ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 23, 2016

Rubani ‘aliyemdhalilisha’ polisi Kenya afutwa


Rubani wa ndege anayedaiwa kumdhalilisha afisa wa polisi wa kike nchini Kenya amefutwa kazi.

Rubani huyo, ambaye ni raia wa Uingereza, alikuwa na ndege aina ya helikopta nambari 5Y-DSN iliyokuwa imembeba Naibu Rais William Ruto wakati wa ziara yake mji wa Ndunyu Njeru, jimbo la Nyandarua katikati mwa nchi hiyo Jumapili.

Kampuni ya Kwae Island Development (KIDL) ambayo humiliki helikopta hiyo imesema kisa hicho ni cha kusikitisha.

“KIDL imefahamu kutoka kwa mitandao ya kijamii na vyanzo vingine vya habari kwamba Alistair Llewelyn alihusika katika kisa tarehe 20 februari 2016. KIDL inasikitishwa sana na kisa hiki na inajitenga kabisa na vitendo vya Alistair Llewelyn,” taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Marco Brighetti, mmiliki wa kampuni hiyo inasema.

“KIDL inaheshimu maafisa wapolisi wa kiume na kike wa Kenya na inalaani kabisa vitendo vya Alistair Llewelyn.”
Rubani adaiwa kumdhalilisha polisi wa kike Kenya

Bw Llewelyn amejisalimisha kwa polisi katika kituo cha Kilimani. Msemaji wa polisi George Kinoti amesema mshukiwa huyo anatarajiwa kufikishwa kortini Jumatano.

Video iliyochukuliwa na mmoja wa walioshuhudia kisa hicho cha Jumapili imesambaa sana mtandaoni watu wakitaka hatua zichukuliwe dhidi ya rubani huyo.

Kwenye video hiyo, rubani huyo anaonekana akimkaripia mwanamke huyo ambaye wakati huo anatumia simu, kumpokonya fimbo yake na kisha majibizano yanatokea. Muda mfupi baadaye, rubani huyo anaonekana akimsukuma afisa huyo wa polisi.

Afisa wa mawasiliano wa Bw Ruto, Bw David Mugonyi, amesema kiongozi huyo amefahamishwa kuhusu kisa hicho.

“Naibu Rais amewaagiza polisi kuchukua hatua mara moja. Naibu Rais anaheshimu polisi wetu wenye bidii ambao hufanya kazi saa nyingi kulinda nchi. Kisa hiki hakikubaliki, na ni cha kusikitisha na nimewataka polisi kuchunguza kitendo hicho cha rubani huyo,” taarifa yake imesema.

BBC

No comments: