ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 6, 2016

Magufuli aagiza mambo matatu kwa CAG, DPP

Rais Dk. John Magufuli, amekutana na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Eutropius Mganga, Ikulu jijini Dar es Salaam na kuwapa mambo matatu muhimu anayoyataka katika serikali yake ya 'Hapa kazi tu'.

Pamoja na kutakiana heri ya Mwaka Mpya, wamezungumzia mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wa Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia yaliyojiri katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana, Prof. Assad alisema kwanza walizungumzia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Profesa Assad alibainisha kuwa Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ihakikishe Tanzania inaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya pato la Taifa (GDP) kwa mujibu wa hesabu zilizofanyika mwaka juzi.

"Hadi mwaka juzi Tanzania ilikua inakusanya mapato kwa kiwango cha asilimia 14 ya pato la Taifa ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikua ikikusanya asilimia 19 ya pato Taifa, na hakuna sababu za msingi za kwa nini Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo," alifafanua Prof. Assad.

Wakati Ofisi ya GAG ikitakitakiwa kufanya mambo hayo mawili, jambo la tatu lilielekezwa kwa DPP, Mganga ambaye alisema mazungumzo yao yalijikita katika suala la kupeana mikakati ya namna ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka inavyopaswa kufanya kazi ili kuendana na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano isemayo "Hapa Kazi Tu"

Aidha, Mganga ameongeza kuwa wamezungumzia umuhimu wa kuwahimiza Watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yake itatekeleza wajibu wake bila kumuonea mtu.

Kiongozi mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber Ally, ambaye pamoja na kumpongeza rais kwa juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake, amesema Waislamu wote nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee na juhudi hizo.

"Na pia kwa niaba ya Waislamu tunataka kumueleza kwamba kazi anayoifanya ni kazi ambayo tunairidhia na tunamuomba aendelee kuifanya wala asiogope, na kauli yake ya 'Hapa Kazi Tu' iendelee, kwa sababu inaonyesha kwamba sasa nchi yetu itakaa mahali pazuri," alibainisha Mufti Mkuu,

Kadhalika, rais alikutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Alhaji Abdallah Bulembo, ambaye alimpongeza kwa kasi nzuri aliyoanza nayo katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015- 2020 na kutaka kasi hiyo iendelee.

Alisema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayoifanya na kwamba Rais Magufuli amemhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo zaidi katika kutekeleza Ilani ya CCM.

"Tunafurahi kwamba yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa ada za shule, na hivi sasa wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada," alisisitiza Alhaji Bulembo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: