Katika hali isiyokuwa ya kawaida wanafunzi wa Shule ya sekondari binafsi ya Buluba iliyopo mjini Shinyanga wameandamana na mabango hadi makao makuu ya Chama cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) wakipinga kitendo cha kufukuzwa kazi kwa mkuu wa shule hiyo, Alexander Yegela.
Tukio hilo limetokea jana asubuhi ambapo wanafunzi hao waliandamana wakiwa na mabango huku wakidai wamefanya hivyo kutokana hatua ya uongozi wa bodi ya shule kumfukuza ghafla mkuu wao ambaye amefanya kazi katika shule hiyo kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Hali hiyo iliwalazimu baadhi ya askari wa Kikosi cha kutuliza Ghasia (FFU) kilichopo jirani na makao makuu ya SHIRECU kufika katika ofisi hizo na kufanikiwa kutuliza jazba waliyokuwa nayo wanafunzi ambao tayari walianza kufanya fujo kwa kurusha mawe na kuvunja baadhi ya milango ya ofisi hizo.
Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la makao makuu ya SHIRECU ambao ni wamiliki wa shule hiyo wanafunzi hao walielezea kushangazwa kwao na kitendo cha bodi ya kumfukuza mwalimu siyo cha kiungwana.
Wanafunzi hao walidai mtu aliyechaguliwa kuchukua nafasi ya mkuu huyo wa shule waliyemtaja kwa jina la John Ndama hana uwezo wa kuiongoza shule hiyo kutokana na uwezo wake mdogo na kwamba mara nyingi amekuwa akijishughulisha na masuala ya kisiasa.
Wakifafanua hatua ya kupinga kutimuliwa kwa Yegela wanafunzi hao walisema wao binafsi hawakubaliani na hatua iliyochukuliwa na uongozi wa SHIRECU kwa vile hawakushirikishwa wala kuelezwa makosa ambayo yamesababisha afukuzwe kazi.
Mmoja wa wanafunzi hao aliyekuwa miongoni mwa kundi kubwa la wanafunzi walioandamana aliyejitambulisha kwa jina la George Boniphace alisema wameamua kuandamana maandamano ya amani kwa lengo la kupinga na kuonesha kutokubaliana na uamuzi uliochukuliwa ghafla na uongozi wa bodi ya shule yao.
“Kwa kweli tumekasirishwa sana na hatua ya viongozi wa SHIRECU kuchukua maamuzi ya ghafla ya kumsimamisha mkuu wetu wa shule Mr. Yegela (Alexander), hatuelewi tatizo, tuna baraza la wanafunzi pale shuleni halikushirikishwa, ghafla tunatangaziwa mkuu mpya wa shule eti sasa ni Mr. Ndama, sisi huyu hatumtaki”,alieleza mwanafunzi huyo.
“Tunataka Yegela arudishwe kazini, huyu mwalimu tangu alipohamishiwa hapa Buluba amebadilisha hali ya shule kwa kiasi kikubwa na ameongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha tano, leo hii ghafla anafukuzwa kazi, ukweli na misimamo yake ya kupenda haki itendeke isiwe sababu ya yeye kufukuzwa,” alieleza Boniphace.
Hata hivyo wanafunzi hao walisema kutokana na mwalimu wao kutumbuliwa jipu hawataingia madarasani mpaka waone
mwalimu mkuu anakabidhiwa ufunguo wa ofisi yake ya mkuu wa shule,
ambapo baada ya kuona kimya waliamua kufunga baadhi za ofisi za shule hiyo.
Kwa upande wake aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Alexander Yegela alisema tayari amepokea barua ya kupunguzwa cheo na kutakiwa kuwa mwalimu wa kawaida
kwa madai kwamba tume ilichunguza na kubaini kuwa anawagawa walimu anafelisha wanafunzi pia anajenga mahusiano mabaya kwa walimu.
“Mpaka sasa ninayo barua niliyopewa ya kushushwa kazi na kuwa mwalimu wa kawaida kwa makosa hayo yaliyotajwa, na sasa anakaimu mwalimu John Ndama ambaye alikuwa mwalimu wa kawaida, mimi nawasikiliza wao kwani
ni shule yao wana haki yao ya kunishusha na kuweka walimu waowanaowataka sina zaidi ya kusem”,alisema Yegela.
Akizungumzia tukio hilo, Meneja Mkuu wa SHIRECU, Joseph Mihangwa alikiri kufanyika kwa maandamano ya wanafunzi hao wakipinga kitendo cha kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa mkuu wa shule yao bila ya wao kushirikishwa.
Hata hivyo Mihangwa alifafanua kuwa Yegela hajafukuzwa kazi bali amebadilishwa nafasi yake ya ukuu wa shule na aliyechuka nafasi hiyo kwa sasa ni, John Ndama ambaye hata hivyo amepewa kushikilia kwa muda wakati Bodi ya shule ikitafuta mwalimu mwenye sifa za kuweza kuwa mkuu wa shule.
“Hatua ya kuondolewa kwenye ukuu wa shule ni mambo yaliyomo ndani ya utawala wa shule, na hii inatokana na matokeo ya uchunguzi wa tume iliyokuwa imeundwa mwaka 2014 kuchunguza mwenendo mzima wa kiutawala katika shule hiyo, hivyo tumewasihi wanafunzi watulie wasubiri maamuzi ya mwisho,” alieleza Mihangwa.
Aidha Mihangwa alisema mkataba wa Yegela kati yake na uongozi wa shule hiyo unakamilika mwezi Machi mwaka huu na kwamba wamewaomba wanafunzi warejee madarasani waendelee na masomo kama kawaida na iwapo wasipotii agizo hilo hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa dhidi yao.
MOHAB MATUKIO
No comments:
Post a Comment