ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 26, 2016

Watu wawili wadakwa wakiwa na bomu la mkono

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya
By Anthony Kayanda, Mwananchi

Kigoma. Polisi mkoani Kigoma wanawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa wakiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la mkono katika Wilaya ya Uvinza.

Kamanda wake, Ferdinand Mtui alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Hata hivyo, Kamanda huyo hakutaja aina ya bomu hilo na ukubwa endapo lingelipulika kwa kuwa wataalamu wa milipuko wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walikuwa wanaendelea kufanya uchunguzi .

Alisema wataalamu hao walikuwa wanafanya uchunguzi ili kubaini aina ya bomu hilo na viwango vyake kabla ya kuliteketeza ili kuepusha madhara kwa jamii.

Hata hivyo, Kamanda Mtui hakuwataja majina watuhumiwa hao akisema upelelezi wa tuhuma dhid yao haujakamilika.

Warundi watiwa mbaroni

Polisi wilayani Kasulu wamewakamata raia 15 wa Burundi kwa tuhuma za kuingia nchini na kufanya vibarua bila ya kuwa na vibali.

Watuhumiwa hao walikamat kwenye mashamba yaliyopo katika Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini, unaojulikana kama pori la Kagerankanda.

Kamanda Mtui alisema kuwa watuhumiwa hao walikuwa wameajiriwa kulima mashamba hayo kinyume cha sheria na kwamba wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka baada ya upelelezi kukamilika.

Kigoma unakabiliwa na wimbi la raia wa Burundi wanaoingia nchini kinyume cha taratibu za uhamiaji kwa ajili ya kufanya kazi za vibarua kwa wenyeji hususan ya mkoani humo na mingine ya Tabora na Katavi kwa kulipwa ujira.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya alitoa wito kwa wakazi wote kuacha tabia ya kuwaajiri wahamiaji haramu kufanya kazi za kilimo na uvuvi kwa kuwa ni kosa kisheria.

Alionya kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu atakayebainika kufanya hivyo.     

No comments: