Mtafiti Mkuu wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dk. Emmarold Mneney (kushoto), akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Salama kilichopo Kata ya Ng'haya baada ya kupokea changamoto zao katika mkutano uliofanyika kijijini hapo juzi.
Mtafiti Kiongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dk. Nicholaus Nyange (kulia), akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Salama kilichopo Kata ya Ng'haya kuhusu matumizi ya Bioteknolojia.
Mratibu Mkuu wa Jukwaa la Bioteknolojia Afrika, Daniel Utunge kutoka nchini Kenya (kulia), akiwa katika mafunzo hayo ya matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo yaliyofanyika kijiji cha Salama wilayani Magu. Kushoto ni Mwanahabari wa gazeti la majira jijini Mwanza.
Mtafiti Mkuu wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dk. Emmarold Mneney (kulia), akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Bugatu wilayani Magu mkoani Mwanza baada ya kupokea changamoto zao za kilimo.
Wakulima wa Kijiji cha Bugatu wilayani Magu mkoani Mwanza wakiwa kwenye mafunzo hayo baada ya kueleza changamoto zao za kilimo kwa watafiti kutoka Costech na Jukwaa la Bioteknolojia.
Mtafiti Kiongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dk. Nicholaus Nyange (kulia), akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Ng'haya kilichopo Kata ya Ng'haya kuhusu matumizi ya Bioteknolojia.
Na Dotto Mwaibale, Magu
WAKULIMA wa Kijiji cha Salama kilichopo Kata ya Ng'haya wilayani Magu mkoani Mwanza wamewatupia lawama maofisa ugani wakidai wamekuwa wakichangia kuporomosha kilimo kwa kuwa hawafiki kuwapa elimu ya kilimo.
Malalamiko hayo waliyatoa mbele ya Watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na waandishi wa habari katika ziara ya watafiti hao mkoani humo ya kujua changamoto zinazo wakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Watafiti hao wako katika ziara hiyo mkoa wa Mwanza na Mara ya kukukutana na wakulima na kutoa mafunzo ya matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo kwa kuwezeshwa na Jukwaa la Bioteknolojia ambapo walifanikiwa kukutana na wakulima wa Kijiji cha Salama, Bugatu na Ng'haya vyote vikiwa wilayani Magu huku changamoto zao zikilingana.
Mmoja wa wakulima wa kijiji hicho Kaabi Mahushi alisema changamoto kubwa waliyonayo katika kilimo ni elimu ya kilimo kwani maofisa ugani hawawafikii hivyo kujikuta wakikosa ushauri kuhusu masuala ya kilimo cha mazao yote.
"Changamoto kubwa tuliyonayo ni kutofikiwa na maofisa ugani tunaiomba serikali kutuletea maofisa hao ili tuweze kupata ushauri wao" alisema Mahushi.
Mkulima Musa Mnyalo alisema ukosefu wa pembejeo, mbegu bora na wataalamu hilo ni eneo jingine linalo warudisha nyuma katika kilimo cha mpunga, pamba, mahindi, mihogo na choroko ambayo yamekuwa yakishambuliwa na magonjwa ikiwemo batobato kwa zao la mihogo.
William Pastory alisema bei ya mbegu ya pamba kwa kilo 6 kuuziwa sh.20,000 ni ghari mno ukilinganisha kuwa bei ya zao hilo imekuwa ikishuka kila wakati kutoka sh.1200 hadi kufikia 700 kwa kilo.
Changamoto zingine zilizotajwa na wakulima hao ni pamoja na kukosekana kwa mbegu bora ya pamba, mazao yao kama mahindi, mihogo, mpunga kushindwa kustawi kutokana na kushambuliwa na wadudu, ukame, ukosefu wa mvua na madawa.
Akizungumza baada ya kupokea changamoto hizo kutoka kwa wakulima hao Mtafiti Mkuu wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dk. Emmarold Mneney alisema Serikali inajua hicho kiliochao na ndio maana imetenga fedha zinazo wasaidia watafiti kufanya utafiti wao utakaotoa majibu ya kuwakomboa wakulima.
"Hivi sasa tupo katika tafiti za mbegu ya mahindi na pamba wakati wowote tutapata majibu yatakayosaidia kupata mbegu bora kwani tafiti zinafanyika katika maabara ya ndani na zikitoa matokeo mazuri tutazalisha mbegu hizo kwa wingi na kuwasambazia wakulima" alisema Dk.Mneney.
Mtafiti Kiongozi wa Costech Dk.Nicholaus Nyange alisema licha ya Tanzania kuwa na changamoto ya mbegu za pamba nchi kadhaa kama, Afrika Kusini, India, Bakinafaso na Sudani zimefanikiwa katika kilimo hicho baada ya kutumia Bioteknolojia ya uzalisha mbegu ambayo inafanyiwa kazi na watafiti hapa nchini ili iweze kutumika.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)
No comments:
Post a Comment