Mwanza. Meneja wa Wakala wa Umeme na Ufundi (Temesa) Mkoa wa Mwanza, Ferdinand Mishamo amesema wanaboresha mfumo wa ukataji tiketi katika Kivuko cha Kigongo-Busisi wilayani Misungwi, ili kuanza kutumia kadi maalumu kwa watumiaji wa usafiri huo.
Akizungumza ofisini kwake jana, Mishamo alisema mfumo huo wa kutumia kadi unalenga kuboresha huduma na kuondoa usumbufu kwa watumiaji hao wa kukata tiketi kila siku.
“Mhandisi kwa sasa anaboresha mfumo huo ili tuanze kutumia kadi maalumu kwa wateja wa kila siku, kama mabasi na wafanyabiashara ili kuondokana na ukataji tiketi wa kila siku.
Licha ya njia hiyo kutuongezea mapato, pia itarahisisha huduma ya kuvuka bila usumbufu,” alisema.
Mishamo alisema uwapo wa mfumo wa kielektroniki katika kivuko hicho umeongeza makusanyo ikilinganishwa na awali.
“Tangu tufunge hii mitambo ya kielektroniki Septemba 2014, makusanyo yameongezeka kutoka Sh8 milioni tulizokuwa tukikusanya hadi kufikia Sh12 milioni kwa siku,” alisema.
Alisema ongezeko hilo limetokana na udhibiti wa udanganyifu uliokuwa ukifanyika awali.
Baadhi ya abiria wanaotumia kivuko hicho, Ashura Katare na Reontine Asanterabi walidai kuwa kuna wakati hukaa kwa zaidi ya saa moja kusubiri usafiri huo, hivyo kuutaka uongozi kulifanyia kazi suala hilo.
Mkuu wa kivuko hicho, Atiki Abdallah alisema licha ya kutakiwa kufanya kazi saa 24, hulazimika kupunguza muda kutokana na gharama za uendeshaji.
“Ikifika saa sita usiku watu na magari hupungua, hivyo wakati mwingine tunalazimika kusubiri kwa sababu hatuwezi kuvusha mtu mmoja kwenda upande mmoja.
Hiyo itakuwa ni hasara,” alisema.
No comments:
Post a Comment