ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 31, 2016

SIKU NNE SHUBIRI KWA SERIKALI BUNGENI

Zilikuwa siku nne ngumu kwa Serikali bungeni. Ndivyo unavyoweza kuelezea hali ilivyokuwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria katika siku za mwanzo za mkutano wa pili wa Bunge la Kumi na Moja.
Mkutano huo ulioanza Jumanne, ulikumbwa na mlolongo wa maombi ya mwongozo kuhusu uamuzi wa kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge.
Jumanne ilikuwa siku ya kujadili hotuba ya Rais John Magufuli, na siku ya pili tu wabunge wa upinzani walihoji uamuzi wa TBC kupunguza matangazo ya moja kwa moja, wakiwasema unawanyima wananchi haki ya kikatiba ya kupata habari.
Jumatano mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko aliuliza swali kuhusu elimu bure na baada ya majibu, wabunge wengi walisimama kutaka kuomba mwongozo na waliponyimwa walipiga kelele zilizosababisha mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuita polisi ili wawaondoe wabunge wa upinzani kwa nguvu.
Ijumaa uongozi wa Bunge ulisimamisha shughuli zake hadi kesho baada ya wabunge wa upinzani kuilazimisha Serikali kuondoa Mapendekezo ya Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano baada ya kung’amua kuwa ni kinyume cha kanuni zinazotaka Bunge la kwanza baada ya uchaguzi, lijadili Mpango wa Maendeleo na si mwelekeo.
Wabunge waliozungumza na gazeti hili jana walisema mambo hayo yamejitokeza kutokana na ugeni wa wabunge na viongozi wa kamati, na kusisitiza kuwa kazi ya Bunge ya kuishauri Serikali imefanyika ndani ya siku hizo nne.
Kauli za wabunge
Mbunge wa Jimbo la Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia alisema Serikali haikuwa imejipanga.
“Hilo limeonekana katika uteuzi wa mawaziri, uteuzi wa wajumbe wa kamati, uchaguzi wa wenyeviti wake na uteuzi wa naibu spika,” alisema akizungumzia sababu ya mwambo kwenda kombo.
Alisema viongozi walikosa umakini kwa kuleta bungeni mambo nyeti bila kujiandaa, akitoa mfano wa suala la TBC na Mpango wa Pili wa Maendeleo.
“Sisi (wapinzani) tulikuwa makini zaidi maana tulikuwa tukitafuta kasoro ndogo katika hoja zinazowasilishwa na Serikali, matokeo yake Serikali imekuja na makosa makubwa katika hoja zake,” alisema Mtulia.
“Tazama ule mpango. Sisi tulieleza kasoro na ukaondolewa. Kama tusingekuwepo bungeni ni wazi kuwa Serikali ingepitisha jambo la hovyo kabisa,” alisema.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema: “Kama ningekuwa na uwezo ningeanza kwa kuwachapa viboko wabunge wa CCM kwa kile walichokifanya jana (juzi).
“Serikali ya CCM inajigamba kuwa inabana matumizi wakati juzi imetumia fedha nyingi kuwalipa askari na kujaza mafuta katika magari kwa kazi ya ajabu ya kuwashughulikia wabunge wa upinzani walioibua hoja za msingi bungeni.”

No comments: