Aliyekuwa mlinzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ofisa usalama mwandamizi, Aloyce Tendewa, amefukuzwa kazi.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, Tendewa amefukuzwa kazi na mwajiri wake ambaye ni Idara ya Usalama wa Taifa (TIS) kwa kosa la kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kikazi.
Mbali na taarifa hizo, imeelezwa pia kuwa sababu nyingine ya kufukuzwa kwake kazi kwa mwanausalama huyo ambayo hata hivyo haijathibitishwa, ni madai ya kutoa taarifa za kubadilishiwa kituo chake cha kazi cha awali.
Inadaiwa kuwa Tendewa baada ya kuvuliwa jukumu la kumlinda Lowassa alibaki na kinyongo moyoni kwa sababu hakuridhika na hatua hiyo hivyo alivujisha taarifa hizo kwa vyombo vya habari jambo lililoelezwa kuwa ni kinyume na maadili ya kazi yake.
Inadaiwa kuwa Tendewa alipewa barua ya kuachishwa kazi juzi jioni baada ya kuvuja kwa uhamisho wake kwenye vyombo vya habari.
“Alikuwa bado anataka kuendelea kumlinda mzee (Lowassa), lakini kuna vitu alishindwa kuvitekeleza kwa ufasaha kwa hiyo kitendo cha kuondolewa kilimuudhi akaamua kupeleka taarifa gazetini jambo ambalo ni kinyume na taratibu zao za kazi za kiusalama,” alidokeza mmoja wa maofisa
Kwa upande mwingine taarifa zinaeleza kuwa mpango wa kutimuliwa kwa Tendewa uliandaliwa kwa muda wa miezi kadhaa na barua ya kufukuzwa iliandikwa baada tu ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.
Kwamba, pamoja na sababu nyingine Tendewa anadaiwa kushindwa kuwasiliana inavyotakikana na viongozi wake kuhusu majukumu yake ya kiulinzi wakati akiwa mlinzi wa Lowassa.
Taarifa zinadai, kushindwa huko kwa Tendewa kuliwafanya viongozi wake kufikia uamuzi wa kumfukuza kazi na kwamba barua yake iliandikwa mapema Desemba mwaka jana, lakini hakukabidhiwa hadi hivi karibuni alipovujisha siri za kuhamishwa kwake kituo cha kazi.
Mmoja wa watoa habari aliyeko serikalini ameeleza kuwa Tendewa aliundiwa kamati ya kumchunguza kuhusu kushindwa kutekeleza majukumu sawasawa ambayo ilifanya kazi kwa muda wa wiki mbili na kuwasilisha ripoti yake makao makuu.
Hata hivyo, alisema bado kuna utata kuhusu mtu aliyesaini barua ya kufukuzwa kazi kwa Tendewa ambaye kwa wadhifa wake ilipaswa kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu lakini badala yake imesainiwa na ofisa wa cheo cha chini.
Tendewa amefukuzwa kazi akiwa amebakiza mwaka mmoja kustaafu utumishi wake katika Idara ya Usalama wa Taifa.
Rekodi za utendaji kazi wa Tendewa zinaonyesha kuwa baada tu ya kuajiriwa na TIS, alipelekwa katika kikosi cha walinzi wa hayati Mwalimu Julius Nyerere na kutokana na uhodari wake aliaminiwa na Mwalimu.
Aidha, rekodi hizo zinaonyesha kuwa Tendewa ni miongoni mwa wana usalama wachache waliopigana vita ya kumng’oa aliyekuwa Rais wa Uganda, Fashisti Iddi Amini Dada mwaka 1978 na 1979 na akiwa vitani alitekwa na kwenda kuzuiliwa nchini Sudan.
Historia hiyo inaonyesha kuwa Tendewa aliokoka kuuawa kwa risasi akiwa mateka muda mfupi baada ya kurejeshwa nchini kutoka Sudan siku chache baada ya Rais Yoweri Museveni kushika madaraka ambapo mmoja wa walinzi wanawake wa rais alimuona na kumtambua kuwa alikuwa mmoja wa wapiganaji hodari wa Tanzania na si muasi kama ilivyokuwa ikidhaniwa hivyo alirudishwa Tanzania.
Baada ya kurejeshwa nyumbani alipewa jukumu la kuwa mlinzi wa Mwalimu Nyerere na hata alipong’atuka madarakani aliendelea na kazi hiyo hadi Mwalimu alipofariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas London nchini Uingereza.
No comments:
Post a Comment