ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 6, 2016

SERIKALI YAWAOMBA WANANCHI KUTII SHERIA ZA ARDHI BILA SHURUTI.

 Mkurugenzi Msaidizi wa usimamizi na udhibiti wa uendelezaji miji Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makazi, George Pangawe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na Zoezi la bomoa bomoa linaliendelea katika kingo za mto Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi wa usimamizi na udhibiti wa uendelezaji miji Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makazi, George Pangawe jijini Dar es Salaam leo. Picha na Emmanuel Massaka.

Na Avila Kakingo.
SERIKALI yawahimiza wananchi waliojenga makazi kwenye sehemu hatarishi, kingo za mito na maeneo ya wazi kuhama kwa hiyari yao ili kupisha Oparesheni ya bomoa bomoa kuendelea bila kikwazo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa usimamizi na udhibiti wa uendelezaji miji Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makazi, George Pangawe wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Pangawe amesema kuwa Serikali itahakikisha haki inatendeka kwa wananchi wote pia itahakikisha haki na usawa wa pande zote wakati wa utekelezaji wa zoezi la bomoabomoa linaloendelea tangu lilipoaza tena Januari 5 mwaka huu.
Zoezi la bomoabomoa linaendelea jijini Dar es Salaam katika kingo za mto Msimbazi ili kuepusha wananchi kupatwa na madhara mbalimbali ambayo huwa yanakitokeza wakati wa mvua kubwa na masika.
Pangawe pia amesema kuwa bonde la mto msimbazi liliainishwa kama ni sehemu hatarishi kwa makazi ya binadamu tangu 1979 na wananchi wa maeneo ya mto huo wakaanza kuvamia kutokana uhaba wa maeneo ya makazi na kuanza kujenga katika kingo za mto huo.
Pia amewasihi wananchi kutii sheria za ardhi bila shuruti ili kuepukana na madhara mbalimbali yanayojitokeza pamoja na upotevu wa mali zao.

No comments: