MPANGO wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili fedha zitumike kuboresha huduma za jamii, umetua kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao sasa wameondolewa malipo ya posho wakati wanapokuwa katika vikao vya kamati zao mbalimbali za kisekta.
Kwa muda mrefu sasa, imezoeleka kwa wabunge kupokea posho kutoka kwenye mashirika na taasisi mbalimbali za umma wanapoketi kutekeleza wajibu wao ndani ya kamati za Bunge.
Hata hivyo, posho hizo hazitakuwapo tena baada ya Msajili wa Hazina, Lawrance Mafuru, kutangaza jana kuwa sasa posho hizo hazitatolewa tena kwani wanachokifanya wabunge ni sehemu ya kazi zao.
Msajili alitoa agizo hilo wakati wa mkutano wake na wakuu wa taasisi na mashirika ya umma na pia wenyeviti wa bodi zao. Msajili Mafuru alisema agizo hilo limetoka kwa Rais Magufuli, na kwamba sasa kinachotakiwa ni kuona utekelezaji wake.
Bodi zafutiwa Posho za Vikao
Kadhalika, Mafuru alisema serikali imefuta posho za mikutano ya bodi ambazo wamekuwa wakilipwa wajumbe na kuagiza kwamba badala yake, kuanzia sasa watakuwa wakilipwa malipo ya bodi peke (board fees), huku maelekezo mengine yakitaka vikao hivyo vya bodi vipunguzwe kutoka kufanyika karibu kila mwezi na sasa vya idadi ya juu vibaki kuwa vinne pekee kwa mwaka.
“Kuna mambo ya hospitality allowances (posho za takrima). Tumepata taarifa kwamba wabunge wanapofanya kazi za kamati, huwa wanalipwa fedha na Bunge. Hivyo kuwapa pesa tena ni double invoice… tunahitaji kuacha hii,” alisema Mafuru.
Alisema zipo taarifa kwamba kuna tatizo la baadhi ya wabunge kuwa katika katika bodi zaidi ya moja na kwamba, utaratibu huo siyo mzuri na unaweza kuathiri utendaji kazi.
“Kuna wakati mwingine unakuta mtu mwingine anakaa kwenye bodi hata tano au saba. Sasa inapotokea anatakiwa kuwajibika katika bodi nyingine, anakuwa hawezi kutekeleza wajibu wake kwavile anakuwa amebanwa na ratiba. Ila tunashukuru kwamba sasa hivi kuna effort (jitihada) nzuri zimefanyika kwa kuruhusu kumuondoa mbunge kwenye bodi,” alisema.
Kadhalika, Mafuru alifichua kuwa baadhi ya Bodi za mashirika na taasisi za umma husafiri na kundi la wabunge kwenda nje ya nchi, lakini mwishowe wabunge hao huwa hawafiki eneo la tukio linalowapeleka nje.
“Unakuta baadhi ya bodi zinasafiri na kundi la wabunge, halafu tunasikia wengine hawafiki eneo la tukio. Kama ni mbinu ya kutaka wabunge wafichefiche madudu, sidhani kama wabunge wa sasa wananunulika. Mtaenda nao huko nje, lakini wakirudi ndani watawalipua tu,” alisema Mafuru.
No comments:
Post a Comment