ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 12, 2016

MASHAMBA 17 YAFUTIWA UMILIKI NA SERIKALI MKOANI PWANI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akikagua mafaili ya hati za ardhi za wananchi yanayodaiwa kukaa kwenye shelvu kwa zaidi ya miaka mitatu pasipo kufikishwa kwa wahusika. Anayempa maelezo ni Afisa Ardhi Mteule, Majaliwa Jaffari. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akikagua mafaili ya hati za ardhi za wananchi yanayodaiwa kukaa kwenye shelvu kwa zaidi ya miaka mitatu pasipo kufikishwa kwa wahusika. Anayempa maelezo ni Afisa Ardhi Mteule, Majaliwa Jaffari. 


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema Serikali imefuta umiliki wa mashamba 17 ambayo hayajaendelezwa katika Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na viongozi wa mkoa huo, Lukuvi alisema Serikali imefuta mashamba hayo baada ya mkoa kutoa mapendekezo ya kutaka yafutwe kwa sababu hayajaendelezwa.
“Baada ya kupata mapendekezo ya mkoa tumefuta miliki ya mashamba lakini wamiliki ni wananchi wa kawaida, mbona vigogo wenye mashamba yasiyoendelezwa hamjawagusa, mnawaogopa? ” aliwahoji viongozi hao.
Lukuvi aliagiza ukaguzi ufanyike kwenye mashamba yote mkoani na kutoa mapendekezo kwa wizara ili yafutwe bila kuangalia cheo wala rangi ya mtu.
Alisema migogoro ya ardhi haiwezi kumalizika kama viongozi watakuwa wanafanya kazi kwa kuangalia vyeo vya watu.
“Msimuogope mtu hata kama ni kigogo lakini msimuonee mtu, tendeni haki,” alisema.
Lukuvi alisema kuna wamiliki 35 wa mashamba mkoani humo ambao wametumia hati za mashamba hayo kukopa mamilioni ya fedha benki, lakini fedha hizo wamezitumia kwenye miradi mingine isiyo na uhusiano wa mashamba hayo.
Alisema pamoja na kukopa fedha hizo, lakini mashamba waliyotumia kupata mikopo wameyatelekeza bila kuyaendeleza.
“Wako watu wamekopa kwa kutumia mashamba ya Mkoa wa Pwani lakini fedha walizopata wamekwenda kujenga nyumba za kupangisha Kigamboni (Dar es Salaam) na mashamba hawayaendelezi tutawanyang’anya,” alisema.
Lukuvi alisema atatoa orodha ya watu hao kwa uongozi wa mkoa ili uweze kuyakagua na kutoa taarifa kwa wizara.
“Hatuwezi kuwatajirisha watu wa Dar es Salaam kwa kutumia mashamba ya Mkoa wa Pwani,” alisema.
Lukuvi alitoa orodha ya mashamba 50 ambayo yamenunuliwa kwenye vijiji vya mkoa huo, lakini hayajaendelezwa na kusababisha migogoro ya ardhi.
“Kutoendeleza mashamba kunasababisha migogoro ya ardhi kwani hivi sasa kuna watu wanayavamia,” alisema.

Bei elekezi ya viwanja
Waziri alisema wizara itatoa bei elekezi katika uuzaji wa viwanja kwa lengo la kupunguza bei.
Alisema hivi sasa halmashauri zimekuwa zikichukua mashamba na kupima viwanja na kuviuza kwa mamilioni ya fedha ambayo si rahisi kwa mwananchi wa kawaida kumudu.
Alisema matokeo yake, viwanja hivyo vimekuwa vikinunuliwa na matajiri kwa malengo ya kuviuza kwa bei kubwa huku watu wa kawaida wakiendelea kujenga kwenye maeneo yasiyopimwa.
“Halmashauri msifanye biashara katika viwanja, hii ni huduma sasa tunaweka bei elekezi ili kila mwananchi aweze kununua,” alisema.
Alizitaka halmashauri zilizochukua mashamba ya watu na kuyapima viwanja kuwalipa fidia kabla ya Juni.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mgeni Baruani alimueleza waziri kwamba mkoa huo una migogoro ya ardhi hasa zile zinazopakana na Mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akisaini kitabu cha wageni alipowasili Ofisi ya mkoa wa Pwani kukagua utendaji wa kazi kuzungumza na wananchi pia kusikiliza malalamiko na kero zao kuhusu maswala ya ardhi alipokuwa kwenye ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kibaha jana. 
Wantedanji na viongozi wakimsikiliza Waziri Lukuvi. 
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Bi. Halima Kiemba akimsomea muhtasari Waziri wakati wa kikao na viongozi pamoja na watendaji wa wilaya hiyo Mkoa wa Pwani jana. Kutoka (kulia) ni Mkubge wa Kibaha, Mhe. Koka Foka na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mgeni Bauani. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akiongea na wafanyakazi na watendaji wa Halmashauri ya Kibaha pamoja katika kikao nao kabla kuzungumza na wananchi na kusikiliza malalamiko na kero zao kuhusu maswala ya ardhi alipokuwa kwenye ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani jana. 
Waziri Lukuvi akielekeza jambo alipotembelea eneo la Stendi ya mabasi eneo la Kibaha Maili moja na kujadili namna ya kufanikisha mradi wa ujenzi wa kituo hicho. Kushoto ni Mbunge wa Kibaha, Mhe. Koka Foka na Mkuu wa Wilaya hiyo Halima Kiemba. 
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akisikiliza kero za Bi. Zena Shabani kabla kupokea vielelezo vya malalamiko na kero za kuzulumiwa ardhi yenye hekari 50 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Mchechu kutoka kwa Zena Shaban (85) alipokuwa katika ziara ya kikazi kusikiliza malalamiko ya wananchi Kibaha Mkoa wa Pwani jana. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akipokea vielelezo vya malalamiko na kero za kuzulumiwa ardhi yenye hekari 50 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Mchechu kutoka kwa Zena Shaban (85) alipokuwa katika ziara ya kikazi kusikiliza malalamiko ya wananchi Kibaha Mkoa wa Pwani jana. 
Mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo akitoa kero zake kwa Waziri. 

No comments: