Jumla ya fedha hizo kwa Wabunge wote zitaigharimu serikali Sh. bilioni 34.38.
Hata hivyo, Nipashe imebaini kuwa hadi kufikia jana mchana, wabunge waliokuwa tayari wameshaingiziwa fedha hizo kwenye akaunti zao ni 160 tu huku wengine waliobaki wakitarajiwa kupata fedha hizo kati ya kesho na keshokutwa.
Kuanza kutolewa kwa mkopo huo kwa wabunge, ambao marejesho yake yanatarajiwa kufanyika ndani ya kipindi chao cha miaka mitano kwa kukatwa kwenye stahili zao, kunahitimisha mjadala uliodumu kwa siku kadhaa kuhusiana na kiwango watakacholipwa.
Baadhi ya wabunge walitaka wapewe walau Sh. milioni 130 kila mmoja kutokana na bei ya magari kupanda kulinganisha na mwaka 2010 wakati walipokopeshwa fedha za kiwango hicho pia, kwa ajili ya ununuzi wa magari binafsi ya kufanyia kazi.
Chanzo kimoja cha uhakika kutoka ofisi ya Bunge kiliiambia Nipashe kuwa ombi la kutaka wabunge wakopeshwe Sh. milioni 130 kila mmoja limekataliwa na hivyo watakopeshwa kwa kiwango sawa na kile kilichotolewa wakati wa kuanza kwa Bunge la 10.
Kati ya Sh. milioni 90 hizo, nusu yake ni ruzuku ya serikali na Wabunge watatakiwa kulipa Sh. milioni 45 tu.
“Hizo fedha walizokuwa wanazitaka hazijapatikana na ndio maana wameanza kuingiziwa Sh. milioni 90 kila mmoja.
Wapo watakaolalamikia kiwango hiki, lakini hiyo ndio hali halisi,” chanzo cha uhakika hapa Dodoma kiliiambia Nipashe.
Kama ombi la wabunge kutaka walipewe kila mmoja Sh. milioni 130 kwa ajili ya kununulia magari lingekubaliwa, serikali ingelazimika kutumia Sh. bilioni 49.66 ili kufanikisha mkopo huo kwa wabunge wote 382.
Kiasi hicho kinatosha kujenga barabara ya lami ya umbali wa kilomita 50, kwa makadirio ya kilomita moja kujengwa kwa Sh. bilioni moja.
Msemaji wa Bunge, Owen Mwandumbya hakupatikana jana ili kuzungumzia tarifa hizo.
WASEMAVYO WABUNGE
Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na taarifa za kuanza kutolewa kwa mkopo wa magari, Mbunge wa Donge, Juma Sadifa, alikiri kuwa ni kweli kwani yeye amekuta benki ameingiziwa Sh. milioni 89 kati ya Sh. milioni 90.
Kiasi kilichopungua kimekatwa kwa ajili ya gharama za bima, alisema.
Alisema kuwa anaamini fedha hizo ni ndogo kwake kwani hazitoshi kununulia gari alilopanga ambalo huuzwa Sh. milioni 200.
"Mimi nataka kununua V9 ambayo inauzwa Sh. milioni 200… wangenipatia hizo milioni 130 zingenisaidia kuongezea ili kununua gari hiyo," alisema Sadifa.
Mbunge wa Shaurimoyo, Mattar Ali Salim, alisema kuwa hadi kufikia jana mchana, yeye alikuwa bado hajawekewa fedha hizo na kwamba, amejulishwa kuwa kundi la awali kwa waliopewa fedha hizo ni wabunge 160.
Salim alisema amejulishwa kuwa mkopo kwa wabunge waliosalia utakamilishwa kufikia Jumanne ambapo wabunge wote watakuwa wameshaingiziwa fedha hizo.
Akieleza zaidi, Salim alisema kiasi cha fedha walichokopeshwa kununua magari ni kidogo na hakitoshelezi mahitaji.
"Mimi nataka kununua Land Cruiser, ile aina ya Mkonge … sasa utaona hizo milioni 90 hazitoshi hata kidogo," alisema Salim.
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, John Heche, alisema yeye bado hajapatiwa fedha hizo lakini amejulishwa kuwa kufikia Jumanne atakuwa ameshaingiziwa benki na hivyo, hawezi kusema zinatosha au hazitoshi wakati bado hajajua ataingiziwa kiasi gani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
1 comment:
really ...kwa nini wasiende kuomba mkopo bank kama watu weingine...ni wizi tu...kila mtu anunue gari kwa mkopop wake bila kuingiza serikali kati. Kwani hizo hela wanazoprea zingefanya mengi tu kama kupata dawa kwa watoto , elimu na vitu vingi tu. Badala yake wanapewa wabunge eti watalipa baada ya 5 yrs....basi waende bank waombe mkopo kwa majina yao na siyo pesa ya serikali.
Post a Comment