Tuesday, January 5, 2016

Mawaziri CUF waenguliwa uzinduzi wa miradi Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeamua kuwaengua mawaziri kutoka Chama cha Wananchi CUF katika ratiba ya uzinduzi wa miradi ya Maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi kufuatia msimamo wao wa kutoitambua serikali ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

Kwa mujibu wa ratiba ya sherehe hizo iliyotolewa jana mjini Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, serikali imeamua miradi yote kuzinduliwa na mawaziri kutoka chama tawala cha CCM, wakiongozwa na Rais Dk. Shein.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana, Balozi Seif alisema uwekaji wa mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi utafanywa na mawaziri wanaotoka CCM kutokana na mawaziri wa CUF kutokuonekana kazini tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani hapa.

“Ratiba ya sherehe za mapinduzi imekamilika na mwaka huu jumla ya miradi 16 itazinduliwa kati ya 24, ikiwamo ya huduma za jamii,”alisema.
Balozi Seif alisema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, pia amekataa kushiriki katika uzinduzi wa miradi ya maendeleo kwa madai serikali ya awamu ya saba imemaliza muda wake wa kubakia madarakani.

Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 28(1) (a) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Rais Dk. Shein bado ni Rais halali hadi Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais.

Alisema SMZ pia bado inawatambua mawaziri wa CUF kuwa ni mawaziri halali kwa mujibu wa Katiba, ndiyo maana wanaendelea kulipwa mishara na marupumarupu mengine na hakuna hata mmoja aliyerejesha fedha hizo serikalini.

Mawaziri walioenguliwa katika uzinduzi wa miradi hiyo ni wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Afya, Rashid Seif Suleiman, Waziri wa Habari, Utamaduni Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji, Waziri wa Mifungo na Uvuvi, Abdillah Jihadi Hassan, Waziri asiyekuwa na wizara maalum, Haji Faki Shaari na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakar.

Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mtumwa Kheir Mbaraka, Naibu Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahara Ali Hamad
CHANZO: NIPASHE

No comments: