Sunday, January 3, 2016

MISAADA YA MBUNGE LWAKATARE (CHADEMA ) YAKATALIWA HOSPITALINI

Baadhi ya wakuu wa vituo vya afya na zahanati katika Manispaa ya Bukoba, wamegoma kupokea misaada kwa ajili ya wajawazito uliotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kwa madai ya kupewa maelekezo na Serikali.
Mbunge huyo mwishoni mwa wiki alikuwa akisambaza vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati, lakini wasimamizi walikataa kuvipokea, huku wengine wakikimbia wakidai walipewa maelekezo na viongozi wao kutovipokea.
Katika hali ya kushangaza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Richard Mihayo ambaye alikuwa katika msafara wa mbunge huyo alitoweka ghafla baada ya kufika Kituo cha Afya cha Zamzam, huku Kaimu mganga, Samwel Chaba akigoma kupokea vifaa hivyo.
Baada ya mkurugenzi kutoweka, mbunge huyo alilazimika kutelekeza vifaa hivyo kituoni hapo na kwenda Zahanati ya Kashai ambako Kaimu Msimamizi wa zahanati hiyo, Emmanel Luviga alikubali kuvipokea.
Katika Kituo cha Afya Rwamishenye vifaa hivyo vilipokewa na wauguzi waliogoma kuzungumza suala lolote.
Baada ya kufika Zahanati ya Kagemu, Msimamizi wake Glory Sailo aligoma kupokea vifaa kwa ajili ya mama wajawazito kwa madai ni maelekezo ya viongozi.
Hatua ya viongozi kuweka vikwazo kwenye upokeaji wa vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni ililalamikiwa na Lwakatare aliyedai aliandika barua manispaa na kutoa nakala hadi ngazi ya mkoa, lakini Mganga Mkuu wa manispaa hiyo, Dk Hamza Mgula alisema hajui lolote kuhusu suala hilo.
Akizungumzia suala hilo, Mihayo alisema kwa kawaida vifaa vya tiba ni lazima vikaguliwe na mganga mkuu wa manispaa ili kuthibitisha ubora, hivyo haviwezi kupelekwa bila kuthibitishwa.

CHANZO: MWANANCHI

7 comments:

Anonymous said...

Wakati huo huo misaada ya Nape inaruhusuwa na serikali hiyo hiyo? Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki democrasia

Anonymous said...

Milioni tatu?

Anonymous said...

Huu ni ujinga. Utakataaje misaada ya kusaidia Afisi yako ili itoe huduma bora kwa wananchi. Tusiingize siasa kwenye maendeleo. Naamini hata Magufuli atamshukuru Lwakatare. Hebu tufanye kazi kwa kushirikiana: uchaguzi umekwisha amesema Magufuli.

Anonymous said...

Mdau wa 1:13 PM, tafadhali jaribu kuelewa regional politics. Politics ya Bukoba/Kagera ni tofauti sana na ile ya Mtama/Lindi. Kagasheki na CCM ndo walikuwa wanatawala Bukoba mjini, na hivyo kuanguka kwa Kagasheki katika uchaguzi uliopita kumeleta bad blood kati ya CCM na Chadema. Hakuna jema Lwakatare can do to appease die-hard Kagasheki followers under the CCM umbrella. Kumbuka, Mtama/Lindi ni ngome ya CCM for decades, na hivyo Nape can do whatever he wishes!

Unknown said...

Nchi ya ajabu Hii CCM badilikeni tuko katika mfumo wa vyama vingi

Anonymous said...

Hakuna Bukoba wala Lindi kuna Tanzania tu. Hapa kazi tu. Uchaguzi umekwisha mwenye kutaka kuchangia shule hata penceli anakaribishwa. Magufuli adumu!

Anonymous said...

But look here mate: hii ni tz, hatuko kwenye siasa za majimbo hapa bado. Swali la msingi ni Kwa nini serikali kuu okataze vyama vingine kufanya yale ambayo ccm inayafanya? Regardless ya eneo la nchi yetu? Hypocrisy at best!!