Advertisements

Thursday, February 11, 2016

Ulaya wamgomea Magufuli.

Umoja wa Ulaya (EU), umemgomea Rais Dk. John Magufuli, kwa kueleza kuwa msimamo wake ni uliotolewa na washirika wa jumuiya ya kimataifa wa kumtaka kushirikiana na vyama vilivyoshiriki uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar kufikia muafaka.

Akijibu swali la Nipashe kutaka kujua walivyopokea ombi la Rais kwa jumuiya za kimataifa kuzungumza na CUF, ili wakubali kushiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, Msemaji wa EU, Balozi Roeland van de Geer, alisema wanasubiri kuona utekelezaji wa tamko lao.

"Msimamo wa washirika kadhaa wa jumuiya ya kimataifa nchini, Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wakizungumzia kuhusu uchaguzi wa marudio kufanyika, umeelezewa bayana kwenye tamko lilitolewa Januari 29, mwaka huu," alisema Balozi Roeland na kuongeza:

"Mpaka sasa EU hatuna la kuongeza zaidi ya tamko hilo linaloelezea msimamo wetu kwa ukamili. Hata hivyo, kwa sasa tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo yake na tunatumaini maendeleo hayo yataleta habari njema kwa wote visiwani humo."

Januari 29, mwaka huu, EU jumuiya ya kimataifa inayojumuisha nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi, Marekani na Uingereza zenye ubalozi nchini, zilitoa tamko la pamoja la kumtaka Rais kuingilia katika mgogoro huo.

“Tunamtaka Rais Magufuli kuonyesha uongozi wake kupitia mgogoro huu wa kisiasa kwa kuingilia kati na kutafuta usuluhishi baina ya vyama vikuu kuhakikisha amani pande zote," ilisema sehemu ya tamko hilo.

Tamko hilo pia lilieleza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa na kasoro zilizoelezwa na kwamba waangalizi wa kutoka Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki, EU, Marekani na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliridhika na mwenendo wa uchaguzi huo.

Walisema wakati mazungumzo baina ya CUF na CCM yakiendelea, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alitangaza uchaguzi wa marudio.

Tamko hilo lilisisitiza kurejewa kwa mazunguzo ya vyama vinavyovutana na kuwa na maridhiano kuliko kurudi kwenye uchaguzi mpya.
Walisema kurudiwa kwa uchaguzi huo kutaongeza hali ya wasiwasi na sitofahamu visiwani humo, hivyo ni vyema pande zote (CUF na CCM) zikakutana na kuwa na makubaliano ya pamoja na ya amani.

"Ili uwe uchaguzi huru na haki ni lazima pande zote zishiriki. Kwa hali iliyopo kwa sasa itakuwa vigumu kwa waangalizi wa kimataifa kushiriki uchaguzi wa marudio," lilifafanua tamko hilo.

Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana, waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) walitoa wito kwa ukamilishwaji wa haraka wa mchakato wa uchaguzi Zanzibar kulingana na kanuni za uchaguzi shirikishi, za uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na kuaminika.

Mwangalizi Mkuu wa EU EOM, Judith Satgentini, alisema: “EU EOM iko tayari kurejea nchini kuangalia mchakato wa uchaguzi Zanzibar pindi makubaliano ya kuendelea yatakapofikiwa."

Jecha alitoa tamko la kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 25, mwaka jana, baada ya kueleza kasoro tisa zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo.

Kumekuwa na mvutano baina ya chama tawala (CCM) na chama kikuu cha upinzani visiwani humo (CUF). Katika mvutano huo, CUF inataka kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, ambao mgombea urais wake, Maalim Seif Sharif Hamad, alijitangaza mshindi kwa kupata kura 200,007 dhidi ya 178,363 alizopata mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein.

Hivi karibuni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, alisema: “Baadhi ya watu, mashirika, EU, Marekani, Jumuiya ya Madola na wote walioona kwamba tume haikutenda haki (Zec kufuta matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar)… kwamba ingemaliza kuhesabu na matangazo yatoke. Lakini tume iliona kabisa kwamba ikifanya hivyo itakuwa imekiuka maadili yake,“ alisema.

“Kwa hiyo kukawa na mvutano. Kwamba kwa upande wa vyama, walivyopewa maamuzi haya ya tume, wakakaa kuona wafanye nini. Na tukadhani katika hivi vyama kuzungumza kule, na sisi bara watatukaribisha, au Serikali ya Muungano watatukaribisha. Lakini wakasema hata, hili mtuachie sisi wenyewe tutalizungumza kuhusu huu uamuzi wa tume,” alisema Balozi Mahiga.

“Wengine wakasema hata misaada tunasimamisha, kama vile Marekani (Fedha za MCC)… tunasimamisha kwa sababu sisi tunaona haya mazungumzo hayatoi majibu na afadhali tu yatangazwe (matokeo ya uchaguzi) kama yalivyokuwa, lakini katika hilo baadaye tume ikasema jamani, afadhali tuite uchaguzi mwingine.

