiki hii.
Taarifa hizo, zimesema CAG alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi, kazi ambayo haina uhusiano na ofisi yake, lakini alilipiwa gharama zote na ofisi yake.
“Bosi wetu aliondoka kwenda Nairobi Jumamosi iliyopita na kurejea Jumanne, alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi bila kibali cha Ikulu, alipaswa kupata kibali kwa sababu ofisi yake ndio ililipa gharama zote.
“Jumla ya gharama zinafika Sh milioni 15, ambazo ni pamoja na posho, tiketi ya ndege, hoteli na gharama nyinginezo,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.
Alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu safari hiyo, Profesa Assad hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo, zaidi ya kutishia kwenda mahakamani.
“Wewe si umesema umepata taarifa kutoka vyanzo vyako na umenipigia ‘for validation’, sasa mimi nakwambia hizo taarifa si za kweli na mkiandika tutachukua hatua,” alijibu CAG.
Baada ya muda, Profesa Assad alipiga simu kwa mhariri akimtaka afike ofisini kwake akachukue nyaraka za kuthibitisha kuruhusiwa na kusafiri nje ya nchi na ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Kutokana na mhariri huyo kuwa nje ya Dar es Salaam, alimtuma mwandishi mwingine kwenda katika ofisi ya CAG ili kuchukua nyaraka hizo. Mwandishi alipofika, CAG alikataa kumpa wala kumwonesha nyaraka hizo.
Juhudi za kumpata Balozi Sefue kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda. Baada ya kupigiwa muda mrefu aliandika ujumbe mfupi wa simu ukisema. “Nimebanwa na majukumu siwezi kupokea simu yako,” ulisomeka ujumbe huo.
Tukio hilo la CAG limekuja siku mbili baada ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kosa la kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.
Watumishi wa taasisi hiyo waliosimamishwa kazi ni Ekwabi Mujungu (Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu), Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.
Profesa Assad aliteuliwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba 5, 2014.
Kabla ya uteuzi wake, alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alichukua nafasi ya Ludovick Utouh ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.
Credit: Mtanzania
3 comments:
Sasa watu kama hwa na anajita msomi. Anafaida Gani na usomi wake, mtu anashindwa hata kufata agizo la nchi yake, anaweka mambo ya nchi mikononi mwake na anajua mkuu wake ameshatamka. Hawa ndio wanaopelekea wengi wahangaike kwa kukosa huduma muhimu, hizo hela ni malipo ya kodi, huu ni wizi. Hata jitu lenyewe ukiliangalia alina busara. Elimu pasipo mahalifa na upeo ni tabu sana,
Ndugu zanguni poleni na shughuli nyingi. Wakati mkuu wa nchi anajitahidi kuchapa kazi, na watendaji wengine wanamadharau, basi wachukuliwe hatua pia wafanyakazi wa ofisi ya rais waliofanya kazi kwa kipindi cha awamu yanne wangehamishiwa kwenye ofisi zingine kwasababu walishafanya madudu mengi. Tunataka mh. Raisi afanye kazi na sura mpya sasa katika ofisi yake.
this movie ya kufuta watu kazi, kufunga magate,kushow up kwenye makazi as supprise yatakuwa hovyo kama hatua hazitachukuliwi kwa wakubwa kama huyu. Also walio fukuzwa wengi ni vyeo vya chini the big ones wako kando wamacheka.
Post a Comment