Monday, January 11, 2016

MH.LUKUVI APIGA MARUFUKU HALMASHAURI KUACHA KUCHUKUA MASHAMBA YA WANANCHI BILA KUWALIPA.

Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mh William Lukuvi amepiga marufuku halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kuchukua mashamba ya wananchi masikini bila kuwalipa fidia kisha kupima viwanja na kuviuza kwa bei kubwa huku wanunuzi wa viwanja hivyo majina yakijirudia nchi nzima kwa lengo la kufanya biashara ya ardhi.
Amepiga marufuku hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kibaha mkoani Pwani saa chache baada ya kuzungumza na uongozi wa mkoa wa Pwani na serikali ya wilaya ya Kibaha akiagiza mashamba yasiyoendelezwa wala kulipiwa tozo kwa muda mrefu yakiwemo ya vigogo yatolewe notisi ili yafutwe na kurudisha mikononi mwa serikali ambapo amesema serikali haitaki kuwepo na biashara ya viwanja hivyo wizara yake pekee ndiyo itatoa bei dira ya viwanja.
Awali akizungumza na viongozi wa serikali ya mkoa wa Pwani na halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mh Lukuvi aliwataka maafisa ardhi wateule kuhakikisha wananchi waliolipia ada na tozo mbalimbali za ardhi tangu mwaka 2002 wanapewa hati zao si zaidi ya mwezi mmoja ili wasifukuzwe kazi na kupunguza chuki na wananchi.
Aidha, Mh, Lukuvi akiwa wilayani Kibaha alitembelea kitovu cha mji wa Kibaha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na soko ambao ujenzi wake licha ya kupata kibali Tamisemi unasuasua ambapo katika mkutano wake akatoa fursa kwa wananchi kutoa kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika ardhi ili aweze kuifanyia kazi.

CHANZO: ITV TANZANIA

No comments: