ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 5, 2016

WAGANGA WANAOCHOCHEA MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI KUSHUGHULIKIWA

Naibu  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Hamad Yussuf Massauni akijibu hoja mbalimbali kuoka kwa Wabunge mbalimbali katika kikao cha 9 cha Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma. Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekua ikifanya operesheni maalum za mara kwa mara za kukamata waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi ambazo ni kichocheo kikubwa cha ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi nchini.

Akijibu swali la Mhe.Mgeni Jadi Kadika Mbunge wa Viti Maaalum(CUF) lililouliza Serikali ina mpango gani wa kuwalinda na kuhakikisha usalama wa maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Hamad Yussuf Massauni amesema Serikali imeanzisha vituo vya kuwahudumia watu wenye ulemavu wa ngozi ambavyo vimesaidia kuimarisha ulinzi ikiwa ni pamoja na Polisi kuwatumia Polisi Jamii kutoa elimu kwa umma  juu ya madhara ya vitendo vya kikatili vya mauaji na kujeruhi vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa msukumo wa imani potofu za ushirikina.

“Kwa takwimu halisi tulizonazo tangu mwaka 2006 mpaka 2015 jumla ya mauaji ya walemavu wa ngozi 43 yametokea na jumla ya watuhumiwa 133 walikamatwa kuhusika na vitendo hivyo na watuhumiwa  19 walihukumiwa adhabu ya kifo”


“ Katika kupambana na vitendo hivi Jeshi la Polisi linakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa askari katika kuhudumia wananchi ambapo kwa Tanzania askari mmoja anahudumia wananchi 1000 mpka 1500 ikiwa ni nje ya matakwa ya kimataifa ya askari mmoja kuhudumia wananchi 400 mpka 450 na uhaba wa magari kwa ajili ya doria mbalimbali ambapo takribani magari 387 yamegawanywa katika maeneo mbalimbali nchini ili bado tunaendelea kupambana na kutatua changamoto hizi kadri ya bajeti iyakavyoruhusu” Alisema Mhe.Massauni.

Wizara kupitia Jeshi la Polisi ikishirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Vijiji,Kata,Wilaya, na Mikoa imeanzisha vikosikazi(TASK FORCES) hususani kwenye Mikoa na Wilaya zilizokithiri matukio ya  ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi ambapo Vikosikazi hivyo hukusanya taarifa za kiintelejensia na kuzifanyia kazi.

No comments: