Rais John Magufuli jana aliibuka ghafla na kushiriki ibada ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Azania Front, Dar es Salaam na kuwaduwaza waumini na viongozi wa kanisa hilo.
Miongoni mwa walioshangaa ujio huo ni Askofu wa Kanisa hilo, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliyekiri kuwa alipoelezwa kwamba Rais anakwenda kanisani hapo aliwabishia wasaidizi wake.
Hata waumini wa kanisa hilo walisema ujio wa Rais Magufuli kanisani hapo umewafariji licha ya kuwa hawakujua wala kuwa na tetesi, tofauti na mazoea yao kwa baadhi ya viongozi.
Elikunda Ngowi alisema ikiwa viongozi wa juu watajishusha kama alivyofanya Dk Magufuli, itakuwa rahisi kupata mawazo ya wananchi wa kawaida yatakayosaidia katika uongozi.
“Hakuna aliyejua kama tutakuwa na Rais hapa kanisani, tumejua asubuhi hii tulipoona ulinzi mzito. Huu ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine ambao wanatakiwa kujishusha,” alisema.
Muumini mwingine, Bariki Edward alisema wataendelea kumuombea kiongozi huyo ili Mungu ampe nguvu ya kuendelea kushughulikia kero zinazowakabili.
Magufuli anena
Alipopewa nafasi ya kuwasalimia waumini wa kanisa hilo, Rais Magufuli aliitumia kumwomba radhi Dk Malasusa kwa kutokutoa taarifa ya ujio wake kwenye ibada hiyo, akifafanua kuwa anaamini yeye ni muumini wa kawaida.
“Ni kweli sikukuomba ruhusa ya kuja hapa, naomba unisamehe sana, nilisema nataka Pasaka hii nisali Azania Front, sasa wasaidizi wangu waliniambia lazima wakueleze wewe Baba Askofu, nikawaambia wasikueleze kwa sababu niliamini sipo tofauti na nyinyi, mimi ni Mkristo wa kawaida,” alisema Dk Magufuli ambaye ni Mkatoliki.
Awali, Askofu Malasusa alisema Tanzania ina bahati kuwa na Rais anayemtegemea Mungu kwenye uongozi wake.
Dk Malasusa ambaye ni mkuu mstaafu wa kanisa hilo Tanzania, alisema alipoambiwa Rais Magufuli atahudhuria ibada kwenye kanisa hilo, alibisha akidhani waliomweleza wamekosea.
“Nilidhani taarifa zile zimekosewa, hivyo nikawabishia waliokuwa wananiambia, hakika hii ni bahati kwetu na wakati mwingine uendelee kuja hata bila taarifa kwa sababu Ikulu iko karibu na kanisa. Tunakukaribisha Rais uje kama ulivyokuja leo, kwa sababu kuwa na kiongozi anayependa ibada, ni jambo jema,” alisema.
Alisema ni hatari kwa Taifa lolote kuongozwa na mtu asiyehudhuria ibada wala kuwa na hofu ya Mungu kwenye uongozi wake.
Hata hivyo, Dk Malasusa alisema Rais Magufuli na viongozi wengine wanaweza kufanikiwa kwenye kazi zao ikiwa Watanzania watawasaidia kuwafichua wala rushwa bila hofu.
“Mimi nikiwabaini wala rushwa nitakwenda kusema. Nawaomba tusaidiane kuwafichua waovu bila woga kwa sababu miaka nenda miaka rudi tumekuwa tukilalamikia mambo haya,” alisema.
Ujumbe wa Rais
Dk Magufuli ambaye katika ibada ya Ijumaa Kuu alisali kwenye Kanisa alilolizoea la Mtakatifu Petro, alisema Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi tajiri zinazotegemewa katika kutoa misaada kwenye nchi nyingine, ikiwa wananchi wake watafanya kazi kwa bidii.
Alisema Watanzania wanapaswa kuitafakari sikukuu ya Pasaka kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake mahali alipo.
“Tukiamua kufanya kazi Tanzania haitakuwa maskini wala kuendelea kubembeleza misaada yenye masharti tunayopewa, Tanzania ni nchi yenye neema na inaweza kuwa miongoni mwa nchi zinazotoa misaada kwa nchi nyingine,” alisema.
Aliwasihi Watanzania kuwa wamoja na kutobaguana kidini, kikabila wala vyama ili kuifikia Tanzania yenye neema anayoamini inawezekana.
Alisema umoja na upendo miongoni mwao ndiyo utakaoifanya nchi iweze kufanikiwa kimaendeleo.
Aliwaomba Watanzania kutochoka kumwombea na kuliombea Taifa akisema jukumu lililo mbele yake ni zito.
“Ninaomba mwendelee kuniombea kwa sababu jukumu hili ni gumu, zito na msalaba. Naamini kwa maombi yenu nitatimiza wajibu wangu kwa ajili ya Watanzania na Mungu,” alisema.
Ukatili wa wanawake
Katika ibada hiyo mjini Dodoma, Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Beatus Kinyaiya alimwomba Rais Magufuli kushughulikia tatizo la unyanyasaji na ukatili kwa wanawake ambalo alisema linazidi kukua nchini.
Akihubiri katika ibada iliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Askofu Kinyaiya alisema baadhi ya wanawake wanalazimika kuzilea familia peke yao kwa sababu ya wanaume ni walevi.
“Bado kuna wanaume wenye tabia mbaya ya kutesa wake zao kwa kuwapiga. Kumpiga mke siyo lazima utumie mkono au chochote, bali wanapigwa kwa kurundikiwa majukumu ya familia,” alisema.
Aliwataka waumini kukumbuka kuwa wanawake ni kama watu wengine na hata Yesu Kristo alilielewa hilo, kuwa hawapaswi kudharauliwa wala kunyanyasika.
Alisema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika familia na wamekuwa wakijibidisha kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji.
“Wengine huanzisha miradi midogomidogo kama ufugaji wa kuku, mbuzi kupika vitumbua, chapati ili kujipatia fedha za kuendesha nyumba zao lakini michango hiyo haithaminiwi,” alisema Askofu Kinyaiya.
Elimu bure isiwapofushe
Katika hatua nyingine, Askofu Evarist Chengula Jimbo Katoliki la Mbeya amewataka wazazi wasibweteke na sera ya Serikali kuhusu elimu bure, kiasi cha kuwaacha watoto wao wakiteseka kwenye shule zenye changamoto nyingi.
Alitoa kauli hiyo katika mahubiri yake ya Pasaka kwenye Kanisa la Bikira Maria wa Fatma, Mwanjelwa.
Alisema pamoja na nia nzuri ya Serikali kuwaondolea mizigo wazazi, Watanzania hawana budi kuamua kuboresha elimu kwa kuhakikisha wanajenga madarasa na kununua madawati badala ya kuwaacha watoto wakirundikana kama vifaranga na kuketi chini au juu ya mawe.
‘’Hali hiyo haisaidii watoto na Taifa, bali inawadhalilisha watoto na kusababisha kero kubwa kwao, wazazi hawana budi kusaidiana na Serikali kwa udi na uvumba katika kuboresha hali hii,” alisema.
Pia, alizungumzia umuhimu wa Serikali kuchukua hatua kali kwa watu wanaotoa mimba akisema hao ni wauaji wa binadamu na ni wabaya kuliko majangili wanaoua wanyamapori.
“Enyi mnaotoa mimba, kama mnafanya hivyo kwa kuogopa gharama za kuwalea watoto, basi waleteni makanisani watalelewa au wafikisheni kwenye vyombo vya Serikali hasa ustawi wa jamii,” alisema.
Kuhusu watu wanaotumbuliwa majipu serikalini, alisema wanatakiwa kwenda kwenye nyumba za ibada kutubu makosa yao ili waweze kusamehewa hata kwa Mungu.
‘‘Tupo katika kipindi cha kurekebishana tabia na maadili ambacho sasa kinajulikana kwa jina la kutumbua majipu, kuwashughulikia wezi, wabadhirifu na wafujaji wa mali za umma, hivyo tuwavumilie wanaoguswa,” alisema.
Ammwagia sifa JPM
Katika ibada hiyo, Askofu KKKT, Dayosisi ya Morogoro, Jacob ole Mameo alimpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake aliosema umejaa hofu ya Mungu.
Alisema kanisa linamwombea dua ili aweze kuendelea kuwatumikia wananchi.
Askofu Mameo alitoa pongezi hizo jana wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Bungo akisema tangu alipochaguliwa, Rais Magufuli ameweka misingi bora ya kuondoa tabaka la walionacho na wasionacho.
“Ahakikishe mapato ya nchi yanakusanywa na kuingizwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote,” alisema.
Akitoa salamu za Pasaka, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Muhingo Rweyemamu alisema bado ipo migogoro mingi ya wakulima na wafugaji inayofanya mkoa ushindwe kuwa katika hali ya utulivu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, Rweyemamu alisema migogoro hiyo imekuwa kero kwa Rais Magufuli, hivyo Serikali ya mkoa itahakikisha inakwisha na kutoa fursa kwa kila kundi kufanya shughuli zake kwa amani na utulivu.
Ukatili dhidi ya watoto
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga alisema kama Tanzania inataka kujenga Taifa la lenye heshima na utulivu ni lazima iwekwe mipango itakayowezesha kila mtu kushiriki kupiga vita vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto.
Akizungumza wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika katika kanisa kuu la Dayosisi hiyo Mjini Lushoto, Askofu Munga aliwataka Wakristo na jamii kwa ujumla kuchukua hatua zitakazowezesha maovu dhidi ya watoto kukomeshwa ikiwamo kupeleka injili kwa makundi yaliyotengwa na kusahauliwa.
Vita ya ufisadi
Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Titus Mdoe aliwataka Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli za kupiga vita ubadhirifu, ufisadi na rushwa.
Akizungumza wakati wa misa ya Pasaka katika Kanisa la Watakatifu wote mkoani Mtwara, Mdoe alisema Rais Magufuli amewaanzishia maisha mapya Watanzania ambayo kila mtu alikuwa anayatafuta.
“Ameonyesha mfano wa kutumbua majipu, basi na sisi tumuunge mkono huku chini, tufanye kazi kama anavyofanya, tusibaki kuwa kama mashabiki wa Simba na Yanga, kila mmoja atimize wajibu wake kwa nafasi yake,” Alisema Mdoe
Kudumisha amani
Katika hatua nyingine, Watanzania wametakiwa kudumisha amani ili kulifanya Taifa liwe na amani ambayo ndiyo siri ya mafanikio katika maendeleo.
Hayo yalisemwa na kasisi kiongozi, mstaafu Canon Moses Subeth wa Kanisa la Anglikana wakati akihubiri ibada ya Pasaka katika Kanisa St John Nzuguni ambako kulikuwa na mkusanyiko wa makanisa mengine.
“Hapa tunatafuta maendeleo, nawasihi sana watu wa Mungu pamoja na viongozi tuendelee kudumisha amani hii na kamwe tusikubali mtu aichezee kwa namna nyingine,” alisema Subeth.
Kauli kama hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa alipowataka waumini kuihubiri amani duniani kote ili kutekeleza agizo la mkombozi wao Yesu Kristo alilowaachia kabla ya kupaa kwake mbinguni.
Waziri akemea rushwa
Katika Kanisa la Mtakatifu Petro, juzi usiku,
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula aliwataka waumini waendelee kuyaenzi yale yote waliyoyapitia wakati wa mfungo.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za rushwa miongoni mwa wabunge, Mabula alisema: “Rushwa ni dhambi hasa kuifanya wakati huu. Naomba uchunguzi ufanywe na watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua zinazostahili.”
Imeandikwa na Julius Mathias, Peter Elias, Matern Kayera, Tumaini Msowoya, Suzan Mwillo (Dar), Sharon Sauwa , Habel Chidawali (Dodoma), Godfrey Kahango (Mbeya), Hamida Shariff (Morogoro), Burhani Yakub (Tanga) na Mary Sanyiwa (Mtwara)
No comments:
Post a Comment