Akijibu baadhi ya hoja za wabunge zilizotolewa wakati wa mjadala wa Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa 2016/17 Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema Rais Magufuli hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia masuala ya Zanzibar.

“Kile ambacho baadhi ya wabunge wamekisema hapa ni kama kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia mamlaka ya Zanzibar na tafsiri yake ni kama unataka kuleta hoja ya kujenga serikali moja,” alisema Masaju.

“Hoja kwamba Rais Magufuli aingilie haiwezekani. Mambo ya ulinzi na usalama ndio ya muungano na hicho ndicho kinafanyika Zanzibar kuhakikisha amani na usalama," alisema.

CHANZO: NIPASHE

9 comments:

Anonymous said...

Hivi EU wakisema wanasubiri Magufuli kutekeleza madai yao, wanadhani Tanzania ni koloni lao? Wakati mbali. Serikali yetu sharti iwe na ubavu wa kuwakemea. Wasitufananishe na Burundi. Hata kwa Rwanda hawa wazungu wanashika adabu yao. Mahiga asiache tukadhalilishwa. Wasimuachie Magufuli kila kitu. Washikishwe adabu.

Wazungu hawa wanapenda kueleza kuheshimu utawala wa Sheria. Zanzibar wana katiba yao.Inapaswa kuheshimiwa na kutambuliwa. Huo ndio utawala bora. Wasisikizwe hao. Hawana muelekeo. Leo wanalia Wakimbizi kutoka Syria. Sisi miaka yote tunawakimbizi kutoka Burundi. Huwasikii hata siku moja. Leo yamewafika wanataka dunia yote ilie.

Waongo hao. Tuwapuuze tu. Tufanye haki tukijiridhisha kwamba tunafanyana haki ya wazi na kweli; sio lazima iwe atakavyo mzungu.

Anonymous said...

Kwa Zanzibar ccm mmelikologa ! Huku bara sawa mmepatia lakini kwa Zanzibar mtatia akili ! Tuombe uzima ili tushuhudie yatakayo tokea !

Anonymous said...

I couldn't agree more. EU should leave us alone. They should not poke their long noses in Zanzibar. Magufuli should tell them to ..... off!!

Anonymous said...

Ni umasikini wetu ndio unaotufanya kuwatetemekea hawa sijui nchi wafadhili/wahisani.Lakini ukiangalia kiasi cha misaada na mchamgo wao ktk bajeti yetu si mkubwa kiasi cha kuruhusu waanze kutupangia nini cha kufanya katika mambo yetu ya ndani.
Na imefikia hatua hata viongozi wetu linapotokea tatizo ktk mambo yetu ya ndani hukimbilia kwanza nje kuliax2 kabla ya kuanza kutafuta solutions kwa kutumia mechanism za kwetu.

Anonymous said...

Na sio kila kitu eti mzungu kasema. Ni binadam kama sisi.Na sisi tutumie upeo wetu na kutambua matatizo yetu na kuzikabili changamoto zetu, sio kila wakati watu furani ndio wako perfect amna binadamu parfect inakuwa ni kumtukuza na kumuona bora kushinda huyu, kila binadam awe mzungu, mweusi,blu wote wanamapungufu

Anonymous said...

Mdau hapo juu unajikanyaga sana zanzibar kuna ccm na ccm hiyo na hii ya bara ni hiyo hiyo moja wizi unao fanyika hivi sasa huko zanzibar wa kurudia uchaguzi ni mpango wa CCM kama chama sasa Haki unayoipigania iko wapi hapo? tuachane na wazungu tusijaribu kuwa laumu wao wakati sisi waswahili ndio tuna matatizo wancho kieleza wao ni kutufahamisha tatizo liko wapi hata angelikuwa mchina anajua kutenda haki tatizo hili angeliona lakini kwa kuwa na yeye hajui haki ni nini ndio maana kakaa kimya.

usijikite kwenye wazungu wakati tatizo ni waswahili tafadhali.

mdau.
uswahilini.

Anonymous said...

Kama hamtaki masharti ya wazungu. Mbona mbakwenda kuwaomba misaada asubuhi na mchana. Ndio wawajengee baraba zenu, vivuko ndio vimekwama. Aaaahh! Waafrika bado mnawahitaji wazungu either you guys like or not...ngoja wawasimamishie misaada muone kama mtaweza hizo nchi zenu...aaahaaa!

Anonymous said...

T. tunajua ni wewe umetoa komenti hii.

Anonymous said...

Wazungu my nose...Hii ni mentality ya kitumwa.Tanzania ni sovereign country,hatupaswi kuingiliwa katika namna tunavyoendesha mambo yetu ya ndani,masharti yeo yaishie katika misaada wanayotoa na si vinginevyo.Hii haiingii akilini hata katika personal level, ni vipi ukapokea msaada kutoka kwa mtu au financial institution then waanze kukupangia jinsi unavyopaswa kulea familia yako?