ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 8, 2016

Maalim Seif apumzishwa Hospitali ya Hindu Mandal

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (katikati) akitoka Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam kumjulia hali Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, jana. Picha na Omar Fungo

By Mwandishi Wetu, Mwananchi


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amepumzishwa katika hospitali ya Hindu Mandal jijini hapa baada ya kujisikia vibaya jana wakati akiwasili hapa akitokea Zanzibar.

Taarifa zinaeleza kuwa Maalim Seif alipatwa na hali hiyo baada kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na baadaye kupelekwa moja kwa moja Hindu Mandal kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mara baada ya kulazwa hospitalini hapo kati ya saa 2 na saa 3 asubuhi, viongozi wa CUF na makada walianza kumtembelea kigogo huyo kumjulia hali na kueleza kuwa kiongozi huyo alikuwa akiendelea vizuri.

Mapema saa 4 asubuhi, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jusa alifika hospitalini hapo kumjulia hali Maalim Seif aliyekuwa akiendelea kutibiwa.

“Nimetoka kumuona hali yake mpaka sasa inaendelea vizuri, anapumzika,” alisema Jusa huku akisisitiza taarifa zaidi atazitoa daktari wake.

Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amepatwa na changamoto hiyo ya kiafya zikiwa ni siku nne tangu arejee kutoka nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Saa nne baada ya Jusa kumuona Maalim Seif, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Juma Duni Haji alifika hospitalini hapo na kwenda moja kwa moja alikokuwa amelazwa kiongozi huyo na baada ya dakika 10 alitoka na kueleza kuwa alikuwa anaendelea vizuri.

Vigogo wa chama hicho waliendelea kumiminika hospitalini hapo ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba aliingia saa 10 jioni naye kama watangulizi aliwaeleza wanahabari kuwa “Maalim Seif anaendelea vizuri, amepumzishwa.”

mwananchipapers@mwananchi.co.tz

1 comment:

Anonymous said...

Tunamtakia Maalim Seif buheri ya afya na tunamuomba Mwenyezi Mungu ampe uponyaji wa haraka. Lakini muhimu kukumbuka na kuwa macho sana maana Watanzania hawajasahau hadithi za akina Kolimba na wengine ambazo bado tunazikumbuka. Kuna kitu kinaitwa njia za mkato, watu wanaweza kuamua kuwa "basi bwana na isiwe taabu"