Mshambuliaji Danny Lyanga aliyeingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Brian Majwega aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 72, baada ya kuunganisha mpira uliotemwa na kipa wa Mbeya City, Hannington Kalyesebula aliyepangua shuti la Awadh Juma.
Simba ilijihakikishia pointi tatu muhimu dakika ya 90, baada ya beki wa Mbeya City, Hassan Mwasapili kujifunga mwenyewe wakati akijaribu kuokoa krosi iliyopigwa na Ibrahimu Ajib na kumpita kipa Kalyesebula. Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 48 na kukalia usukani ikifutiwa na Yanga na Azam zenye pointi 47, baada ya kutoka sare 2-2 juzi.
Akizungumzia nafasi ya timu yake katika mbio za ubingwa, Kocha wa Simba, Jackson Mayanja alisema kwa sasa kikosi chake kimekamilika na amejipanga kwa mechi zote zilizobaki.
“Lengo ni kumaliza katika nafasi ya juu zaidi, ushindi huu umetuongezea nguvu kufikia mafanikio hayo, hatukujiandaa kwa ajili ya Mbeya City pekee ila timu zote,” alisema Mayanja.
Katika mchezo huo, kinara wa ufungaji wa Simba, Hamis Kiiza alishindwa kuonyesha makali yake akipoteza nafasi kadhaa za kufunga kama ilivyokuwa kwa kiungo wa Mbeya City, Haruna Moshi ‘Boban’.
Hata hivyo, Mbeya City watajilaumu wenye kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza kushinda mchezo huo.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Kocha wa Simba raia wa Uganda, Mayanja alilazimika kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Majwega, Kiiza na Emery Nimubona kuwaigiza Lyanga, Awadhi Juma na Ramadhan Kessy; wakati mpinzani wake raia wa Malawi, Kinnah Phiri akiwatoa Boban na Ditram Nchimbi na kuwaingiza Themi Felix na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa Simba na kurudi mchezo kwa kugongeana pasi za haraka na kupitisha mashambulizi yao kutokea pembeni kwa Kessy na Mohamed Hussen na kufanikiwa kuifungua ngome ya Mbeya City na kupata mabao yao mawili.
Kocha wa Mbeya City, Phiri alisema wachezaji wake walicheza vizuri makosa madogo katika safu ya ulinzi yamewagharimu.
“Simba ina wachezaji wengi wenye uzoefu, wametumia vizuri nafasi chache walizopata kutufunga,” alisema Phiri.
Simba: Vicent Angban, Emery Nimubona, Mohamed Hussen, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justine Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahimu Ajibu na Brian Majwega.
Mbeya City: Hannington Kalyesebula, Hassan Mwasapili, Abubakar Shaban, Tumba Sued, Haruna Shamte, Kenny Ally, Raphael Alpha, Haruna Moshi, Geofred Mlawa, Joseph Mahundi na Ditram Nchimbi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment