Advertisements

Saturday, February 13, 2016

BOMBA LA MCHEPUKO LAWANG’OA VIGOGO



Siku moja baada ya kugundua bomba la mchepuko lililokuwa likisambaza mafuta ya wizi bandarini, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi mtendaji mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) na meneja wake aliyekuwa kitengo cha bandari.


Mtendaji huyo mkuu, Magdalena Chuwa, na meneja wa kitengo cha bandari, Bernadina Mwijarubi wamesimamishwa kazi kuanzia jana ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini baada ya mamlaka hiyo kuzuia kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha makatibu wakuu kilichofanyika jana ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alimuagiza katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Adelhelm Meru kuwaandikia watumishi hao barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi.
“Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.
Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itaiandikia barua ofisi ya Takukuru na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja, na ikithibitika kuwa walihusika hatua zitachukuliwa na kama itathibitika hawakuhusika, watarudishwa kazini.
Pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia mita (flow meters) uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uachwe mara moja.
Juzi, Waziri Majaliwa alifanya ziara kukagua mita za zamani zilizopo Kurasini na kisha akatembelea na kukagua mita mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu Sh12.96 bilioni.
Pia alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya Tiper yaliyoko Kigamboni na ambayo yanaymilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa kampuni ya Tiper imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kuu la mafuta linalotoka bandarini, hali iliyomlazimu Majaliwa kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Jana (juzi) niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema.

No comments: