ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 6, 2016

SUMATRA YAWAOMBA WANANCHI KUPENDEKEZA NAULI ZA BRT

 Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT), Bw. David Mgwassa akifafanua jambo wakati wa majadiliano ya wadau juu mapendekezo ya nauli zitakazotumika na mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam jana.  Majadiliano hayo yanaendelea.
Wadau wa sekta ya usafiri wakiwa katika majadiliano ya mapendekezo ya nauli zitakazotumika baada ya kuanza kwa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jana jijini Dar es Salaam.  Majadiliano ya mapendekezo hayo yaliyotolewa na kampuni ya UDA-RT bado yanaendelea. 


Mamlaka ya Udhibi wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) jana imewaomba  wakazi wa Jiji la Dar es Salaam  kupendekeza kwa maandishi ya nauli zitakazotumika katika Mradi wa Mabasi ya Yaendayo Haraka (BRT) wa jijini Dar es Salaam.Huduma  katika kipindi cha mpito zimepangwa kuanza Januari 10, mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA,Bw. Gillird Ngewe, ametoa ombi hilo baada ya nauli zilizopendekezwa naKampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT) kukataliwa na mkutano wa wadau wa usafiri uliofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini jana. UDA-RT itatoa huduma za kipindi cha mpito.
“Tumeletewa mapendekezo haya ya nauli na UDA-RT na wote tumeyajadili na wengi wetu tunahitaji yafanyiwe kazi zaidi.  Tuleteeni mapendekezo yenu. Na sisi tunawaondoa wasiwasi kuwa mapendekezo ya nauli na maoni yenu tutavifanyia kazi,” aliahidi Bw Ngewe.
Ameeleza kuwa  katika  kuamua suala la nauli SUMATRA haiwezi kuangalia tu mapendekezo ya waendeshaji wa mradi mabasi hayo, bali inazingatia pia maoni ya wadau, wananchi na hali halisi ya nchi, na kuahidi kwamba maoni na mapendekezo yote yatapewa uzito wakati wa kuamua nauli za kutumika.
“Sisi ni wadhibiti  maoni yenu yatafanyiwa kazi na endeleni kujenga utamaduni wa kushiriki majadiliano kama ilivyo hivi leo;   hii itasaidia mamlaka kufanya kazi zake kwa urahisi na kwa maslahi ya nchi”, amesisitiza Bw.Ngewe.
Amewahakikishia wananchi kuwa nauli zitakazopangwa ndizo tu zitakazotozwa na wenye mabasi na si vinginevyo.Bw Ngewe ametumia nafasi hiyo kuwataka wenye mabasi ya abiria kufuata sheria kwa kutoza nuali elekezi nchi nzima ili kujenga utamaduni wa kufanya biashara yenye maslahi kwa pande zote mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa UDA-RT,Bw. David Mgwassa, amesifu mchango wa wadau na kuahidi kuutumia katika kupendekeza nauli zenye maslahi kwa pande zote mbili.
“Tunathamini maoni ya wadau na tunaomba pia mamlaka izingatie hali ya uendeshaji wa mabasi ili watumiaji na kampuni tuweze kufaidika na mradi mzima”, alisema,Bw. Mgwassa.
Awali kampuni yake ilipendekeza nauli ya 1,200/- kutoka Kimara hadi Kivukoni na 700/- kutoka Mbezi hadi Kimara Tsh. 700 na 1,400/- kwa njia za mrisho  wa nji kuu.  Mapendekezo yote yalikataliwa na wadau katika mkutano wa jana.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Wakaji la SUMATURA (SUMMATRA Consumers’ Council),Dkt. Oscar Kikoyo, ameitaka mamlaka hiyo kuzingatia maoni ya wadau na nauli zinazotumika sasa ndizo zitumiwe na mradi wa BRT  ili kuwapunguzia wananchi mzigo.Amesema nauli zitozwe kwa kilometa au ukanda na amepinga wazo la nauli ya aina moja kwa barabara nzima.
“Tunatambua kuwa huu ni uwekezaji mkubwa na kwa maoni umekuja kuboresha maisha ya wananchi. Kwa hiyo  nauli za mabasi hay zibaki ni hizi zilizopo”, amesema Dkt. Kikoyo.Wachangia wengine waliona nauli zilizopendekezwa na Kampuni ya UDA-RT ni kubwa mno.

1 comment:

Anonymous said...

unataka mapendekezo mapya ya nini wakati unajua wazi nauli ya mabasi ya umma mijini nchi nzima ni shilingi mia nne.acheni wizi,acheni ubabaishaji.ni lipi msillijua,hamzijui nauli za dala-dala?mnataka mtuongezee wananchi ugumu wa maisha na kuharbu kazi zetu.jee hamjui na sisi malofa tuna mchango mkubwa kwenye PATO LA TAIFA.HAPA,SERIKALI ITULINDE,VINGINEVYO,TUTAKOSA IMANI NA SERIKALI YETU AMBAYO ILISHAANZA KAZI KWA MATUMAINI.