ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 4, 2016

Bakwata yataka ufafanuzi msamaha wa kodi

Mwenyekiti wa Taasisi ya Imam Bukhary Islamic
By Hadija Jumanne, Mwananchi

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) pamoja na taasisi zake limeiomba Serikali kutoa ufafanuzi masuala ya misamaha ya kodi kwa taasisi za dini ili kuondoa changamoto zinazoweza kusababisha upendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislam ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis alisema kama utaratibu wa kudai taarifa za matumizi ya misamaha ya nyuma umeanzishwa, Serikali iwaweke wazi wanufaika wote wa misamaha hiyo na isiwaachie maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waifanye kazi hiyo.

Alisema Novemba 19 mwaka jana, TRA iliandika barua kwa Baraza ikitaka ipatiwe taarifa mbalimbali kwa lengo la kutoa msamaha wa gari moja aina ya Iveco lililoombewa msamaha kama taasisi za dini zinavyofanya.

“Katika barua ile, tuliambiwa tutoe taarifa hizo ndani ya siku saba na tuambatanishe kazi za magari 82 yaliyoingizwa nchini tangu 2006, vitabu vinavyoonyesha safari za magari hayo, majina ya madereva, risiti za kulipia mafuta, bima, huduma za matengenezo na pia tuwasilishe ushahidi wa fedha zinazotumika kununua magari hayo pamoja na hesabu za mwaka,” alisema Sheikh Khamisi.

Bakwata ilisema katika kipindi cha miaka 10 kuanzia 2006 hadi 2015, baraza pamoja na taasisi zake, ilipata misamaha ya kodi yenye thamani ya Sh1.9 bilioni.

Msamaha huo ni wa kutoa magari 82 bandarini yenye thamani ya Sh6.8 bilioni ikiwa ni wastani wa magari manane kwa mwaka.

Wakati huo huo, ilielezwa kuwa misamaha ya kodi inayotolewa na TRA kwa taasisi nyingine za dini zisizokuwa za Kiislamu katika kipindi hicho ilikuwa Sh90 bilioni, sawa na magari 3,937 ya aina mbalimbali yaliyokuwa na thamani ya Sh331 bilioni ambayo ni wastani wa magari 394 kwa mwaka.

“Takwimu zinaonyesha kuwa Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake zimefaidika na msamaha wa kodi ya jumla ya Sh19.5 bilioni kwa kuingiza magari 691 yenye thamani ya Sh59 bilioni ambayo ni sawa na wastani wa magari 69 kwa mwaka na msamaha huu ni takribani mara kumi na moja ya ule waliopewa Bakwata,” alidai Sheikh Khamisi.

Alisema katika kipindi hicho cha miaka 10, Jumuia ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCCT) pamoja na taasisi zake, ilipata msamaha wa kodi ya Sh13.8 bilioni kutokana na kuingiza magari 527 yenye thamani ya Sh42.9 bilioni, sawa na wastani wa magari 53 kwa mwaka na kodi iliyosamehewa ni zaidi ya mara 13 ya ile iliyosamehewa Bakwata na taasisi zake.

“Pia Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania pamoja na taasisi zake, walipata msamaha wa kodi wenye thamani ya Sh57 bilioni kutokana na kuingiza magari 2,719 yaliyokuwa na thamani ya Sh186 bilioni ikiwa ni wastani wa magari 272 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na msamaha huu ni zaidi ya mara 30 ya msamaha waliopatiwa Bakwata,” alifafanua.

Alisema mbali na msamaha wa taasisi hizo za dini, pia jumuiya za Wahindu na Mabudha pamoja na taasisi zao walipatiwa msamaha wa kodi wa Sh9 bilioni baada ya kuingiza magari 203 yaliyokuwa na thamani ya Sh36 bilioni ambayo ni sawa na wastani wa magari 20 kwa mwaka na msamaha huo ni mara tano ya waliopatiwa Bakwata.

Alisema kutokana na misamaha hiyo, Baraza kwa niaba ya Waislam, wametilia shaka msimamo wa TRA wa kuwataka wapeleke vielelezo vya magari 82 yaliyosamehewa kodi katika kipindi hicho cha miaka 10.

“Baada ya kufanya mashauriano na taasisi nyingine, tunachukua nafasi hii kuiomba Serikali itupatie ufafanuzi,” alisema.

2 comments:

Anonymous said...

Kuombwa kuwasilisha vielekezo au ushahidi haimaanishe umenyimwa msamaha.Taasisi nyingine zitaendelea kupata misamaha kama vinawakilisha ushahidi kama inavyoagizwa na TRA. Swala la kuuliza hapa ni je hizi jumuia nyingine zinawakilisha ushahidi kama inavyoelekezwa na TRA

Anonymous said...

Iko haja ya serikali kufanya tathmini katika taasisi hizi.Unapoongelea msamaha wa kodi wa magari appx.300 kwa mwaka bila justification haileti maana.