ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 5, 2016

Lowassa afichua alichoteta na Waziri Mkuu Majaliwa

Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ametoboa siri juu ya alichozungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, walipokutana mjini Moshi.

Lowassa alieleza kuwa Waziri Mkuu Majaliwa amewapa ruhusa Chadema kuzunguka nchi nzima na kufanya mikutano kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kuwapigia kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Lowassa akiwa katika ibada maalum ya kumwingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fedrick Shoo, Jumapili iliyopita, alikutana na Majaliwa na kusalimiana.

Lakini katika mazungumzo yao, haikufahamika mara moja walizungumza nini viongozi hao.

Akizungumza na viongozi wa Baraza la Wazee wa Jimbo la Ubungo waliofika ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kumshukuru kwa kazi aliyoifanya wakati wa uchaguzi mkuu, Lowassa alisema Waziri Mkuu Majaliwa amewaruhusu kufanya mikutano nchi nzima.

Alisema Chadema kinatarajia kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wananchi kwa kuwapigia kura na kuwachagua wabunge na madiwani wa Chadema kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Alisema upangaji wa ratiba hiyo utaanza litakapomalizika Bunge.

“Chama kinatarajia kufanya mikutano nchi nzima kuwashukurru wananchi kwa kazi nzuri ya kuwapa kura nyingi, tena nilipokutana na Waziri Mkuu Moshi alinipa kibali hicho,” alisema Lowassa.

Lowassa alisema kabla ya kuanza kazi hiyo, Kamati Kuu ya Chama itafanya kikao cha kujadili uchaguzi mkuu uliopita kwa kuangalia wapi walikosea na kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kuhusu Chadema kutofanya fujo baada ya matokeo ya uchaguzi, Lowassa alisema aliona amani ni kitu cha muhimu kuliko kuingia Ikulu, hivyo aliwashawishi wananchama kutofanya fujo.

Alisema dunia nzima hata CCM inafahamu kuwa Chadema ilishinda uchaguzi huo lakini matokeo yalichakachuliwa, akitolea mfano Jimbo la Tunduma mkoani Mbeya alipofanya mkutano uliofurika watu wengi lakini wakati wa matokeo ilielezwa kuwa alipata kura 3,000.

Alisema Chadema kwa sasa ina mikakati ya kuongoza nchi katika uchaguzi ujao, mojawapo ikiwa kuwatumia wazee wa vijiji kukiimarisha chama katika ngazi ya matawi.

KATIBA MPYA
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Lowassa alisema anataka kuwapo mjadala mkubwa bungeni wakati wa mchakato wa kuipitisha.
Alisema moja ya vipengelea vinavyohitajika kubadilishwa ni upatikanaji wa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na kusema inahitajika kuwa huru.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi haifai. Ilipaswa kufukuzwa mara baada ya uchaguzi kumalizika kwa kuwa iliipendelea CCM. Dunia nzima hata wenyewe CCM wanajua kuwa nilishinda uchaguzi,” alisems Lowassa.

Alisema kipengele cha wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kinapaswa kubadilishwa nacho kwa kuwa wanakuwa na mamlaka makubwa, mojawapo ni kuwapa amri wakurugenzi wa halmashauri kuchakachua matokeo na kumpitisha mgombea anayetakiwa na CCM

“Wakuu wa wilaya na mikoa ni watu wabaya sana. Wanaisaidia CCM wakijua kuwa wasipofanya hivyo ugali wao utamwagika, wanafaa kuondolewa kabisa,” alisema Lowassa.

Alisema Watanzania wanapaswa kuhamishia machungu waliyoyapata wakati wa uchaguzi mkuu kwenye katiba mpya, kwa kutoikubali NEC ambayo haitakuwa huru

Hata hivyo, Lowassa alionyesha wasiwasi wa upatikanaji wa katiba hiyo, na kueleza kuwa endapo katiba hiyo itapelekwa bungeni na kupigiwa kura, kuna uwezekano mkubwa ikapita kwa sababu ya kuwapo kwa uwingi wa wabunge wa CCM.

Mwenyekiti wa wazee Chadema Jimbo la Ubungo, Enock Ngombale, akizungumza kwa niaba ya wazee hao, alisema wanampongeza Lowassa kwa uamuzi wa kuihama CCM, kufanya kampeni kwa ustaarabu, kugombea urais, na kuleta ushindi mkubwa wa kura za urais, wabunge na madiwani.

SUALA LA ZANZIBAR
Lowassa alisema mgogoro ulioko Zanzibar usiposhughulikiwa kwa umakini na umahiri, utaleta matatizo makubwa kwa taifa zima.
Alisema endapo uchaguzi utarudiwa na CUF kutokushiriki, kunaweza kuleta madhara makubwa visiwani humo kwa sababu Wazanzibari hawatakubali kuongozwa na rais ambaye hawajamchagua.

Alisema CCM ndio walioanzisha mfumo wa kupokezana madaraka kila baada ya miaka mitano, lakini anashangaa kwa kipindi hiki kumetokea mgogoro.

Alisema CUF na CCM wanapaswa kurudi katika meza ya majadiliano, alisema haoni sababu ya watanzania kudhurika wakati mgogoro unaweza kumalizwa kwa majadiliano.

“Naogopa sana nchi kuingia katika machafuko wakati viongozi wanaweza kuzungumza na kumaliza, tusiwaruhusu Al-qaeda wakaingia nchini,” alisema Lowassa.

Alisema maslahi ya vyeo yanapaswa kuwekwa pembeni na kuwasaidia Wazanzibar ambao kwa sasa wanaishi kwa woga na wasiwasi, na kueleza kuwa kurudiwa kwa uchaguzi si njia ya kutatua mgogoro huo.
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

So what? Lowassa, wake up! Wanakupa morale tuu ili ujisikie vizuri (superficial). Usichanganye uwingi wa watu wanaohudhuria mikutano yenu na wapigaji kura. Ku-entertain underage teenagers kujaza stadiums siyo sawa na kuwa na idadi kubwa ya Wafuasi watakaopiga kura. Mliwanunua vijana wadogo kujaza viwanja, lakini hamkuweza kuwanunua wapiga kura kwa sababu, Watu wazima (adults) na Wazee (elders) wengi wanajua Ukawa/Chadema ni Chama FEKI.

Anonymous said...

Go away!

Anonymous said...

Mtoa mada asante. Inaelekea umetoa maelezo yako.kwa aina ya uchukinwa namna yake. Ila kinachoelezwa na mheshimiwa Lowasa ni ukweli ambao unaeleweka alilofanya nikuweka bayana hali halisi na bado tunayo huko Zanzibar na maandalizi yasokuwa haki kama ilivyokuwa Bara ndio yaleyale chama kishapanga kutoa matokeo waliyoyaandaa na wala sio yatokanayo na uchaguzi unaolengwa. Mh. Rais JPM anayofanya yanaridhisha lakini swala la Katiba na Zanzibar sio ya mchezo kukaliwa na kulazimishwa nchi itakuwa kwenye mfumo usioendelevu. Ninapita tu.