ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 6, 2016

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KIWANDA CHA TUMBAKU MKOANI RUVUMA NA KUWASIMAMISHA KAZI VIONGOZI WA CHAMA CHA USHIRIKA CHA SONAMCU

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kusindika tumbaku cha mkoani Ruvuma na kuwasimamisha kazi viongozi wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika cha SONAMCU.



Akizungumza jana jioni(Jumanne, Januari 5, 2016), katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo ya Songea, wakati alipokutana na wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Namtumbo, Wananchama wa Vyama Vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Mkoa pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Waziri Mkuu amesema, Serikali ina dhamira ya kufufua kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU, na lengo la kutembelea kiwanda hicho ni katika utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli la kufufua viwanda nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea maeneno mbalimbali ya kiwanda hicho na kukagua mitambo iliyokua ikitumika kusindika tumbaku, kabla kiwanda hicho kuzimwa miaka kadhaa iliyopita baada ya kukosa malighafi za kuendelea na uzalishaji. 
Pia, amemtaka Afisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bibi. Stela Lugongo kuandaa na kuwasilisha kwake mkakati wa kufufua kiwanda hicho cha kusindika tumbaku, na baadae kuwasimamisha kazi viongozi wote wa Chama Kikuu cha Ushirika cha SONAMCU waliohusika na tuhuma hizo na kutaka wafikishwe Mahakamani.


“Serikali imeazimia kufufua viwanda, hasa vile ambavyo havina wawekezaji vimebaki vyenyewe, Tunahitaji kujua namna ya kuvifufua”. Alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa pia, amesikiliza na kujibu kero mbalimbali za wakulima wa tumbaku wa Mkoa huo, ambao walilalamikia mfumo wa Vyama vya Ushirika na namna ambavyo vyama hivi vimekua vikiwaibia fedha zao hadi kushindwa kuendelea kulima zao la tumbaku na kukosa masoko ya mazao yao.
Aidha, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kuwa watulivu na kusubiri maamuzi ya Mahakama baada ya kuwa viongozi wa Chama cha Ushirika SONAMCU ambao wamehusika na wizi wa fedha za wakulima kiashi cha Shilingi milioni 800 kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014 tayari wamefikishwa Mahakamani na uchunguzi unaendelea. Pia, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu kukutana na wakulima hao ili kupatia ufumbuzi matatizo yao.
Aidha, ametoa wito kwa wakulima kuendelea kulima zao la tumbaku kwa kuwa linaongeza pato la mtu mmoja mmoja, linasaidia kuchangia pato la Mkoa na kukua kwa uchumi wa nchi. Amewashauri wakulima kuunda na kuviendesha Vyama Vya Ushirika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. 
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake mkoani Ruvuma, atafanya majumuisho ya ziara hiyo leo, kabla ya kuagana na viongozi wa Chama na Serikali na kurejea jijini Dar es Salaam. 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMMATANO, JANUARI 6, 2016.

No comments: