ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 18, 2016

DKT. KALEMANI AAGIZA WADAIWA SUGU WA UMEME ‘WASHUGHULIKIWE’

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ishihimulwa, Kata ya Bukumbi, wilaya ya Nzega hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora.
Nyaya za umeme katika Kijiji cha Mambali, Wilaya ya Nzega. Kijiji hiki ni miongoni mwa vijiji vilivyounganishiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Awamu ya Pili ya REA.


Na Veronica Simba - Nzega

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafikisha Mahakamani wadaiwa wake sugu hususan Kampuni na watu binafsi.

Dkt Kalemani alitoa agizo hilo jana wilayani Nzega, akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Tabora kukagua miradi mbalimbali ya sekta za nishati na madini inayotekelezwa chini ya Wizara yake.

Alisema, Serikali ilikwishaanza kulipa madeni yake kwa TANESCO, hivyo hakuna budi Kampuni na watu binafsi wanaodaiwa na Shirika hilo kulipa madeni yao pia.

“Meneja wa TANESCO, Sheria ya Umeme inakuruhusu kuwachukulia hatua wadaiwa waliogoma kulipa madeni yao. Wapeleke Mahakamani.” Katika kuhakikisha agizo lake linapewa uzito unaostahili, Naibu Waziri aliwaagiza Mameneja wa TANESCO wa Mkoa wa Tabora kumpatia orodha ya majina ya wale wote wanaodaiwa na Shirika hilo mkoani humo ifikapo kesho Ijumaa, Februari 19 mwaka huu.

“Mnipatie orodha hiyo ifikapo Ijumaa, iwe ni kampuni ya mtu mzito au mtu mwingine yeyote,” alisisitiza. Aliongeza kuwa, ni lazima hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya waliokaidi kulipa kwani kitendo hicho ni kuihujumu TANESCO.

Naibu Waziri alisema Serikali imedhamiria kukusanya mapato yote stahiki kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo alimwambia Meneja wa TANESCO Mkoa wa Tabora kuwa asipochukua hatua kama alivyomwagiza, hatasita kumuwajibisha yeye mwenyewe.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kalemani ameagiza kuwa Makandarasi wote wanaojihusisha na shughuli za kutandaza waya na vifaa vingine kwa ajili ya kuunganisha umeme majumbani na katika majengo mbalimbali (wiring), kujisajili katika Ofisi za Wilaya za TANESCO.

Alisema, agizo hilo linafuatia kuwepo na wimbi la matapeli maarufu kama vishoka ambao hufanya kazi hiyo ya kuunganisha umeme pasipo kuwa na utaalam husika.

Aidha, aliwataka wananchi kutofautisha kazi zinazofanywa na TANESCO na zile zinazofanywa na Makandarasi binafsi katika zoezi zima la kuunganisha umeme.

Alisema, kazi ya TANESCO ni kusimika nguzo za umeme na kuunganisha Waya unaoingiza umeme katika nyumba au jengo husika lakini si kazi ya Shirika hilo kufunga Waya na Vifaa vya umeme ndani ya nyumba au jengo.

“Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika sana kwamba wanatapeliwa kwa kutozwa fedha nyingi na/au kufungiwa vifaa vya umeme visivyo na ubora kwenye nyumba zao. Mara nyingi lawama hizo huelekezwa TANESCO.”

Dkt Kalemani alisema, ndiyo maana Serikali kupitia Wizara yake, imeamua kuwa Makandarasi wote wanaojihusisha na shughuli hizo wasajiliwe katika Ofisi za TANESCO za Wilaya ili wafahamike na hivyo kuwaepushia wananchi adha ya kutapeliwa.

No comments: