Dar es Salaam. Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF) umesema upo tayari kulipa fedha ili Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC) lirushe vipindi vya moja kwa moja vya Bunge.
Akizungumza jijini jana, Mkurugenzi Mkuu wa TMF, Ernest Sungura alisema iwapo tatizo kubwa ni fedha kama inavyoelezwa, basi shirika hilo lipo tayari kuisaidia Serikali ili wananchi wapate taarifa za ndani ya Bunge.
“Tupo tayari kuisaidia Serikali katika hili kwa sababu tumeona ni busara wananchi wakapata taarifa muhimu na zenye tija, kutoka katika chombo hicho muhimu cha kutunga sheria,” alisema.
Alisema TMF imefanya mkutano na wamiliki wa vyombo vya habari, mameneja na wahariri kwa ajili ya kutambulisha mfumo mpya wa kutoa fungu kwa taasisi lakini pia kwa waandishi na vyombo vya habari.
Sungura alifafanua azma ya mpango huo baada ya kupokea maombi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene aliyeitaka TMF kuangalia uwezekano wa wadau kuchangia katika maendeleo ya sheria mpya za vyombo vya habari.
Katika mkutano huo, Mwambene alisema kwa sheria hiyo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya vyombo vya habari nchini, hivyo itakuwa vyema kama TMF itawasaidia wadau kushiriki katika kutunga sheria hizo.
“Kwa sababu TMF inajihusisha na masuala ya kuvisaidia vyombo vya habari, tunaamini kuwa inaweza pia kusaidia katika kuwahimiza wadau na kushiriki kutunga sheria za vyombo vya habari,” alisema Mwambene aliyemwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Alirudia ahadi ya Nape kwa wadau wa vyombo vya habari kuwa, Serikali haiwezi kupitisha muswada wa habari ambao haujakubaliwa na wadau wote.
“Niwaambie tu kuwa tumeelekeza nguvu katika kuhakikisha kuwa tuna sheria ambazo zimekubaliwa na wadau wote kwa sababu wanachangia maendeleo ya sekta ya habari,” alisema.
Hivi karibuni, Serikali ilikosolewa vikali baada ya kusimamisha urushaji wa vipindi vya moja kwa moja vya Bunge na Nape alitoa ufafanuzi kuwa TBC ilichukua uamuzi huo kutokana na vikwazo vya kiuchumi akisema inahitaji kiasi cha Sh4.2 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kugharimia vipindi hivyo.
Hata hivyo, wabunge wa upinzani na wanaharakati wengine waliuchukulia uamuzi huo wa Serikali kama mbinu ya kuwazuia wananchi kuona uozo na udhaifu ndani ya Bunge hilo.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, George Mziray alisema hana taarifa za TMF kutaka kugharimia vipindi vya Bunge.
“Hizo taarifa ndiyo kwanza nazisikia kutoka kwako, siwezi kuzungumza chochote mpaka nizihakiki maana hazijafika kwangu,” alisema.
2 comments:
Tafadhali, tutafurahi na kushukuru kuona TMF inatumia hizo pesa kuwasaidia wananchi kiuchumi. TMF should set priorities and direct funding to causes which matters most.
TMF watumie pesa hizo kuboresha studio na mitambo ya TBC. Zinatia aibu
Post a Comment