Januari 25, mwaka huu, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitangaza agizo la rais kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili ambao mikataba yao imekwisha.
Mabalozi hao ni Dk. Batilda Buriani aliyeko Tokyo Japan na Dk. James Msekela, aliyeko Rome, Italia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Balozi Sefue alisema siku hiyo mabalozi hao walitakiwa kukabidhi kazi kwa maafisa wakuu au waandamizi ambao wako chini yao.
Hata hivyo, jana Waziri Mahiga alipoulizwa juu ya agizo hilo, alisema kukosekana kwa fedha kumekuwa kikwazo katika kulitekeleza agizo hilo lakini kwa sasa wako katika hatua za mwisho kuhakikisha fedha za kugharamia usafiri, posho na mizigo yao zinapatikana.
Februari 15, mwaka huu, Rais Magufuli aliwateua aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau kuwa mabalozi.
Tarifa ya Ikulu juu ya uteuzi wao iliyotolewa na Balozi Sefue ilieleza kuwa vituo vya mabalozi hao wapya vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.
Lakini Dk. Mahiga alitolea ufafanuzi kuwa mabalozi watatu walioteuliwa na rais wanasubiri kupangiwa vituo vya kazi na kwamba kuwapeleka na kuwarudisha watumishi ni gharama kubwa ambayo inahitaji maandalizi.
“Kuwarudisha mabalozi na watumishi hawa ni gharama kwani wanahitaji marupurupu yao na kusafirisha mizigo na wakati mwingine haikuwa kwenye kasma yetu, lakini watarudi kwa kuwa tumeshapata fedha za kuwagharimia,” alisisitiza.
Hadi sasa vituo sita vya ubalozi viko wazi ambavyo ni London nchini Uingereza, Tokyo (Japan), Rome (Italia) na Brussels (Ubelgiji) kutokana na aliyekuwa Balozi Dk. Deodorous Kamala kuchaguliwa kuwa mbunge.
Wengine ni Kuala Lumpar, Malaysia kutokana na Balozi Dk. Aziz Mlima kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Brasilia, Brazil baada ya Balozi Francis Malambugi kustaafu.
Balozi mwingine aliyerejeshwa nyumbani ni Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe, anayerejea wizarani kupangiwa kazi nyingine.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment