Hospitali hiyo kwa muda mrefu ilikuwa na shida ya vitanda, hali iliyosababisha wagonjwa wengi kulala sakafuni mpaka Rais wa tano, John Magufuli alipoagiza kununuliwa kwa vitanda 300 kutoka fedha ambazo ilikuwa zitumike kwa ajili ya sherehe ya uzinduzi wa Bunge la 11, Novemba 20 mwaka jana.
Nipashe ilizunguka kwenye wodi mbalimbali kutaka kujua hali ikoje baada ya kutolewa kwa vitanda vya Magufuli na kukuta baadhi ya vitanda vikiwa vitupu, hali ambayo haikuwepo awali.
Watu kadhaa waliolazwa hospitalini hapo na ambao walizungumza na gazeti hili, walielezea kushangazwa na uwepo wa vitanda vingi kuliko mahitaji, wakisema haijawahi kutokea mgonjwa kuchagua kitanda cha kulala kwenye wodi.
“Ili upate kitanda wakati ule lazima ndugu zako wazungumze vizuri na wauguzi ili mgonjwa mmoja akiruhusiwa uwekwe kitandani maana wagonjwa wanakuwa wengi hadi sehemu ya kukanyaga inakuwa shida,” alisema Hassan Abdul, wodi namba 18 Sewahaji.
"Lakini sasa hivi unaweza kujionea mwenyewe hali ilivyo."
Alisema alipofikishwa hospitalini hapo wiki tatu zilizopita kutokana na ajali ya gari, alipatiwa kitanda na anaendelea vizuri na matibabu na kwamba ameshuhudia wagonjwa mbalimbali wanaofika kwenye wodi hiyo wakipatiwa vitanda kwasababu hakuna uhaba.
"Mimi ndio mara yangu ya kwanza kulazwa hapa, napata huduma nzuri kitu ambacho hata ndugu zangu wanashangaa ingawa nimesikia kwa watu kwamba ujio wa Rais Magufuli ndio umesababisha wauguzi na madaktari kuongeza ubora wa huduma zao," alisema.
"Wenzangu ambao nimewakuta wananiambia kabla ya ujio wa Magufuli hali haikuwa hivi, madaktari wanakujali na hata ukipangiwa vipimo unapelekwa kwa muda unaotakiwa... yaani hakuna ucheleweshaji," alisema Chatherine Njau aliyelazwa wodi ya Kibasila.
Aidha, Nipashe iligundua usafi wa wodi mbalimbali umeongezeka tofauti na hali ya miaka mingi na wagonjwa waliohojiwa walisema wanadhani imechangiwa na ziara ya ghafla ya Rais Magufuli hospitalini hapo, Novemba 9, mwaka jana.
Akizungumzia maboresho hayo, Ofisa Habari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Patrick Mvungi alisema hakuna mgonjwa anayelala chini au kukosa nafasi katika wodi wanazohudumia.
"Hakuna mgonjwa anayelala chini kwa sasa, vitanda vipo vingi na vingine vimekosa watu wa kuvitumia, naomba watanzania waendelee kutumia hospitali yao kikamilifu maana tumeboresha huduma na hakuna kulala chini," alisema Mvungi.
Wakati akizindua Bunge la 11 Mjini Dodoma, Novemba 20 mwaka jana, Rais Magufuli aliagiza zaidi ya milioni 200 zilizopangwa kutumika kwa ajili ya vinywaji na chakula vya sherehe ya kuwapongeza wabunge, zipelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kununulia vitanda na mashuka.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
1 comment:
Ukiona hivyo hao wameanza kupata nafuu, wanatakiwa waruhusiwe kwenda nyumbani. Mgonjwa achagui kitanda.
Post a Comment