ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 17, 2015

WAZIRI KITWANGA AWAPA POLISI SIKU MOJA YA KUJIELEZA NI KWA NINI HAWALINDI BANDARI YA DAR ES SALAAM

Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ametoa siku moja kwa Jeshi la Polisi kueleza ni kwa nini askari hawalindi Bandari ya Dar es Salaam badala yake kazi hiyo inafanywa na kampuni binafsi za ulinzi.
Kitwanga amepanga kukutana na viongozi waandamizi wa Polisi kesho ili kujadili mipango na mikakati mbalimbali ya kuongeza ufanisi wa kazi ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumza na maofisa waandamizi wa polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika Chuo cha Taaluma ya Polisi na kuangalia makazi ya askari, Kurasini, Kitwanga alieleza kusikitishwa na hatua ya polisi kuacha kutoa ulinzi bandarini na kuita kitendo hicho kuwa ni udhaifu wa jeshi hilo.
Alisema kitendo hicho kimetoa mwanya kwa baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi wakati wa kushusha bidhaa zao akisema Bandari ni eneo la mpaka ambalo linahitaji ulinzi wa polisi kama mipaka mingine ya nchi.
Akionekana kukerwa, Waziri Kitwanga alimkatisha Kamishna wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipojaribu kutoa sababu akimtaka kutumia siku nzima ya leo kuandaa majibu ili kesho wayazungumze kwenye kikao rasmi.
Waziri Kitwanga amelitaka pia jeshi la polisi kumweleza mipango ya kukabiliana na dawa za kulevya kwa sababu ndiyo zimekuwa chanzo cha matukio mengi ya uhalifu ikiwamo tishio la ugaidi.
Alisema haiwezekani kitengo cha kupambana na dawa za kulevya kikaachiwa jukumu hilo wakati jeshi la polisi liko kwenye operesheni zake kila siku.
Kuhusu msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, waziri huyo alisema ni uzembe wa askari wa usalama barabarani kwa sababu wameshindwa kusimamia sheria na kuwachukulia hatua madereva wazembe.
Alisema zipo nchi za Afrika ambazo hazina askari wa barabarani kwa sababu kiwango cha nidhamu ya madereva wake ni kikubwa na wamekuwa wakifanya vizuri kuhakikisha kwamba suala la msongamano usio wa lazima unadhibitiwa kwa kufuata sheria.
Baadhi ya askari walimweleza Kitwanga kero zao. Mmoja wao, Alphonce Malowa alisema nyumba za askari ni chache na nyingi zimechakaa kiasi cha kuwafanya kudharaulika mbele ya wananchi.
Inspekta Novatus Makondowa alieleza juu ya umuhimu wa Serikali kuwasomesha walimu wa chuo cha taaluma za polisi ili kuwajengea uwezo zaidi wa kufundisha maofisa wengine chuoni hapo.     

2 comments:

Anonymous said...

MHE KITWANGA,HUYO KOVA NI KIRUSI AMESABABISHA WIZI MKUBWA NA KWA MIAKA MINGI BANDARINI,BANDARI IMEMFANYA AWE TAJIRI'HARAMU' MKUBWA,ASIMAME KAZI ACHUNGUZWEKAJINUFAISHA SANA MASHAHIDI NI ASKARI WA CHINI YAKE.

Jay said...

Sikia Mheshimiwa Kitwanga, huu mchezo wa bandari na wizi mwingi wa ujambazi hapa Dar Es Salaam, huyo kamanda wako Kova ni muhusika mkuu na wenzake. Wao wanachofanya ni kujihusisha na ujambazi kutumia vijana wao na kama ikitokea jambazi kaiba bila wao kujuwa basi huyo jambazi lazima tu atakamatwa, that is for sure. Kama unataka ushahidi kamili wa kukutana na mimi face to face mpe mwenye hii blog namba zako kisha aanitumie kwenye e-mail yangu nahapa nitakutafuta. Nina ushahidi tosha dhidi ya Kova hata na wizi wanaoufanya bandarini kwa idhini ya Kikwete na mawaziri wake. Tafadhali safisheni nchii hii, hawa kina Kova ni wapuuzi sana na wauwaji wakubwa. Mwaka jana mwanzoni, kuna mzigo ulikamatwa pale bandarini ukiwa unatoka bila kukaguliwa, then akaja mtu (wa usalama) na kusema kuwa ni wa mzee, jamaa wakaangaliana tu then wakaliachia gari kwenda kujulikanako. Kwa kweli hii nchi umasikini twajitakia wenyewe kwa kutokuwa makini na viashiria uchumi.


Plz: Mwenye blog hii ukipata contacts za Mh. naomba unitumie haraka kabla sijaenda mkoani kula Krisimasi.